Monday, September 23, 2013

TAMKO KWA UMMA JUU YA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAANDISHI WA VYOMBO VYA HABARI VYA UMMA NCHINI TANZANIA


 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu hivi karibuni ulikamilisaha ziara ya kuangalia na kutathmini mahitaji ya watetezi wa haki za binadamu yaani mashirika yanayotetea haki za binadamu wakiwamo waandishi wa habari. 

Kwa mujibu wa mazungumzo na maelezo tuliyoyapata katika dodoso zilizojazwa na waandishi wa habari wa vyombo vya umma inaonekana kuna uhasama mkubwa unaojengeka baina ya waandishi wa vyombo vya umma na wananchi ama na vyama vyao vya siasa. 

Mgogoro huu wa kiusalama baina ya wananchi na vyama vyao dhidi ya waandishi wa habari wa vyombo vya umma umejitokeza mara nyingi kwenye mikutano ya kisiasa na kwenye mivutano ya raia kwa upande mmoja na serikali na wawekezaji kwa upande mwingine. 

Mtandao umebaini kuwa hali hii tete ya kiusalama kwa waandishi wanaoripoti katika vyombo vya umma unazidi kukua na huenda ukawa na madhara makubwa kwa wanahabari hawa hadi kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. 

Matukio ya kufukuzwa, kupigwa mawe na kudhalilishwa kwa waandishi hawa yamekuwa ni mengi kwa mujibu wa viongozi wa Vilabu 16 vya waandishi wa habari ambavyo Mtandao ulivitembelea kujua hali ya usalama kwa waandishi.

Mifano halisi ni kama ifuatavyo; takriban katika mikoa yenye rasilimali au upinzani mkubwa wa kisiasa kama Mbeya, Iringa, Arusha, Kigoma , Dar es Salama kumekuwepo na matukio ya kuwadhalilisha waandishi wanaoripoti katika vyombo vya umma.

Matukio haya ni kama yale yaliyomkuta mtangazaji wa Shirika la Utangazi la Taifa (TBC), Bw. Marin Hassani Marini pale alipozongwa na wananchi siku ya uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa mwaka 2010 eneo la Jangwani Dar es Salaam, baada ya matangazo ya shirika hilo kukatika ghafla.

Matukio kama hayo yanaonekana kuzidi na hadi kufikia chaguzi zijazo huenda waandishi hawa wakashindwa kufanya kazi katika vyombo hivi vya umma vinavyotumia kodi ya Watanzania.
 

Kukatika ama kukatishwa kwa matangazo kumekuwa mwiba kwa waandishi wa habari kwa kuwa watazamaji na wananchi wanahisi kuwa waandishi ndio wahusika wa matukio haya bila kufahamu kwamba wao hupokea maelekezo kutoka kwa viongozi wao na wahariri. 

Tukio kama hili lilimkumba mwandishi mwingine wa TBC mwezi mei 2013 katika mvutano wa serikali na wananchi wa Mtwara. Baada ya mitambo ya TBC kukatika wakati wananchi hao wakiwa katika maandamano, moja kwa moja wananchi waliamua kumuadhibu mwandishi Kassimu Mikongolo kwa kumchomea nyumba yake na gari kwa kuamini amehusika na kukatika kwa matangazo ya TBC mkoani humo. 

Matukio mengine yamekuwa yakijitokeza Mkoani Arusha. Mfano waandishi wa TBC toka chaguzi ndogo zilizofanyika Mkoani humo wamekuwa wakifukuzwa na kukatazwa kuhudhuria mikutano ya siasa hasa mikutano ya CHADEMA. 

Hali imewafanya waandhishi wa vyombo vya umma kuwatumia waandishi wa vyombo vingine kuwachukilia taarifa katika mikutano ya kisiasa. Waandishi waliojikuta katika wakati Mgumu kufanya kazi zao ni pamoja na Leornard Manga, Sechela Kongola na Khalifan Mshana na Ben Mwaipaja. Kwa upande wa Kigoma, waandishi wa vyombo vya umma wanadai kuwa wanafanya kazi vizuri na viongozi wa vyama vyote vya upinzani, isipokuwa wananchi ndiwo bado hawana imani na utoaji wa taarifa katika vyombo vya umma. 

Dotto Elias TBC Kigoma aliwahi kujikuta katika wakati mgumu katika mkutano wa CHADEMA kutokana na wananchi kutaka kumdhuru, kilichomsadia ni viongozi wa CHADEMA kuongea na wanachama wao wasifanye lolote na wamruhusu aendelee na mikutano. 


Katika Mkoa wa Ruvuma, Mwandishi Gervas Msigwa wa TBC mara nyingi amejikuta akipata wakati mgumu kuhudhuria mikutano ya siasa hasa ya CHADEMA, mfano uchaguzi mdogo kata Lisabon Songea Mjini 2011 Msigwa alipigwa na kukimbia. 


Mkoani Iringa mwandishi wa magazeti ya umma Habari Leo na Daily News Frank Leonard , alipigwa na walinzi wa CCM (Green Guard) kutokana na misimamo yake ya kuandika ukweli katika chaguzi za ndani za CCM mwaka 2010. 


Tukio hili linadhirisha kuwa viongozi wa chama tawala wakati mwingine hulazimisha waandishi wa vyombo vya umma kuandika kile wanachokitaka na wasipofanya hivyo hujikuta katika hali utata kiusalama. Matukio haya kwa waandishi wa umma ni mengi wengine walishashushwa kwenye ndege kwa kuhisiwa kuwa wanaandaa taarifa zisizotakiwa na chama fulani. 


Waandishi wa habari wa TBC, wakati mwingine wamelazimika kutoa nembo za TBC kwenye magari yao au kamera zao ili kunusuru maisha yao. Mfano katika hatua ya kufuatilia kesi zinawahusu Shekh Issa Ponda na Alfred Rwakatare wa CHADEMA waandishi George Kasembe na Nora Uledi walijikuta wakitaka kunyang’wa kamera zao na kuzomewa na wafuasi wa watuhumiwa hawa. Chanzo cha Mitafaruku Hii

 
• Katika uchunguzi wetu tumebaini kwamba tatizo inawezekana lisiwe katika ngazi ya chini yaani wanahabari ambao wameaajiriwa katika vyombo vya umma kwa sababu wao wanalazimika kufuata sera za vyombo vyao au maelekezo wanayopewa na viongozi wao kazini. Historia inaonyesha kwamba wanahabari wakati mwingine wanajikuta wakiwa njia panda na kushindwa kufahamu wasimamie wapi mara wanaposhitukizwa katika mivutano kati ya serikali kwa upande mmoja na wanajamii yaani wananchi kwa ujumla kwa upande mwingine.

• Changamoto nyingine ni pale baadhi ya watendaji serikalini kama vile wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi wa maendeleo katika ngazi hizo za wilaya na mikoa wanapoamua kuwatumia waandishi wa vyombo vya umma na hata magazeti yanayomilikiwa na umma kwa manufaa yao binafsi au ya kiserikali/chama tawala. Watendaji hao huona kwamba wanahabari wa TBC na vyombo vingine vya umma ni maafisa habari wao. Jambo hilo hufanyika kwa njia ya ushawishi wa aina mbali mbali ikiwamo malipo ya ziada, kupewa ofisi ndani ya ofisi za wakuu wa mikoa au wilaya, lakini wakati mwingine hata kwa kuwalazimisha kuripoti kile ambacho watendaji hao wanakitaka.
 

• Kwa upande mwingine ipo changamoto, kwani baadhi ya taasisi wakati mwingine hazitaki kuwashirikisha wanahabari kutoka katika vyombo vya umma kwa madai kwamba hawatarajii vyombo hivyo vitaripoti taarifa yoyote ile inayokosoa serikali na yenye maslahi kwa umma. Hii inamaanisha kwamba, baadhi ya wananchi, vyama vya siasa na taasisi binafsi au hata za umma zimekosa imani na vyombo vya habari vya umma.
 

Kutokana na mazingira haya waandishi wa vyombo vya umma hufanya kazi kwa mashaka mashaka kwa kutofahamu hatma yao iwapo wataripoti kinyume na matarajio ya mashabiki wa kisiasa katika maeneo hayo au kinyume cha matarajio ya wananchi. 
 
Hivi karibuni Mtandao huu ulifanya mazungumzo na TBC ambapo ilikiri kuhusu taarifa za baadhi ya vitisho kwa waandishi wao, na mfano halisi ukawa ni suala la Kassimu Mikongolo. Viongozi wa TBC walisema wanaongoza chombo kutokana na sera na kanuni zao za kazi, hivyo walikanusha uvumi kwamba TBC ni chombo chenye kuelemea upande mmoja kwa maana ya kwamba kimelalia upande wa serikal na chama tawala, walilisitiza kwamba hicho ni chombo cha umma na kina ripoti kwa usawa na pia kutii mamlaka iliyopo. Nini Kifanyike
 

• Kuhusu suala la usalama wa waandishi, TBC huwa wanatoa mafunzo mara chache hasa mara Uchaguzi Mkuu unapokaribia, lakini imeonekana kuna umuhimu wa Mtandao kuanzisha ubia na TBC na kuwatembelea wanahabari wake kwa ajili ya mafunzo ya usalama hasa katika mikutano ya kisiasa na maeneo yenye mivutano kati ya serikali na raia.

• Ipo haja ya kuboresha miongozo ya vyombo vya umma ili kuendana na nyakati hizi za vyama vingi na kupunguza maamuzi binafsi ya baadhi ya watendaji.

• Kuna haja pia ya kuwa na mkutano wa pamoja kati ya vyombo vya umma, vyama vya siasa na Mtandao ili kujadili usalama wa waandishi hawa katika chaguzi zijazo.

• Mtandao unawasihi watanzania wote na vyama vya siasa kuacha kuwadhalilisha waandishi hawa wa vyombo vya umma wanapokuwa katika maeneo au mikutano yao na kuchukua hatua dhidi ya menejimenti pale wanapohisi kwamba wamekosewa.

• Tunawashauri waandishi wote wa vyombo vya umma na menejiment zao kuwa vyombo vya umma ni mali ya umma hivyo wanapaswa wakati wote kuwatumikia watanzania na si serikali wala chama chochote.

• Tunashauri pia vyombo vya umma vipewe rasilimali ya kujenga ofisi zao nje ya majengo ya viongozi wa kiserikali. Kufanya hivyo kutarudisha imani kwa wananchi na kuondoa dhana iliyojengeka kuwa wao wamekuwa ni maafisa habari wa viongozi wa serikali.

• Tunawashukuru TBC kwa kumsaidia Kassim Mikongolo kutoka katika eneo ambalo lilikuwa hatari kwake kimaisha na Mtandao unaunga mkono hatua hiyo kwa kumsaidia Mikongolo kurudisha baadhi ya gharama wakati akiendelea kusaidiwa na TBC ili kupata fidia ya nyumba yake.

• Tunawasihi viongozi wa siasa kutoa elimu ya haki za mwandishi kwa wanachama wao na kuimarisha ulinzi na usalama wa waandishi wanapokuwa katika mikutano yao.

• Tunawasihi sana viongozi wa serikali na wanasiasa wote hasa wa chama tawala, waache tabia ya kuwagawa waandishi wa habari kwa matabaka kwa malengo ya kutaka kuwapata waandishi wa habari amabao wataandika kile wanachokitaka kiandikwe na sio kuandika ukweli na hali halisi. Tabia hii imewafanya waandishi wawe njia panda na kujikuta wakiwatumikia viongozi na wanasiasa kama maafisa habari wao na kujiweka katika mazingira magumu ya kiusalama.
 
Imeletwa kwenu kwa niaba ya Mtandao na: Onesmo Olengurumwa Mratibu Taifa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD-Coalition).  Onesmo Olengurumwa  MRATIBU MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU

No comments:

Post a Comment