Monday, September 16, 2013

VIONGOZI HAWAPIGI KELELE WAKULIMA KUIBIWA!!!-SAID NKUMBA



 

Na Hastin Liumba,Sikonge.

MBUNGE wa jimbo la Sikonge mkoani Tabora,Said Nkumba anasikitishwa na kusononeka kutokana na baadhi ya viongozi wenzake kukaa kimya na kushindwa kupiga kelele wakulima wa nchi hii wanavyoibiwa.

Nkumba alisema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya kupokewa kwa maandamano na wananchi wa jimbo lake siku chache zilizopita,maandamano yaliyoanzia kata ya Pangale hadi Sikonge mjini hadi nyumbani kwake.

Alisema kutokana na kauli yake bungeni ya kutaka mswada wa sheria za ushirika usainiwe na rais  Dkt Jakaya Kikwete,na kutaka Apex ifutwe kutokana na kukosa msaada, uzalendo wa kweli kwa wakulima nchini hususani wa zao la tumbaku ndicho kiini cha wananchi wa jimbo lake kumlaki kwa maandamano.

Alisema umefika wakati sasa kwa viongozi wenye dhamana kujipanga upya ili kuweza kusaidia wakulima wa nchi hii ili wasibaki kama yatima kwenye haki zao za msingi kwani taarifa za sasa zinaonyesha wakulima wengi hawajitambui katika uwezo wao wa kuendesha ushirika.

“Wanaushirika wote ndiyo wenye nguzo za kuendesha ushirika na ifikie mahali viongozi wote wasio waaminifu na wezi kuondolewa mara moja na hii ni njia mbadala ya kumkomboa mkulima kwani kupewa madaraka isiwe sehemu ya kujitajirisha.”alisema Nkumba.

Alisema mkulima angefikia mahali pazuri endapo kungekuwa na maamuzi ya kuwajibishana na itakuwa haina maana kuwa na vyombo vya ushirika vinavyoendelea kukaa kimya wakati wizi,dhuluma dhidi ya wakulima inaendelea.

Nkumba alisema ana imani kubwa kwa rais Dkt Jakaya Kikwete atausaini mswada ule…..na hiyo itakuwa ni ishara tosha sasa mkulima wa nchi hii anakombolewa cha msingi tu kuwepo na utekelezaji wa maamuzi waliyopewa baadhi ya viongozi.

Hata hivyo siku chache baada ya mswada huo kupitishwa na kutaka kufutwa kwa Apex wameibuka baadhi ya viongozi wanaolalamika na kuitisha vyombo vya habari kutaka rais Dkt Jakaya Kikwete kutosaini mswada huo.

“Haya yanayolalamikiwa na wale wanaotaka rais asisaini ule mswada inaonyesha kuna maslahi yao hapa kwa hawa wanaojiita wanaushirika……napata mashaka sana na hawa watu na hapa jamii inawaona hawajui mbona hawalalamiki mkulima kubeba mzigo mzito kwa muda mrefu lakini hawakuitisha vyombo vya habari kulalama.”alisema.

Alisema kamwe hataacha kupiga kelele kumsaidia mkulima hasa wa zao la tumbaku na sasa moto kauwasha hatauzima na hakuna atayemziba mdomo.

Mbunge huyo anasema anawashukuru wakulima na wananchi kwa ujumla kwani toka ametoka bungeni amekuwa akipokea simu nyingi za pongezi toka wananchi wa baadhi ya mikoa na kumtaka aendelee na mapambano katika kumkomboa mkulima wa nchi hii.

Alisema wao kama wabunge hawana mipaka ya kutetea wananchi zaidi ni kutetea makundi yote ya jamii hivyo mtu mwenye kuona kuna mipaka basi huyo ni sehemu ya wale wanaotaka mkulima aendelee kubeba mzigo mzito hasa wa madeni makubwa na wizi.



No comments:

Post a Comment