Wednesday, March 20, 2013

DC NZEGA AWATAKA WALIOVAMIA HIFADHI YA MISITU IPALA KUONDOKA MARA MOJA.

Na Lucas Raphael, Nzega.

Serikali wilayani Nzega katika mkoa wa Tabora imeagiza wananchi wote waliovamia misitu ya hifadhi ya Ipala iliyoko katika kijiji cha Ugembe, kata ya Mwakashanhala wilayani humo kuondoka mara moja kwa hiari yao, vinginevyo wataondolewa kwa nguvu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Nzega, Bi. Zaituni Msangi wiki iliyopita katika doria maalumu ya kutembelea misitu hiyo ambayo iliripotiwa kuvamiwa na wananchi hao na kuendesha shughuli za aina mbalimbali kinyume na taratibu.

DC alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona vitendo vya uvamizi wa maeneo maalumu yaliyohifadhiwa na serikali vikiendelea kuongezeka hapa nchini hali inayochangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa mazingira.

‘Hawa watu hawastahili kuishi katika maeneo haya, uwepo wao ni kinyume na sheria, lakini pia wanaharibu mazingira ya hifadhi hizi za serikali, kwa sababu wanakatakata miti ovyo kwa ajili ya shughuli zao za kilimo, ufugaji na uchomaji mkaa sambamba na uvuvi wa samaki’, alisema DC.

Aidha, DC alibainisha kuwa wananchi waliovamia hifadhi hiyo ya Ipala wamekuwa wakidanganywa na baadhi ya watu wanaojifanya kuwa ni maofisa wa serikali ili watoe hela kwa kisingizio cha kuwamilikisha maeneo hayo bila kutambua kuwa mtu yeyote haruhusiwi kuweka makazi katika maeneo ya misitu ya hifadhi.

‘Tayari tumeweka kikosi kazi cha kufanya doria katika maeneo hayo, na tumeshapewa taarifa za uwepo wa mtu mmoja anayewarubuni wananchi hao kwa kujifanya kuwa yeye ni ofisa wa serikali na ameahidi kuwagawia viwanja katika maeneo hayo ya hifadhi, tumeshaweka mtego wa kumkamata’, aliongeza DC.

DC alibainisha kuwa doria hiyo inayofanywa na watu 18 kutoka vikosi vya FFU, wanyama pori, wataalamu wa maliasili na mgambo, tayari imefanikisha kukamatwa kwa magunia 400 ya mkaa ambao ulikuwa umehifadhiwa katika nyumba zilizoko ndani ya msitu huo wa hifadhi, japo watuhumiwa wote walifanikiwa kukimbia.

Katika msako huo mbali na kukamatwa kwa magunia hayo ya mkaa, kikosi hicho pia kilifanikiwa kukamata gobole 1 na silaha zingine za kijadi zilizokuwa zikitumiwa na wavamizi hao katika msitu huo na bado msako unaendelea, mpaka wahakikishe wavamizi wote wamerudi kwao sambamba na kukomesha usafirishaji wa mkaa.

Aidha, DC aliongeza kuwa katika jitihada za kuhakikisha kuwa uvamizi huo wa hifadhi unadhibitiwa, wameamua kuitisha kikao cha ujirani mwema ili kuweka mikakati ya pamoja na kulifanya zoezi hili kuwa endelevu kwa kuwashirikisha wakuu wa wilaya jirani za Shinyanga, Kishapu na Nzega yenyewe.

No comments:

Post a Comment