Saturday, December 1, 2012

BWAWA LA MRADI WA UMWAGILIAJI LA ULYANYAMA ‘SIKONGE’ LAKAUKA

Na Allan Ntana, SIKONGE
 
Kukosekana kwa mvua za kutosha mwaka huu kwa baadhi ya maeneo mkoani Tabora,
kumeanza kuonyesha dalili mbaya hasa katika wilaya ya Sikonge, hali inayoashiria kuwepo kwa upungufu wa chakula katika maeneo hayo, kwa  kuwa shughuli nyingi za kilimo hasa kilimo cha umwagiliaji, zimekwama kutokana na kukauka kwa bwawa lililokuwa likitegemewa sana na wananchi katika eneo hilo.

Hayo yalibainishwa katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Sikonge kilichofanyika juzi wilayani hapa katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi Sikonge FDC, ambapo madiwani walitaarifiwa juu ya kukauka kwa bwawa hilo la mradi wa umwagiliaji na hivyo kufanya shughuli zote za kilimo kusimama.

Akitoa taarifa mbele ya baraza juu ya hali halisi ya bwawa hilo la mradi wa umwagiliaji, unaotegemewa sana na wakazi wengi wa vijiji vya Kisanga, Ulyanyama, Ufisi na vijiji jirani katika kilimo cha mpunga, Kaimu mhandisi wa idara ya maji wilayani hapo Bw. Wibonela Jafari, alisema kuwa bwawa hilo limekauka kabisa na yamebakia matope sehemu zilizo nyingi.

Aidha Bw. Jafari alisema kuwa kukosekana kwa mvua za kutosha mwaka huu kumeathiri sana shughuli za kilimo katika maeneo mengi na hasa kwa wakazi walio katika ukanda wa bonde hili la Ulyanyama, na kuongeza kuwa kwa sasa hivi hakuna maji kabisa, hivyo hakuna kilimo kinachoendelea.

Bw. Jafari alitaja athari mbalimbali zinazotokana na hali hiyo kuwa ni kukwama kwa shughuli zote za kilimo cha umwagiliaji, kukwama kwa mipango ya halmashauri ya kutumia bwawa hilo kusambaza maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani katika vijiji vya Tutuo, Mlogolo, Mkolye, Tumbili na Sikonge mjini na mifugo kukosa maji,  hali ambayo itafanya mifugo mingi kufa.

Kutokana na hali ilivyo Bw. Jafari aliwasihi wananchi kujiepusha na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo  ili kulinda vyanzo vya maji katika maeneo yaliyo mengi na akawashauri wananchi hao wageukie kilimo cha mazao ya msimu kama vile mhogo, viazi vitamu, alizeti na wale walioacha kulima tumbaku waanze sasa kulima pindi mvua zitakapoanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. Paul Nkulila, akizungumzia hali hiyo, alikiri  kuwa hali si shwari katika maeneo mengi kwani mvua imekuwa kidogo sana, na kubainisha kuwa  katika bwawa la Ulyanyama maji yamekaribia kukauka kabisa na yaliyobaki ni machafu sana hayafai kwa shughuli yoyote ya kilimo.

 Bw. Nkulila aliongeza kuwa baada ya kuona hali ya mvua siyo nzuri, na kugundua upungufu uliopo wa tani 2700 za chakula,  waliwatahadharisha wananchi kutouza chakula chote,  sambamba na kuwashuri kuchukua hatua hasa kwa kugeukia kilimo cha mazao mbadala yanayostahimili ukame, na akabainisha kuwa jitihada zinaendelea za kuwatafutia mbegu za mazao kama vile mtama na mhogo.

…. ‘‘Tunataka kuchukua mbegu za mhogo toka kituo cha utafiti cha Malugu kilichoko mkoani Kagera kwani hili ni zao mbadala linaloweza kustahimili ukame na kuwa  msaada mkubwa katika wilaya yetu’’, alibainisha Bw. Nkulila 

Bw. Nkulila aliongeza kuwa tayari halmashauri imeshaomba chakula cha msaada toka serikalini, na akabainisha kuwa mda si mrefu watapata tani 113 za mahindi ya ruzuku na tani 13.5 za mahindi ya bure, na yote yatatolewa kwa familia zilizothibitishwa kuwa na upungufu katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment