Saturday, September 14, 2013

CHF TABORA BADO YAKABILIWA NA CHANGAMOTO KADHAA.


 

MFUKO wa afya ya jamii (CHF),mkoa wa Tabora bado unakabiliwa na
changanoto kadhaa ambazo zimekuwa ni kikwazo cha mfuko huo kupiga
hatua ili uwe na tija kwa wanachama wake.

Meneja wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NIHF), kanda ya Tabora
Emmanuel Adina alisema hayo wakati alipokuwa akifanya mahojiano na
gazeti hili ofisini kwake.

Adina alisema baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji wa
dawa za kutosha na vifaa tiba kwenye zahanati za vituo vya afya.

Aliongeza changamoto nyingine ni pamoja na wananchi bado kutokuwa na
elimu ya kutosha kuhusu tiba kwa njia ya bima ya afya,uhamasishaji
hafifu toka kwa wadau kama watu mashuhuri,viongozi wa dini na
wanasiasa.

Alitaja myingine kuwa ni uchache wa watumishi wa kada ya afya kwenye
vituo vya kutolea huduma na baadhi ya halmashauri kutoanzisha huduma
CHF na TIKA.

Hata hivyo licha ya changamoto hizo bado wameendelea kukabiliana nazo
ikiwemo kuongeza uhamasishaji kila kata,kupunguza uhaba wa dawa katika
vituo ili kuwavutia wananchi kujiandikisha kwa wingi.

Aliongeza kuwa njia nyingine ni kuandikisha wanachama kupitia vyama
vya msingi,kuimarisha usimamizi elekezi katika  vituo vya kutolea
huduma na watumishi kupangwa kwa usawa katika vituo hasa vilivyo
seehemu ngumu kufikika.

Nyingine ni kujaribu kutengeneza mazingira ya mfuko wa CHF kujiunga
iwe lazima kwa wananchi wote wasio kwenye sekta isiyo rasmi na vituo
vipewe mgao wa dawa kwa wakati na kadri ya maombi yao ya kila robo ya
mwaka.

Adina alizungumzia wanchama kila wilaya na kudai hadi kufikia mwezi
juni 2013 wilaya ya Nzega ilikuwa ikiongoza kwa kuwa na wanachama wa
CHF kaya 9,308,Igunga 6,471,Uyui 4,078, Sikonge 2,146 na Urambo ya
mwisho ilikuwa na wanachama kaya 1,031.

Alisema hadi mwezi disemba 2013 wanatarajia ongezeko la wanachama wa
CHF kwa kila wilaya kufikia Uyui kaya 20,000, Urambo 14,000, Igunga
10,000, Nzega 2,000,Manispaa 2,000 na Uyui kaya 1,000.

No comments:

Post a Comment