Na Lucas Raphael,Tabora
MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya -NHIF, umedhamiria kujenga jengo la kitega uchumi
mkoani Tabora litakalokuwa na ghorofa sita.
Hayo
yalibainishwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Rehan Athuman katika
semina ya wadau mbalimbali wa mfuko huo iliyofanyika juzi katika ukumbi wa
Mtemi Isike Mwana Kiyungi mkoani humo.
Alisema
NHIF imekusudia kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa
wanachama wake hapa nchini na katika siku za usoni mfuko huo una mpango wa
kujenga jengo la kisasa katika mkoa wa Tabora litakalokuwa na ghorofa sita ili
kurahisisha utoaji huduma.
Aidha
alisema mfuko huo umedhamiria kuboresha na kupanua wigo wa utoaji huduma za
afya katika mikoa yote hapa nchini ili wanachama wake waweze kujivunia ubora wa
huduma hizo sambamba na kusajili wanachama wapya kwa wingi zaidi.
Ili
kuboresha huduma za mfuko wa afya ya jamii mkoani Tabora na kusogeza huduma
hizo karibu na wananchi NHIF inakusudia pia kujenga jengo la kituo cha
matibabu katika Manispaa hiyo kwa lengo la kupanua wigo wa huduma hizo.
‘Mikoa
mingi hapa nchini ina upungufu wa vituo vya afya, zahanati na hospitali kubwa,
ndio maana tumeona ipo haja ya kujenga kituo hicho cha matibabu mkoani hapa
kama ambavyo tumedhamiria kufanya katika mikoa mingine pia’, alisema.
Aidha
aliuomba uongozi wa serikali ya mkoa huo kushikamana na kuongeza hamasa kwa
wananchi ili waweze kujiunga na kufaidi huduma mbalimbali za kiafya zitolewazo
na mfuko huo.
Mkuu
wa Mkoa huo Fatma Mwassa na Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa hiyo Alfred Luanda
walimhakikishia kuwa Manispaa hiyo iko tayari kushirikiana na mfuko huo
sambamba na kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi na kituo
cha matibabu kama mfuko huo ulivyokusudia.
Luanda
aliwataka viongozi wote katika Manispaa hiyo kubadilika kiutendaji kwa kuongeza
ufanisi katika kazi zao badala ya kuendekeza malumbano yasiyokuwa na tija ili
kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika Manispaa hiyo.
‘Manispaa
yetu haishindwi kusajili idadi kubwa ya wanachama katika mfuko wa afya ya
jamii-CHF, kinachotakiwa ni kubadilika tu kiutendaji na kuanza upya
uhamasishaji wa wananchi’, aliongeza.
Katika
mkutano huo wajumbe walipendekeza kiwango cha mchango wa kujiunga katika huduma
hizo za mfuko wa afya ya jamii kwa mwaka kiwe shilingi 10,000 kwa kichwa,
gharama ambayo itamwezesha mhusika kupata huduma za afya katika kituo chochote
kile mkoani humo kwa kutumia kadi maalumu ya tiba.
Mwisho
|
Friday, January 17, 2014
NHIF’ KUJENGA JENGO LA KITEGA UCHUMI TABORA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment