Viongozi wa Chama cha Msingi cha wakulima wa Tumbaku Kisanga, kutoka kushoto ni mwenyekiti wa chama hicho Rashid Mazinge akifuatiwa na diwani wa kata hiyo Abdallah Msumeno (Picha na Alan Mtana) |
CHAMA Cha Msingi cha Wakulima wa Tumbaku katika kata ya Kisanga
wilayani Sikonge mkoani Tabora kimetenga sh 5,100,000 za mauzo ya
tumbaku kwa msimu wa 2013/2014 kwa ajili ya kutunisha mfuko maalumu wa
kuweka umeme katika kata hiyo yenye vijiji 3.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Rashid Mazinge, katika
taarifa yake kwa waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho wiki
iliyopita.
Alisema chama hicho chenye jumla ya wanachama 700 kimekusudia kuweka
umeme katika makao makuu ya kata hiyo yaliyoko katika kijiji cha
Kisanga na vijiji vyake na kwa kuanzia wameanzisha mfuko maalumu wa
umeme kwa ajili ya kutimiza lengo hilo.
Aidha alisema wametenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya maandalizi
ya awali ambapo wataanza kwa kununua vifaa mbalimbali vya umeme
ikiwemo vifaa vya komputa na printa vitakavyosaidia kurahisisha
shughuli mbalimbali za ki-ofisi katika ofisi ya chama hicho, tayari
komputa kadhaa zimeshanunuliwa.
‘Ndugu waandishi wa habari, tumekusudia kuweka umeme katika kijiji
chetu ndio maana tumeanza kukusanya fedha na kuzitunza kama
wanakikundi, mda si mrefu tutaenda wilayani kufuatilia taratibu
zingine, tunaomba na ninyi mtusaidie huko wilayani ili tufanikiwe
haraka’, alisema.
Alibainisha kuwa chama kimefikia hatua hiyo baada ya kupata mafanikio
makubwa katika msimu wa 2012/2013 na 2013/2014 hali iliyowafanya
wanachama wake kwa kauli moja kuridhia haja ya kuanzishwa mfuko huo
ili kujiletea maendeleo katika kata hiyo yenye vijiji 3 (Utyatya,
Mwamayunga na Kisanga).
Katika msimu wa 2012/2013 chama hicho kilizalisha jumla ya kilo
940,049 za tumbaku zenye thamani ya Dola za kimarekani 2,538,132 (sawa
na sh bil 4.1) na mapato ya ushuru yalikuwa dola za kimarekani 65,000
(sawa na sh mil 103.4), kwa mapato hayo waliweza kulipa deni la
pembejeo la dola 692,000.(sawa na sh bil 1.1) kutoka benki ya NMB na
kubakiwa na fedha ya kutosha.
Aidha katika msimu wa 2013/2014 walilenga kuzalisha jumla ya kilo
1,400,000 zenye thamani ya Dola 3,920,000 sawa na sh bilioni 6.3 na
mapato ya ushuru walilenga kukusanya dola 98,000 sawa na sh mil 156.8
hali ambayo itawawezesha kulipa deni la pembejeo dola 968,000 sawa na
sh bil 1.5 toka NMB.
Alitaja mafanikio ya chama hicho kuwa ni kuanzishwa mfuko wa ujenzi wa
ghala la kuhifadhia tumbaku ambao umetengewa kiasi cha Dola 31,000 (sh
mil 49.3), ujenzi wa ofisi ya kata ambapo chama hicho kimechangia sh
mil 3, kuanzisha mfuko wa umeme, kuanzisha KISANGA SACCOS LTD ambayo
mpaka sasa ina jumla ya Dola 21,000 (sawa na sh mil 33,495,000).
Alisema chama hicho kimedhamiria kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo
kupitia vikao mbalimbali vya wanachama wake ambapo kimetenga sh
milioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa gari aina ya FUSO ili kurahisisha
huduma mbalimbali za wakulima kijijini hapo, pia kimekusudia kukusanya
Dola 84,000 (sh mil 134,000,000) ili kuongeza nguvu ya SACCOS yao.
Pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto kadhaa zinazowakabili ikiwemo
mikopo na bei kubwa za pembejeo, ucheleweshaji na upatikanaji wa
pembejeo hizo, kutokuwa na umeme, ubovu wa barabara zinazounganisha
vijiji hivyo, ukosefu wa maji safi na salama, ukosefu wa nyumba ya
mganga wa zahanati na kituo cha polisi.
Diwani wa kata hiyo Abdallah Msumeno mbali na kupongeza hatua ya chama
hicho kutenga sh mil 2 kwa ajili ya kununua viti 100 vya plastic na
kutenga sh 576,000 za michango ya wanachama katika mfuko wa NSSF pia
ametoa wito kwa wakulima hao kufuata kalenda ya msimu wa kilimo ili
kupata mafanikio zaidi.
No comments:
Post a Comment