Sunday, February 10, 2013

HATUJAWAHI KUKAA KIKAO CHA KISHERIA KUPENDEKEZA KUWASIMAMISHA AMA KUFUKUZWA KAZI WATUMISHI



NA LUCAS RAPHAEL,TABORA


BARAZA la madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Tabora,limemjia juu mkurugenzi wa manispaa hiyo Sipola Liana, kwa madai kuwa hawakuwahi kukaa kikao chochote na kupendekeza kusimamishwa ama kufukuzwa kazi, kwa watumishi watano wa manispaa hiyo kwani taratibu zimekiukwa.

Kauli hiyo ya pamoja ilitolewa leo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo.

Wakichangia kwa nyakati tofauti,madiwani hao walisema mapema mwezi agosti 27,mwaka 2012,waliletewa taarifa kuwa watumishi watano wa manispaa hiyo wamesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Aidha waliongeza kuwa kwenye kikao cha baraza hilo,walijulishwa na ofisi ya mkurugenzi kuwa kuna tume itaundwa na mkuu wa mkoa wa Tabora,Fatma Mwassa,kuchunguza ukweli wa tuhuma zinazowakabili huku barua za kusimamishwa kwao zikisomeka kuwa 

“wamesimamishwa kazi kwa kutokutimiza majukumu yao”.
Waliongeza kuwa toka wamesimamishwa kazi hadi sasa muda wa kisheria ulishapita kuundwa tume na zaidi hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na ofisi ya mkurugenzi juu ya hatua iliyofikia ya kuundwa tume hiyo.

Aidha waliongeza kuwa wao kama madiwani wameona mbele yao kuna hatari ya halmashauri kufikishwa mahakamani  kwani wanaotuhumiwa na kusimamishwa kazi hawakuwahi kupewa hati za mashitaka,kabla ya kusimamishwa na hadi leo hakuna cha tume wala nini.

Walisema kusimaishwa kazi kwa watumishi hao,mchumi wa manispaa Charles Mduma,afisa ardhi mteule Charles Mkalipa,kaimu afisa utumishi Joyce Masoga,mweka hazina Grace Manwinkwi na mhandisi wa manispaa Siraji Mbuta taratibu za utumishi kuwasimamisha hazikufuatwa.

“Tunachoona hapa vitu vinaamuliwa tu bila ya madiwani kukaa kwenye vikao halali vya kisheria kwani hatujawahi kupeleka mapendekezo yoyote TAMISEMI, juu ya kile kinachodai ni tuhuma za watumishi hao tumeletewa taarifa tu kuwa wamepewa barua za kusimamishwa……hatujawahi kukaa kikao chochote kuwasimamisha kazi tunakana kwa kauli moja.” Walisema.

Waliongeza kuwa mapema mwezi novemba 7,mwaka 2012 walisikia kuwa mkurugenzi wa manispaa Tabora Sipola Liana,amewaandikia barua watumishi waliosimamishwa kazi ikisema “wanapumnzishwa kazi kwa muda kupisha uchunguzi” hali ambayo wao kama madiwani hawakukaa kikao chochote kujadili na kupendekeza.

“Barua zote mbili ziliandikwa na mkurugenzi bila sisi kukaa vikao kuamua hayo yaliyoandikwa sasa leo hakuna kinachoendelea hakuna taarifa ya tume iliyoundwa wala hakuna majibu yoyote ya kusimamishwa kazi kwa hawa watumishi hii maana yake nini na tayari kuna kila dalili za halmashauri kufikishwa mahakamani kwani taratibu za utumishi zilikiukwa” walisema.

Walisema ikibidi kuwatetea ili kuinusuru manispaa hiyo kwani vitu vinaamuliwa kienyeji tu halafu hakuna mrejesho wowote hadi sasa hizo barua ziliandikwa kwa idhini ya vikao gani na kwamba afisa ardhi mteule,Charles Mkalipa, yeye ndiye anayesaaini baadhi ya faili sasa maamuzi yake yamesimama nani anafanya kazi hiyo.

Akijibu hoja za madiwani hao mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Sipola Liana alisema yeye baada ya kufika kwenye kituo cha Tabora,alikuta barua ya kusimaishwa kazi kwa watumishi hao, na aliona kuna makosa makubwa yaliyopo na hivyo aliamua kuandika barua upya za kuwapumzisha kazi kwa muda badala ya ile ya mwanzo ya kuwasimamisha kazi.

Kuhusu uchunguzi alisema tayari ulishaanza na hati za mashitaka walishapewa na wamejibu  utetezi wao na hivyo ofisi yake imeshamwandikia katibu tawala(RAS),Kudra Mwinyimvua ili tume hiyo iletwe na inaweza toka mkoani ama TAMISEMI.

Mwisho-


No comments:

Post a Comment