Saturday, December 27, 2014

ASKOFU TAG ATAKA WAKRISTO WAJIEPUSHA NA DHAMBI

 

Katibu wa kanisa la TAG-Kitete Christian Center Mzee Chivinja Mathias akipokea kadi ya Krismas kwa niaba ya waumini wote kutoka kwa Akofu Paul Meivukie wa jimbo la Tabora (wa kwanza kulia akiwa na mkewe) 
Waumini wa kanisa la TAG tawi la Kitete Christian Center (KCC) la mjini Tabora  wakiwa katika ibada ya sikukuu ya Krismas kanisa hapo jana (Picha na Allan Ntana)

Na Allan Ntana, Tabora

WAKRISTO  hapa nchini wamekumbushwa kumtumaini Bwana Yesu katika maisha yao yote kwa kuwa alikuja duniani ili wanadamu wote wakombolewe kutoka katika mateso ya aina mbalimbali sambamba na ondoleo la dhambi.

Kuzaliwa kwaYesu kristo ni mpango kamili wa Mungu kumkomboa mwanadamu kutoka katika taabu, mateso na kuonewa kwa namna yoyote ile na shetani, ndio maana kila amwendeaye na kumwamini maisha yake yanabadilika.

Hayo yamebainishwa jana na Askofu Agustino Dedu alipokuwa akihutubia mamia ya waumini wa kanisa la TAG katika ibada maalumu ya maadhimisho ya sikukuu ya krismasi iliyofanyika jana katika kanisa la Kitete Christian Centre lililopo katika Manispaa ya Tabora.

Alisema wakristu wana kila sababu ya kuadhimisha sikukuu ya krismas kwa kuwa inawakumbusha umuhimu na makusudi ya kuzaliwa kwa mkombozi wetu Yesu Kristu miaka 2000 iliyopita hapa duniani.

Aidha alisema Yesu Kristo alikidhi vigezo vyote vya kuitwa mkombozi wa ulimwengu kwa sababu hata kabla ya kuzaliwa kwake ilishatabiriwa kuwa atazaliwa mtoto wa mwanamume katika mji wa Bethlehemu na jina lake ataitwa Emanuel yaani Mungu pamoja nasi na huyo atakuwa ni mkombozi wa ulimwengu.

Kama hiyo haitoshi hata kutungwa kwa mimba yake kulikuwa kwa miujiza kwani  Mariamu aliyekuwa bikira alipata ujauzito kwa uweza wa Roho Mtakatifu yaani pasipo kulala na mwanamume yeyote na hata alipozaliwa ulimwengu wote ulitaharuki na taarifa zake zilisambaa dunia nzima jambo ambalo si la kawaida mwanadamu wa kawaida anapozaliwa. 

‘Wakristu hatuna budi kumtumaini Yesu kwa kuwa alitolewa kwa ajili yetu ili tuokolewe, tuwe huru na dhambi, tuwe na nguvu za kuendelea kumshinda mwovu shetani, na zaidi ya yote tuishi maisha matakatifu ya kumpendeza’, aliongeza.

 Askofu alifafanua kuwa mtu akiwa ndani yaYesu anakuwa kiumbe kipya kwa kuwa mtizamo wake, tabia zake, fikra na mawazo yake yanabadilika pia, wala hawazi kutenda uharibifu au jambo lolote lililo kinyume na mapenzi ya Mungu.

Naye Askofu wa Kanisa la TAG jimbo la Tabora Paul Meivukie amewataka wakristu wote kuendelea kujishusha zaidi na kujiepusha na mambo yote yaliyochukizo kwa Mungu ili wazidi kumpendeza sambamba na imani zao kukua zaidi.

Akizungumzia sakata la fedha zilizochotwa katika akaunti ya ESCROWAskofu Meivukie alisema kiongozi yeyote anayepewa dhamana ya kuongoza wizara au idara yoyote ya serikali yupo kwa niaba ya wananchi hivyo anapaswa kuwa mwadilifu na kuwa na hofu ya Mungu kwa kutumia madaraka yake vizuri.

No comments:

Post a Comment