Friday, February 1, 2013

MWANASHERIA AWATAHARISHA KIDATO CHA SITA NA NDOA ZA UTOTONI


 Mwanasheria wa kujitegemea Bw.Emmanuel Mwasaka akitoa cheti kwa mhitimu wa kidato cha Sita katika mahafali ya Shule ya Sekondari ya Tabora Wasichana ambapo Bw.Mwakasaka alikuwa mgeni rasmi.
 Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tabora Wasichana Bi.Helen Makala akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika katika shule hiyo. 
 Baadhi ya watumishi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Tabora Wasichana wakiwa katika mahafali hayo.
 Wahitimu wa kidato cha Sita Shule ya Sekondari ya Tabora Wasichana wakiimba nyimbo ikiwa ni sehemu ya mahafali.


Na Lucas Raphael-Tabora

Mwanasheria wa kujitegemea nchini Bw.Emmanuel Mwakasaka amewatahadharisha  wahitimu wa kidato cha Sita  na suala la ndoa za utotoni kwakuwa zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya kutaka kujiendeleza zaidi  kielimu.

Akizungumza katika mahafali ya kidato cha sita Shule ya Sekondari ya Tabora wasichana Bw.Mwakasaka ambaye pia ni mdau wa maendeleo mkoani Tabora,alisema ipo haja kwa wahitimu hao kuwa na mtazamo wa kuendelea zaidi na masomo kuliko kufikiria kuolewa wakati huu wakiwa na umri mdogo jambo ambalo huenda likawatia kwenye matatizo katika maisha yao.

Alisema maisha ya sasa yamekumbwa na changamoto nyingi ambapo kwa sehemu kubwa ya maisha yanahitaji kujitosheleza zaidi kielimu ili kuweza kuyamudu.

''Hivi sasa jamani mtakuwa katika kipindi kigumu sana wakati huu mnapokwenda majumbani kwenu,changamoto ni nyingi hasa mbaya zaidi kwa ninyi mnaokwenda vijijini,maana huko si ajabu mnaweza kuwa wazazi au walezi wenu wamekwisha chukua fedha kwa ajili ya kuwaozesheni"alisema Mwakasaka.

Hata hivyo Bw.Mwakasaka pamoja na kuahidi kusaidia komyuta tatu,Projekta moja na Jenereta moja katika Shule hiyo alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi wanaobaki Shuleni hapo kuona umuhimu wa masomo ya Sayansi ambayo kimsingi alidai kuwa yamekuwa yakitoa ajira kwa wingi kuliko masomo mengine ulimwenguni.

Kwaupande wake mkuu wa Shule hiyo ya Tabora Wasichana Bi.Helen Makala katika risala yake kwenye mahafali hayo alisema kukosekana kwa uzio katika Shule hiyo ni moja ya changamoto kubwa na ni tishio kwa maisha ya wanafunzi hao wakike.

Alisema licha ya Shule hiyo kufanya vizuri lakini wanafunzi wamekuwa wakiishi katika mazingira ya wasiwasi kutokana na vibaka kuvamia mara kwa mara na kuiba nyakati za usiku.

"Shule hii ina eneo la hekta 97.4 hakuna uzio wowote hata wa kuzunguuka eneo dogo linalozunguuka majengo,mazingira haya ni hatarishi zaidi kwa wanafunzi wa kike wakiwemo albino na wasioona"alisema mkuu huyo.

Aidha Shule ya Tabora wasichana ambayo ni ya bweni ilianzishwa mnamo mwaka 1928 ikitajwa kuwa baadhi ya viongozi wakubwa wanawake  wa serikali ya Tanzania wamesoma katika shule hiyo ambayo kwasasa inajumla ya wanafunzi wapatao 610. 
 

No comments:

Post a Comment