Jeshi la polisi wilaya ya Igunga mkoani
Tabora jana liliwafikisha mahakamani tena makada watano wa Chadema
wanaokabiliwa na kesi ya kummwagia tindikali kada wa Ccm Mussa Tesha na
kusomewa shitaka upya.
Washtakiwa hao waliwasili jana saa 12:45
wakitokea Tabora na kufikishwa mahakamani majira ya saa 1:15 usiku huku kukiwa
na ulinzi mkali wa polisi ambapo wafuasi wa Chadema wakiwa wamefurika
mahakamani.
Akiwasomea shitaka mbele ya Hakimu mkazi
mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Igunga Bw.Ajali Milanzi,mwendesha mashtaka
mrakibu msaidizi wa polisi Cosmas Mboya aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao
wanashtakiwa kwa kosa la kumwagia tindikali Bw.Mussa Tesha mkazi wa Igunga
mjini na kumsababishia maumivu makali mwilini mwake.
Aliongeza kuwa washtakiwa hao walitenda kosa
kinyume na kifungu namba 225 sura ya 16 kanuni ya adhabu iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002,ambapo
aliimbia mahakama kuwa washtakiwa Evodius
Justian mkazi wa Bukoba,Osca Kaijage mkazi wa Shinyanga,Seif Kabuta
mkazi wa
Nyasaka Mwanza,Rajabu Kihawa mkazi wa Dodoma na Henly Kilewo mkazi wa
Dar es
salamu wanakabiliwa na shitaka la kumshambulia na kumwagia tindikali
Bw.Mussa Tesha wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga
mwaka 2011.
Mwendesha mashtaka huyo Bw. Mboya aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao mnamo
septemba tisa mwaka 2011 majira ya usiku maeneo ya msitu wa Hanihani wilayani
Igunga walimmwagia tindikali Tesha mwilini mwake maeneo ya mdomo
,pua,uso na bega la kulia.
Baada ya kusomewa shitaka hilo washtakiwa
wote walikana na wako nje kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya
dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya
shilingi milioni kumi na kesi hiyo imeahirishwa hadi septemba 10 mwaka huu
itakapotajwa tena.
Kwaupande wake wakili anayewatetea washtakiwa hao
watano Bw.Peter Kibatara akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo
alisema kuwa anaishukuru mahakama kuu Tanzania kanda ya Tabora kwa kuonyesha
ujasiri na kutimiza majukumu yake kama ilivyo kwa kufuata haki na sheria.
“Namshukuru jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya
Tanzania kanda ya Tabora Simon Lukelerwa kwa kuwa na weredi wa kutoa uamuzi
ulio sahihi na kwa kufuata haki na sheria kwani ni maamuzi yaliyoshiba pia
naishukuru mahakama ya wilaya ya Igunga kwa kuweza kuwapatia dhamana washtakiwa
kwani ni haki yao muhimu na ya msingi sana”alisema Kibatara.
Aidha mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora
Bw.Kansa Mbaruku alisema kuwa amefurahishwa na maamuzi yaliyotolewa na mahakama
kuu ya Tabora kwani imezingatia sheria kikamilifu.
“Huu ni mwendelezo wa Gharama za haki hivyo
tunaamini wanachadema kuwa katika harakati za kuikomboa nchi hii kuna gharama
zake ambazo ndizo hizi,hivyo sisi hatuwezi kuvunjika moyo na kukosa nguvu
katika kupigania haki za msingi za wananchi na kulikomboa taifa hili kwani lina
rasilimali nyingi lakini wananchi hawanufaiki nazo”alisema Mbaruku.
Awali washtakiwa hao walifutiwa shitaka
lililokuwa likiwakabili la kumwagia tindikali Mussa Tesha katika mahakama hiyohiyo na baadae
kukamatwa tena na kupelekwa Tabora ambapo walisomewa shitaka la ugaidi na baadae
mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Tabora iliwafutia shitaka na kuamuru warudishwe Igunga na kusomewa
shitaka lililokuwa likiwakabili mwanzo la kumwagia tindikali Bw.Tesha.
No comments:
Post a Comment