Wednesday, August 21, 2013

KALIUA HATUTAKIA HATI CHAFU -MWENYEKITI JOHN KADUTU



 
 NA LUCAS RAPHAEL KALIUA

Wataalamu na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya kaliua mkoani Tabora wameaswa  kufanya kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vya ubadhirifu wa mali na fedha za umma ili halmashauri hiyo ipate hati safi wakati wote.

Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,John Kadutu wakati akilihutubia baraza la kwanza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua lililokutana katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Kaliua.

Alisema watumishi hao wanapaswa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuifanikisha  halmashauri hiyo kupata hati safi na sio hati ya mashaka wala chafu kutoka kwa mdhibiti na mkaguzi  mkuu wa hesabu za serikali nchini.

Kadutu amebainisha kuwa halmashauri hiyo haitawavumilia watumishi wazembe na wabadhirifu ambao wataisababisha halmashauri hiyo kushindwa kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

Alibainisha kuwa wafanyakazi hao watakuwa na uhalali wa kuendelea kufanya kazi katika halmashauri hiyo endapo watajituma kufanya kazi kwa juhudi na maarifa jambo ambalo litasaidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili wilaya hiyo mpya.

Kadutu amewataka wakuu wa idara kuweka taarifa zao vizuri na kwa usahihi kila mara na kuondokana na tabia ya ubabaishaji ambao umekuwa ukijitokeza katika halmashauri nyingine na kwamba madiwani hawatokuwa tayari kuburuzwa ili kupokea taarifa za ubabaishaji.

Hata hivyo amemtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kuwasimamia kwa karibu wakuu wa idara na watumishi wengine wa halmashauri hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao na hivyo kuiepusha ubabaishaji.

Aidha mwenyekiti huyo amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kutimiza wajibu wao kwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo na fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali wilayani humo.

Alikemea tabia ya baadhi ya madiwani wanakumbatia maovu kwa kupitisha miradi iliyotekelezwa chini ya kiwango ikiwemo majengo ya idara mbalimbali katika maeneo yao jambo ambalo linapaswa kuachwa mara moja kwa kutofanya kazi kwa mazoea.

Mwenyekiti John Kadutu amekuwa mwenyekiti wa kwanza wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua baada ya kuchaguliwa kwa kura 25 za ndio zilizopigwa na wajumbe 25 wa kikao hicho cha baraza la madiwani.
Halmashuri ya wilaya ya Kaliua imezaliwa kutokana na kuundwa kwa wilaya mpya ya Kaliua kutoka ambapo awali ilikuwa wilaya ya Urambo.

MWISHO


No comments:

Post a Comment