Sunday, December 16, 2012

TUMBAKU YAWA KINARA WA KULIINGIZIA TAIFA FEDHA ZA KIGENI

 Na Lucas Raphael,Tabora


Tumbaku.

Serikali imewapongeza wakulima wa tumbaku nchini kutokana na juhudi kubwa wanazozifanya za kuongeza uzalisha zao hilo ambalo limekuwa zao la kwanza kwa kuingiza fedha za kigeni hapa nchini kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Mkuu wa mkoa wa Tabora,Bi Fatma Mwassa, ametoa pongezi hizo kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa tumbaku nchini uliofanyika mjini Tabora na kuhudhuriwa na wawakilishi wa wakulima, bodi ya tumbaku, wanunuzi wa zao hilo na viongozi wa serikali.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa zao la tumbaku limeweza kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 289 kwa kipindi cha mwaka jana, kutoka shilingi bilioni 89 mwaka 2006  na hivyo kuwa zao linalotegemewa zaidi kwa kipato cha fedha za kigeni kupitiia sekta ya kilimo.

Mwassa, aliwataka wakulima wa zao hilo kuongeza juhudi zaidi na kuzalisha kilo milioni 125 kwa msimu ujao kutoka kilo milioni 89 za msimu uliopita, huku akitaka wanunuzi wa zao hilo kuhakikisha wanatoa bei nzuri.

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya tumbaku Tanzania, Wilfred Mushi, amesema kuwa pamoja na uzalishaji huo kuimarika na kuwapa faida kubwa wakulima bado bodi hiyo imeweka mkakati wa miaka mitano utakaosaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la tumbaku kutoka kilo milioni 89 mwaka jana hadi kufikia kilo milioni 840 mwaka 1917.

Mwakilishi wa wakulima wa zao la tumbaku kutoka wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, Said Ntahondi, amelalamikia mwenendo mzima wa masoko ya zao la tumbaku huku akibaini kuwa kuna baadhi ya madaraja yanauzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa gharama za uzalishaji.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment