Friday, June 27, 2014

SUMATRA TABORA YAJIPANGA KUELIMISHA ABIRIA JUU YA HAKI ZAO WAWAPO SAFARINI




 
NI DHAHIRI abiria walio wengi hawajui haki zao ni zipi wanapokuwa safarini na hata ajali inapotokea au gari kuharibika au kukatishwa safari kabla ya kufika mwisho wa safari iwe kwa usafiri wa majini au nchi kavu hawajui haki zao ni zipi au wafanye nini.

Kwa mantiki hiyo Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini  ( SUMATRA) mkoani TABORA  imedhamiria  kutoa elimu ya matumizi bora ya vyombo vya usafiri na haki za abiria wanaotumia vyombo hivyo.

Afisa  mfawidhi  wa SUMATRA mkoani Tabora  Joseph  Michael  anabainisha kuwa mamlaka hiyo imeamua kuchukua hatua hiyo ili kupunguza kero mbalimbali zinazowakabili watumiaji wa vyombo hivyo vya moto ambazo zinapelekea wengi wao kupoteza haki zao za msingi ikiwemo kupoteza mali, kupata ulemavu au kifo.

Michael anaongeza kuwa kama watumiaji wa vyombo hivyo watakuwa na  uelewa wa kutosha juu ya haki zao na uelewa wa sheria na kanuni za usalama wa barabarani ajali na misuguano kati ya abiria, makondakta au mwenye chombo itapungua kwa kiasi  kikubwa.

Aidha  anasema katika  mwaka  wa fedha  wa 2014/2015 SUMATRA imeweka  mkakati wa  kutoa mafunzo kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri ili wasafiri hao waweze kujua wajibu na haki yao ya kupata taarifa mbalimbali pindi wanapokuwa safarini.

Anasema kama wasafiri hao wakijua haki zao pindi wanapokuwa safarini watakuwa na uwezo wa kugomea chombo hicho cha usafiri  pale watakapoona hakina vigezo vya kusafirisha abiria  pia watakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya nauli stahiki wanazostahili kulipia ambazo pia  zimeidhinishwa na SUMATRA.

Haki za abiria safarini;
Akifafanua baadhi ya haki za msingi kisheria kwa watumiaji vyombo vya barabarani kwa mujibu wa mamlaka hiyo, Michael anasema;

Abiria ana haki ya  kurudishiwa nauli yake chombo cha usafiri kinapochelewa kuanza safari saa mbili baada ya muda uliopangwa kwenye ratiba na tiketi (kanuni No.21-(2)),  pia ana haki ya kupewa tiketi  ndani ya ofisi ya  mtoa huduma ya usafiri husika na siyo  vinginevyo (kanuni ya  17- (1p ) na ya 24–(1 ).

Anataja haki nyingine kuwa ni kutonyanyaswa au kutumia lugha  za matusi au vitendo vyovyote kinyume na taratibu au kwa mujibu wa haki za binaadamu iwe kwa abiria  mtu mzima au mwanafunzi kama kanuni ya 18-(1a,g,h ).

 Haki nyingine ni ya kufikishwa mwisho wa safari yaani kituo husika anakoelekea abiria (kanuni ya 18-(1d), haki ya kutosimamishwa ndani ya chombo cha usafiri hasa kwa mabasi ya mikoani   awapo  safarini  (kanuni 17- 1f) ), Haki  ya kulipa nauli   iliyoidhinishwa  na mamlaka  ya  SUMATRA na  si zaidi  ya  kiwango husika   (kanuni ya 34-1, 2, 3) ).

Haki ya  kutoendeshwa na dereva mmoja (kwa mabasi ya mikoani ) zaidi  ya saa nane (kanuni ya 17-1g), kulindwa kwa mikanda ya usalama  (Passengers seat belt ) wakati wote wa  safari (kanuni ya 17-1i ), kupata huduma muhimu  za usafiri, afya na taarifa  zinazohusiana na safari yake (kanuni ya 17- 11,m,n).

Pia anaongeza kuwa abiria ana haki ya kurudishiwa nauli pungufu ya 15% tu ya kiasi alicholipa kama ilivyoainishwa  kwenye  tiketi endapo abiria atavunja  safari ndani ya muda chini ya saa 24  kabla ya muda wa chombo cha usafiri kuanza safari (kanuni ya 24-3).

Wafanyakazi katika  gari la abiria wanakatazwa nini;
Michael anaeleza kuwa kanuni ya 18 ya sheria za SUMATRA [GN] NO.218/2007 inaelezea wafanyakazi katika gari la abiria wakiwa kazini wanakatazwa kutofanya mambo yafuatayo;

Kutumia lugha  chafu  ya  uhasama  kwa abiria, kuwaziba  au kuwazuia  kwa makusudi wahudumiaji wenyewe wa usafiri,
kuendesha  gari zaidi ya vikomo vya spidi kwa kushindania  abiria au kukatisha safari kabla ya  kufika  kituo cha mwisho.

Mfanyakazi au dereva wa gari haruhusiwi  kuendesha  gari  la abiria akiwa amekunywa pombe au kutumia madawa ya kulenya kiasi chochote kile pia haruhusiwi  kuendesha gari la abiria kwa uzembe au namna ya hatari au kinyume na sheria ya usalama  barabarani au sheria nyinginezo.

Aidha haruhusiwi kubughudhi au kusumbua abiria kwa namna yoyote ile hata kama ni mwanafunzi, kuendesha gari la abiria hali dereva anazungumza na simu za kiganjani  na kupakia wanyama hai au vitu vya hatari kwenye gari la abiria.

Aidha Michael anabainisha kuwa mmiliki wa leseni ya gari la abiria au mtumishi wake ambaye atavunja au kushindwa kutekeleza kanuni ndogo  ya [1] atakuwa anatenda kosa  la jinai na  anapaswa, kutiwa  hatiani, kutozwa faini isiyo chini ya laki tano, au kufungwa jela  kwa muda usiyopunguwa mwaka  1  na usiozidi miaka miwili au vitu kwa pamoja.

Gari la abiria likiharibika njiani abiria afanye nini;
Michael anaeleza kuwa Kanuni ya 22 ya sheria za SUMATRA [GH] No. 218/2007 inayohusu kuharibika kwa gari la abiria inasema ikiwa gari la abiria litaharibika au haliko katika  hali ya  kuanza au kuendelea na safari, mmiliki wa leseni ya gari au mfanyakazi wake lazima atafute mbadala wa usafiri ndani ya dakika 10 au arudishe nauli.

Anaongeza kuwa gari likiharibika linatakiwa kuondolewa barabarani na kama gari hilo linatoa huduma ndani ya mji na mji basi litengenezwe ndani ya muda usiozidi masaa.

Ikiwa  baada ya matengenezo ya gari la abiria kwa mujibu wa kanuni ndogo ya 1[b] gari hilo bado  haliko katika hali ya kuanza au kuendelea  na safari, mmiliki wa leseni au mfanyakazi lazima atoe usafiri mbadala.

Haki ya kulipia Mzigo.
Michael anaeleza kuwa kanuni ya 23 ya sheria  za SUMATRA [GN] No. 218/2007 inasema abiria  ana haki kubeba mzigo wenye uzito wa kilo 20 na mtoto mzigo wenye uzito wa kilo 10 bila malipo ila akibeba mzigo zaidi ya ule unaoruhusiwa kubebwa bila malipo mmiliki wa leseni ya gari la abiria ana haki ya kumtoza kwa kilo ya ziada kwa mujibu wa viwango vilivyoruhusiwa.

Haki ya Kufuta oda ya safari na Kurudishiwa Nauli.
Michael anasema Kanuni ya 24 ya sheria  za SUMATRA [GN] No 218/2007 inatoa haki kwa abiria kufuta oda yake ya safari ndani ya masaa 24  au zaidi kabla ya muda wa kuanza safari ya gari la abiria na kurudishiwa nauli yake.

Abiria  ana  haki ya kurudishiwa nauli baada  ya kukatwa asilimia 15  ya nauli hiyo endapo oda ya safari itafutwa ndani ya muda  unaopungua masaa 24 kabla ya muda uliopangwa.

Haki ya Kupewa Tiketi.
Michael anabainisha kuwa Kanuni ya 25 ya sheria  za SUMATRA [GN] No.218/2007 inazungumzia haki ya abiria kupewa tiketi yenye jina lake  pamoja na namba ya kiti chake na haki ya kufahamu muda wa kuwasili kituoni na kuanza safari.

Abiria  pia ana haki ya kufahamu  kituo aendacho, tarehe ya  kutolewa tiketi na tarehe ya safari, kufahamu  namba  ya usajili wa  gari hilo la abiria, kufahamu  nauli ya safari hiyo, kufahamu jina la njia  ihudumiwayo, na kufahamu anuani  na namba ya simu  ya mmiliki wa leseni ya gari hilo.

 ‘Kwa huduma za usafiri ndani ya mji, mmiliki wa gari la abiria atatoa tiketi zilizochapishwa ambazo zinaonesha namba  ya usajili wa gari lenye leseni, njia, nauli iliyoidhinishwa, jina na anuani ya gari au mmiliki wake  na tarehe ya kutolewa’, aliongeza.

Nauli za Watoto na Wanafunzi.
Anafafanua kuwa Kanuni ya 26 ya  sheri za SUMATRA [GN] No.218/2007 inabainisha kuwa kila mtoto na mwanafunzi atakayepanda gari la abiria atakua na haki ya kusafiri kwa kulipa nusu ya nauli  anayotozwa mtu mzima kwa safari hiyo hiyo.

No comments:

Post a Comment