Tuesday, August 6, 2013

CCM NA MADIWANI WAKE TABORA MJINI WAVUTANA UCHAGUZI WA NAIBU MEYA


Ofisi ya CCM wilaya ya Tabora mjini
Na Mwandishi Wetu,Tabora

KUMEZUKA hali ya sintofahamu miongoni mwa madiwani wa halmashauri ya
manispaa Tabora, uongozi wa CCM, baaada ya mwenyekiti wa CCM mkoa wa
Tabora Hassan Wakasuvi kuahirisha uchaguzi wa naibu meya wa manispaa
hiyo.

Uchaguzi huo ulikuwa ufanyike tangu julai 31,2013 ambapo uchaguzi
huo hufanyika kila mwaka na nafasi hiyo hadi uchaguzi huo unafanyika
ilikuwa ikishikiliwa na diwani wa kata ya Ipuli  Bw.Waziri Mlenda.

Hata hivyo licha ya uchaguzi huo kuhairishwa hakuna taarifa yoyote ya
mkoa ilioonyesha ni lini uchaguzi huo utafanyika,lakini imedaiwa kuwa
kuna mipango ya kutaka kuchakachua wagombea wasiotakiwa na baadhi,
vigogo wa mkoa wa Tabora ndani ya CCM na kuweka anayetakiwa.

CCM wilaya ilipendekeza majina ya wagombea ambao ni Musa Msamazi,Salum
Luzila,Shaban Kaombwe,Alfonce Shushi, Waziri Mlenda ambaye imedaiwa
alipata alama mbaya kwenye usahili na Ndaki ambapo CCM wilaya Tabora
mjini ilipanga uchaguzi wake mwezi julai 31 mwaka huu kabla ya
kuhairishwa ghafla.

Baadhi ya madiwani wameudokeza  mtandao huu kuwa mwenyekiti wa CCM
mkoa wa Tabora,Hassan Wakasuvi ameaharisha uchaguzi huo kutokana na kile
kilichodaiwa kuwa kuna mgombea mmoja alikuwa hamtaki huku akimtaka
mwingine ambaye imedaiwa kuwa ndiyo chaguo lake.

Kutokana na hilo baadhi ya madiwani wamesikika wakitamka kuwa ipo siku
CCM Tabora viongozi wake watakiingiza chama kwenye mgogoro usioisha
kwani wamekuwa wabinafsi sana kwenye chaguzi mbalimbali zinapokuja na
kwa maana hiyo wapinzani hasa CHADEMA wanaweza kupata nafasi.

Madiwani hao walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa wapo wagombea wana
ualakini wa vyeti vya shule hali ambayo inapingwa na baadhi madiwani
wakidai ‘wakubwa’ wanawabeba kwa maslahi yao.

Chanzo cha taarifa toka ndani ya CCM mkoa kimesema uchaguzi huo wa
naibu meya wapo viongozi wa CCM mkoa kila mtu ana mgombea wake huku
mstahiki meya wa manispaa Ghulam Remtulah akidaiwa kumbeba diwani wa
Ikomwa Musa Msamazi,lakini Ghalam amekana na kudai hataki kujiingiza
kwenye mgogoro huo.

Wakati hayo yakisemwa mwenyekiti wa CCM mkoa Hassan Wakasuvi amedaiwa
na baadhi ya madiwani kuwa anataka naibu meya wa zamani Waziri Mlenda
arejee kwenye kiti hicho na ndiyo chanzo cha uchaguzi kuarishwa hali
ambayo tayari imerejesha mgogoro wa pande mbili wa madiwani hao.

Aidha taarifa hizo zimesema kuwa CCM mkoa wa iliketi kikao kujadili
majina ya wagombea mwezi julai 24, mwaka huu ambapo pamoja na kubariki
uchaguzi ufanyike licha ya wagombea kadhaa kupewa alama ‘D’ ambayo
kimsingi haina sifa ya kuwa mgombea.

Tayari hadi sasa madiwani hayo wamesema kuwa kuna rushwa inanukia
kwenye uchagzi huo na wametishia kwenda TAKUKURU kushitaki endapo
mizengwe itaendelea ili kuuvuruga uchaguzi huo kwa maslahi ya viongozi
wachache wa CCM.

Akizungumzia shutuma dihdi yake mwenyekiti wa CCM mkoa wa
Tabora,Hassan Wakasuvi alikanusha kuwa na mgombea anayemtaka na kwamba
shutuma hizo zinalenga kumchafua na kumpakazia.

“Sina mgombea ambaye nina maslahi naye wala sijapewa kiwanja wala
fedha….taratibu kadhaa kwa mujibu wa uchaguzi huo hazikukamilika ndiyo
maana tukashauri waahirishe ili kuweza kukamilisha taratibu
hizo.”aliongeza.

Wakasuvi kwa sauti ya mshangao alisema kuhusu baadhi ya wagombea wenye
walakini na vyeti vya shule mamlaka zipo zitachunguza endapo kutakuwa
na umuhimu wa kufanya hivyo lakini chama kama chama hakina mamlaka ya
kufanya hivyo kama vyeti vya wagombea vinavyoonekana kuwa ni sahihi.

Naye mwenyekiti wa CCM wilaya Abdurahaman Moshi Nkonkota ameuambia
mtandao huu kuwa uchaguzi wa naibu meya uliahirishwa jumatano na
anatarajia kukutana siku ya Alhamis kupanga tarehe ya kufanya uchaguzi
huo.

No comments:

Post a Comment