Askari Polisi wa
kituo kidogo cha Tarafa ya Ulyankulu wilayani Kaliua mkoani Tabora wamemuua kwa
kumpiga risasi begani kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la John Joseph(28) kwa tuhuma
za kuleta vurugu na kutaka kuchoma
moto Kituo hicho cha
Polisi,wakiwashurutisha askari hao kumwachia
mtuhumiwa mmoja wa wizi
wa ng’ombe ili waweze kumwadhibu wenyewe.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Peter Ouma
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amelieza mtanzania kuwa marehemu
John Joseph juzi majira ya saa tano asubuhi akiwa na wananchi wengine
walimkamata kijana mmoja Shija Matenga(23)kwa
tuhuma za kuiba ng’ombe watano huko wilayani Kasulu mkoani Kigoma ambaye
aliwaswaga hadi eneo la Ulyankulu wilayani Kaliuawa ambako alikamatwa na kuanza
kupigwa.
Ouma alifafanua kuwa
wakati kundi la wananchi hao ambao
miongoni mwao akiwemo
marehemu Joseph wakiendelea kumshambulia mtuhumiwa huyo wa wizi wa mifugo Shija
Matenga,askari Polisi wa
kituo hicho cha
King’wangoko kilichopo tarafa ya
Ulyankulu chini ya uongozi wa mkuu wa
Kituo hicho namba E.1295 D/SGT
KIMOLA walipata taarifa hiyo na
hivyo askari wawili waliagizwa kufika
eneo la tukio kujaribu kuwazuia wananchi
hao ambao tayari walikwisha mfunga kamba mtuhumiwa huku wakikusanya majani kwa
lengo la kutaka kumchoma moto.
Kwa mujibu wa Kamanda Ouma baada ya askari hao
kufanikiwa kumuokoa mtuhumiwa
walimfikisha kituoni wakati kundi
la wananchi hao likiwafuatilia
kwa nyuma wakiwa wanawarushia mawe,chupa na fimbo askari
Polisi hao ambao nao wakalazimika kujikinga kwa kufyatua risasi iliyompata John
Joseph begani na hatimaye kufariki dunia hatua chache
kutoka Kituoni hapo.
Katika sakata hilo lililodumu kwa muda mfupi Malembeka Matemele(22)ambaye ni mkazi wa
Ulyankulu alipigwa risasi paja la mguu wa kulia huku kamanda Ouma akimtaja kuwa
ni mmoja kati ya vinara wa vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya mtu mmoja.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wa tarafa ya Ulyankulu ambao
hawakutaka majina yao yatajwe hadharani wamelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa
kufanya mauaji hayo ya raia asiyekuwa na hatia.
Wamesema wakati wa purukushani hizo zikiendelea
marehemu John alipigwa risasi akiwa anatokea nyumbani kwake hatua ambayo
wamelitafsiri tukio hilo kuwa ni la kinyama na huku wakiziomba taasisi
zinazotetea haki za binadamu kufuatilia na kuchunguza ukweli wa tukio hilo la
maonezi.
No comments:
Post a Comment