Mbunge wa jimbo la Tabora mjini Mh.Ismail Aden Rage |
Baadhi ya wananchi mjini Tabora wamekiomba chama cha mapinduzi kimtayarishie mbunge wa jimbo la Tabora mjini Bw.Ismail Rage mkutano wa hadhara ambao utawawezesha kumuuliza maswali mbunge huyo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ahadi alizozitoa yeye kama mbunge wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara aliyouitisha Mbunge wa vitimaalum mkoa wa Tabora Bi.Munde Tambwe kata ya Gongoni manispaa ya Tabora,walisema wamekuwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona mbunge wao akiitisha mikutano ili waweze kupata fursa ya kuuliza maswali lakini imekuwa ni vigumu kwa kile walichodai wamekuwa wakiambiwa ana majukumu mengine ya kitaifa kwenye kamati za Bunge anazozitumikia.
Mmoja kati ya wananchi hao aliyezungumza na mtandao huu,Ali Maganga alisema watu wanashangazwa na mbunge wetu Bw.Rage kutofanya mikutano ya mara kwa mara pindi anapotoka bungeni ili aweze kuchukua maoni na hoja zetu aziwasilishe huko kama ilivyoada ya madaraka aliyoyaomba lakini sasa imekuwa kinyume kabisa huku akimtaja mbunge wa vitimaalum Bi.Munde amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara na kuonekana yuko karibu zaidi na wananchi kuliko mbunge mwenye jimbo lake.
''Sasa kama CCM wameliona hilo ni vema wamlazimishe afanye mkutano na wananchi na tena siku hiyo asiseme chochote maana mengi aliyozungumza bungeni tunayajua yanafanywa na Serikali kuu na wala si yeye,tunachotaka ahadi alizotuahidi,Mbona wabunge wengine wanatoa ahadi na kutekeleza mfano huyo Munde kila alichoahidi anafanya"alisema Maganga
"Mimi ni mwana CCM damu,kwakweli tangu mbunge wetu tumchague nimeona mkutano mmoja tu wa kwake na siku hiyo alikuwa anatoa hundi za mfuko wa jimbo na wala si fedha zake za mfukoni kama wanavyofanya akina Lowassa,Sitta,Mkono,Komba na wengineo"Maganga alizidi kusisitiza.
Hata hivyo kumekuwa na taarifa kutoka CCM Tabora kuwa mbunge wa jimbo la Tabora mjini Bw.Ismail Rage ameandaa mikutano kadhaa ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kushika wadhifa huo jambo ambalo pia linatafsirika kuwa limekuja dakika za majeruhi kwa kile kinacholinganishwa na wakati alipochaguliwa mwaka 2010 hadi sasa 2014 muda ambao umebakia takribani mwaka mmoja kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine.
Wananchi ambao bado wanashauku kubwa la kutaka kumhoji mbunge wao Bw.Rage kupitia mikutano ya hadhara kuhusu yale anayowasilisha bungeni kuwa ametumwa na nani na hivyo kuendelea kukosa fursa hiyo ni wazi kwamba wanaendelea kukijengea chuki chama cha mapinduzi kwa kushindwa kumbana mbunge huyo kutofanya mikutano ya mara kwa mara.
''Matokeo yake ndio kama hivi tunamuona kwenye mkutano uliondaliwa na Mbunge mwenzake na tunapotaka kumuuliza maswali watu wakishangilia wanasema eti tunamzomea,ukweli unabaki pale pale mbunge wetu anahoja za kujibu kwetu vinginevyo chama hakitutendei haki sisi kama wananchi"alisema Nassor
Mbunge wa jimbo la Tabora mjini Bw.Rage pamoja na malalamiko hayo yanayotoka kwa wananchi na kukiweka CCM kwenye nafasi ngumu hasa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na hatimaye uchaguzi mkuu wa 2015 ameanza kuwa karibu na wananchi na hata hivi majuzi aliwatembelea wananchi waliokumbwa na mafuriko huko kata ya Malolo hatua ambayo baadhi ya wananchi wanaitafsiri kuwa ni kukumbuka shuka wakati kumekucha.
No comments:
Post a Comment