Sunday, February 17, 2013

BUNGE LA KIKOMONIST LAZINDULIWA HUKO DODOMA

 

 

2-wakipinga  3a972
Bunge la Kikomunist Lazinduliwa
Huko Dodoma
Ni habari za kusikitisha na kuhuzunisha kuona kwamba taratibu za ukomunist ambao ulipigwa marufuku kote duniani mwaka 1991 leo hii bunge letu limezindua mikakati ya kuliendesha bunge kwa kutumia taratibu za kikomunist! 

Baadhi ya makala zangu za nyuma nimewahi kuelezea kwamba moja ya silaha zinazotumiwa sana na wakomunist ni kutengeneza mazingira ya usiri kati ya watawala na watawaliwa, kwa vile watawal;a siku zote hawapo sahihi na wala hawajiamini mbele ya watawaliwa ambao ndiyo wananchi waliowaweka madarakani.
 
Wakomunist wanapangiwa waseme nini!? Waende wapi na wapi wasiende!? Wavae nini na nini wasivae!? Wale nini na nini wasile!? Wafikiri juu ya nini nakadhalika!

Siamini kwamba katibu wa bunge Dr. Thomas Kashililah alitafakari kabla hajaozungumzia hoja yake ya kutaka vikao vya bunge visirushwe moja kwa moja, nasema hivyo kwa vile sababu alizozitoa si sababu za kimsingi wala hazileti fikirishi kwa mtu yeyote anayejua maana bunge ni nini, na nani mwenye mamlaka na bunge!? 

Bunge ni mali ya umma, na umma ndiyo unalichagua bunge na kama umma ndiyo unalichagua bunge sioni sababu ya kuwafungia wabunge wasionekane au wasisikike wanachokiongea kwa kisingizio cha kukiuka maadili na kanuni za bunge!

Tena ni vizuri wabunge wanapopigana wananchi waone ili wajue kinachowapiganisha ni kitu gani? Kinachowapiganisha kinalenga maslahi ya umma au binafsi; wananchi wanataka kuona ni mbunge gani yupo tayari kupigana na hata kung’olewa meno kwa ajili yao! Hivyo npyo tunavyowapima wabunge wale wanaojitoa muhanga kwa ajili yetu, na pia kuwaona wale wanafiki wakisimama majukwaani wanatoa ahadi za uongo kwamba watasimamia haki lakini wakiingia bungeni ni waoga hata kunyosha kidole wanaogopa!

Wabunge kupigana bungeni ni jambo la kawaida kwa mabunge mengi duniani, tumewahi kushuhudia wabunge wa Uingereza, Urusi, Ukraine, Marekani, Brazili na kwingineko wabunge wakishindana kuhusu hoja na kuishia kurushiana matusi na mwishowe kupigana, hivyo na sisi tusione kitu cha ajabu wabunge kupigana, kwa vile kupigana kwa wabunge ni ishara ya kukua kwa democrasia. 

Ukikuta bungeni hakuna mizozo wala mivutano ya hoja, basi jua kwamba hakuna democrasia na bunge hilo ni bunge la mwelekeo mmoja.

Sababu alizotoa katibu wa bunge Dr. Thomas Kashililah za kwamba wabunge wanawake wanapojua kwamba watatoa hoja, huwa wanakuja wamevaa vizuri na kujipodoa akiitumia sababu hii kama kigezo cha kutorusha matangazo moja kwa moja; mimi naoni hii ni sababu isiyokuwa na msingi kwa vile mwanamke hata akienda gengeni kununua nyanya ni lazima ajipodoe! Sasa unataka akiingia bungeni awe amevaa ovyo ovyo wakati anaenda kusikilizwa na waajiri wake ambao ni wananchi! 

Wakimuona amevaa ovyo ovyo na hakujipodoa si wananchi
watamnyima kura uchaguzi ujao!?

Dr. Thomas Kashililah anaposema baadhi ya wabunge wanapochangia hoja huwa
wanazungumza mpaka mishipa inatoka, hivyo anataka kuitumia hoja hii kama sababu ya vikao vya bunge kutorushwa moja kwa moja; pia hii si sababu ya msingi ambayo inaweza kutolewa na katibu wa bunge; bungeni ndipo sehemu pekee ya kuonyesha umahiri wa kuongea kwa vile bungeni ni jukwaa pekee linalotambuliwa kikatiba katika kutetea maslahi ya umma; na kama mbunge atalitumia jukwaa hili kwa manufaa yake wewe muache tu kwa vile sisi wananchi tupo macho tunamuangali moja kwa moja kupitia runinga zetu. 

Akizidisha umimi 2015
tutampumzisha!
Dr. Thomas Kashililah anaposema waandishi wa habari wanampiga picha spika akiwa ameinama au amelala bungeni, na akitaka kukitumia kigezo hichoi kama kuunyima umma wa watanzania kutoshuhudia bunge lao ambalo wameliajiri na kuliruhusu kutumia kodi zao, pia ni sababu ambayo haina msingi na kulingana wadhifa aliokuwa nao katibu wa bunge hakustahili kutetea sababu kama hiyo, kwa vile bungeni ni jukwaa la kujadili matatizo ya wananchi na wala siyo sehemu ya kulala au kupumzika; 

kama spika analalalala bungeni inaonyesha hatekelezi wajibu wake kikamilifu na kama ndiyo hivyo ni kwanini bunge lisimuwajibishe!?

Bwana Kasililah anataka aturejeshe nyuma kwenye zile enzi za giza la kikomunist ambapo wabunge walikuwa wanajifungia na kuongea mambo waliyotaka na baada kuyachambua yale tuliyostahili kuyasikia na kutangaziwa kwa njia ya redio, na yale tusiyostahili walibaki nayo wenyewe! Bunge la kikomunist hupangiwa uvae nguo gani!? uulize swali gani!? utoe jibu gani!? mwandishi wa habari apige picha gani au akaandike kwenye gazeti kitu gani!? 

Huu ndiyo utaratibu wa mabunge ya kikomunist yalivyokuwa enzi hizo, sasa wewe na uelewa wako unataka uwarudishe watu kizani kwa maslahi yako binafsi, hatutakubali kwa hilo hata siku moja. 

Wewe waache wabunge wafanye wafanyavyo sisi ndiyo waajiri wao ukifika muda wa kusitisha ajira zao tutafanya hivyo mara moja, wewe tunachokuomba ukiona spika amelala na huku bunge linaendelea mwamshe ili azinduke usingizini asije akaidhinisha sheria za maangamizi!

Dr. Noordin Jella (Ph.D. in Economics)
Former Lecturer of Mzumbe, Open & KIU – Dar, Universities.
Currently: Freelance Journalist & Seasonal Political
Analyst
Email: norjella@yahoo.com
Mobile: +255 782 000 131

No comments:

Post a Comment