WATUMISHI wa
halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, wametakiwa kujituma katika
utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zote za kimaendeleo zinazofanyika
katika idara zao.
Rai hiyo
imetolewa na mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu, alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la
madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo
kilichofanyika mjini Sikonge.
Akizungumza
katika kikao hicho, Selengu alisema huu ni wakati wa kila mtumishi kutekeleza
majukumu yake ipasavyo ili kufanikisha mpango wa maendeleo ulioidhinishwa
katika vikao mbalimbali vya halmashauri hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha kila
mradi uliokusudiwa utekelezwe na kufanikishwa.
‘Huu ni wakati
wa matokeo makubwa sasa (BIG RESULTS NOW!), hatuhitaji kuendelea kusukumana
sukumana katika utendaji…..kila mmoja
anatakiwa kujituma anapotekeleza majukumu yake , hili sio suala la
kubembelezana, watumishi walio wengi
wanafanya kazi kwa kusukumwa sukumwa kwanza, nataka kila mtu afanye kazi yake
kama inavyopaswa, alisema Selengu.
Aidha,
Selengu alisema uzembe unachangia baadhi
ya watendaji wakuu wa idara kushindwa
kusimamia vyema ufanisi wa miradi ya
maendeleo iliyoko chini ya idara zao hali ambayo imekuwa ikisababisha miradi
hiyo kuwa na mapungufu kadha wa kadha ikiwemo kutokamilika kwa wakati
uliopangwa.
‘Kuanzia
sasa tunataka matokeo ya kila kazi inayofanyika yaonekane …..tunataka matokeo
makubwa sasa sio kesho!’ alibainisha.
Akizungumzia
hali ya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo, Selengu alivitaka vikundi vyote
vya sungusungu kushirikiana kwa karibu zaidi na jeshi la polisi ili kudhibiti
uharifu na mauaji ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo mbalimbali ya
wilaya hiyo hususani katika kata ya Kipili.
Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya hiyo Shadrack Mhagama, akizungumzia hali ya utendaji, alisema
idara zote ambazo zimeonekana kuwa na mapungufu kadha wa kadha, wakuu wake
wametakiwa kurekebisha kasoro hizo mara moja kama zilivyoainishwa katika
taarifa ya mkaguzi wa hesabu za ndani .
‘Tumebaini mapungufu
yaliyopo yanasababishwa na kasoro za kiutendaji katika idara husika, hivyo
tukiyafumbia macho yatatuharibia utendaji mzima wa halmashauri na hatimaye
kupata hati mbaya kutoka kwa wakaguzi, ni lazima mapungufu haya tuyakomeshe’,
alisema Mhagama.
Aidha
Mhagama aliongeza kuwa watendaji wote wa idara zenye mapungufu
watatakiwa kutueleza ni kwa nini mapungufu hayo yamejitokeza katika
idara zao na sababu zilizochangia mapungufu hayo.
No comments:
Post a Comment