Thursday, January 16, 2014

POLISI WAUA RAIA ULYANKULU TABORA KWA RISASI,WAJERUHI MMOJA



Askari  Polisi wa kituo kidogo cha Tarafa ya Ulyankulu wilayani Kaliua mkoani Tabora wamemuua kwa kumpiga risasi  begani  kijana mmoja aliyefahamika  kwa jina la John Joseph(28)  kwa tuhuma  za kuleta vurugu na kutaka kuchoma  moto  Kituo hicho cha Polisi,wakiwashurutisha  askari  hao kumwachia  mtuhumiwa  mmoja  wa wizi  wa ng’ombe ili waweze  kumwadhibu  wenyewe.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Peter Ouma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amelieza mtanzania kuwa marehemu John Joseph juzi majira ya saa tano asubuhi akiwa na wananchi wengine walimkamata kijana mmoja  Shija Matenga(23)kwa tuhuma za kuiba ng’ombe watano huko wilayani Kasulu mkoani Kigoma ambaye aliwaswaga hadi eneo la Ulyankulu wilayani Kaliuawa ambako alikamatwa na kuanza kupigwa.

Ouma alifafanua kuwa  wakati kundi la wananchi hao ambao  miongoni mwao akiwemo  marehemu  Joseph  wakiendelea kumshambulia  mtuhumiwa huyo wa wizi wa mifugo  Shija  Matenga,askari  Polisi wa kituo  hicho  cha  King’wangoko  kilichopo tarafa ya Ulyankulu chini ya uongozi  wa mkuu wa Kituo  hicho namba  E.1295 D/SGT  KIMOLA  walipata taarifa hiyo na hivyo askari wawili waliagizwa  kufika eneo la tukio kujaribu kuwazuia  wananchi hao ambao tayari walikwisha mfunga kamba mtuhumiwa huku wakikusanya majani kwa lengo la kutaka kumchoma moto.

Kwa mujibu wa Kamanda Ouma baada ya askari  hao  kufanikiwa kumuokoa mtuhumiwa  walimfikisha kituoni  wakati  kundi  la  wananchi  hao  likiwafuatilia kwa nyuma wakiwa wanawarushia mawe,chupa na fimbo  askari  Polisi hao ambao  nao  wakalazimika  kujikinga kwa kufyatua risasi iliyompata John Joseph  begani  na hatimaye kufariki dunia hatua chache kutoka Kituoni hapo.

Katika sakata hilo lililodumu kwa muda mfupi  Malembeka Matemele(22)ambaye ni mkazi wa Ulyankulu alipigwa risasi paja la mguu wa kulia huku kamanda Ouma akimtaja kuwa ni mmoja kati ya vinara wa vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya mtu mmoja.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa tarafa ya Ulyankulu ambao hawakutaka majina yao yatajwe hadharani wamelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kufanya mauaji hayo ya raia asiyekuwa na hatia.
Wamesema wakati wa purukushani hizo  zikiendelea  marehemu John alipigwa risasi akiwa anatokea nyumbani kwake hatua ambayo wamelitafsiri tukio hilo kuwa ni la kinyama na huku wakiziomba taasisi zinazotetea haki za binadamu kufuatilia na kuchunguza ukweli wa tukio hilo la maonezi.

No comments:

Post a Comment