Monday, July 22, 2013

MWAKASAKA,WAZAMBI WATEULIWA KUWA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA WILAYA CCM TABORA MJINI


Mlezi wa Chipukizi mkoa wa Tabora Bw.Emmanuel Mwakasaka

NA LUCAS RAPHAEL,TABORA

Chama  cha mapinduzi  wilaya ya  Tabora  mjini  kimeamua kukata mzizi wa fitna baada  ya  kuwateua  wanachama  wawili  Emmanuel  Mwakasaka  na Nassor Wazambi kuwa  wajumbe wa halmashauri kuu  ya  wilaya  hatua  ambayo  imezua  gumzo  na  kupengezwa  na  wanachama waliowengi kwa uamuzi huo wa busara.

Hatua hiyo  imekuja siku chache baada ya Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Bw.Ismail Rage kusikika amemshitaki makao makuu ya CCM Taifa mjumbe wa kamati ya fedha na kamanda wa vijana Chipukizi Tabora Bw.Emmanuel Mwakasaka kuwa amekuwa akijipitisha kwa wananchi jimboni humo kwa lengo la kutaka kugombea Ubunge  ifikapo mwaka 2015 jambo ambalo limebainika kuwa ni majungu wanayotengenezewa watu wenye nia ya kukisaidia Chama hicho.

Habari alizozinasa mdodosaji wetu kutoka ndani ya Chama hicho,zinasema kuwa katika kikao cha halmashauri kuu ya wilaya ya CCM Tabora mjini kilichoketi  leo  tarehe  20 Julai 2013 kujadili masuala mbalimbali ya Chama hicho katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi,Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora mjini  Bw. Moshi Nkokota kabla ya kukifunga kikao hicho alitangaza rasmi kuwateua wajumbe wawili ambao wataziba nafasi ngazi ya halmashauri kuu ya wilaya hiyo ambapo alimtaja Nassor Wazambi na Emmanuel Mwakasaka kuwa ni wajumbe halali kufuatia katiba ya Chama hicho inayompatia fursa Mwenyekiti ya kuwateua.

Bw.Nkonkota alianza kwa kusema amekuwa anashangazwa na tabia ya baadhi ya watu wanaokuwa wanazorotesha juhudi za wengine wenye nia ya kukisaidia chama hicho ambacho kwa sasa kimeingia kwenye wimbi la kukabiliana na vyama vya upinzani na hivyo kutoa onyo kali  kwa yeyote mwenye tabia ya kuanzisha majungu ya kuvunja nguvu za wengine eti kwa kigezo cha kuwatishia kuwashitaki makao makuu ya CCM ngazi ya Taifa. 

Alisema milango ipo wazi kwa kada yeyote wa CCM kuonesha uwezo wake katika kukisaidia Chama na kwamba hatachukuliwa kama mtu aliyeanza kampeni mapema huku akiweka wazi kuwa CCM itaendelea kuthamini michango ya mwanachama yeyote mwenye nia nzuri kwa Chama hicho.

Akizungumzia juhudi anazozionesha Bw.Mwakasaka ambaye ni kada wa CCM anayeaminika kwa wanachama wa kawaida na viongozi kwa ujumla,Nkonkota alisema Kada huyo amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia mambo mbalimbali na kwamba anashiriki mikutano mingi ya hadhara na kuwa na uwezo mzuri wa kujibu hoja za wananchi katika kuitetea serikali iliyoko madarakani kwa kueleza utekelezaji wa ilani ya CCM bila kutafuna maneno.

Alisema  Mwakasaka kwa ushahidi wa waziwazi ameweza kuwarejesha wanachama wa CCM waliokimbilia vyama vya upinzani kama Chadema na Cuf kupitia mikutano ya hadhara  na hivyo kuendelea kukipa nguvu CCM ambayo ilianza kusemwa vibaya  na  wananchi kupitia mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Bw.Aden Rage kwa kile kinachodaiwa kuwa kutokuwa karibu na wananchi kwa kutofanya mikutano ya mara kwa mara kama wafanyavyo wabunge kwenye majimbo mengine.  

Kuhusu Nassor Wazambi ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Tabora  naye anatambulika kwa mchango wake katika kuwaunganisha vijana hatua  ambayo imekuwa endelevu na kuenziwa na Mwenyekiti wa UVCCM wa sasa ambaye ni Bw.Lucas Masanja.

Mara baada ya Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Tabora  Bw.Nkonkota  kuwatangaza wajumbe hao wawili Mwakasaka na Wazambi,baadhi wa wajumbe waliohudhuria katika mkutano huo waliibuka  na kelele za shangwe huku wakiinua viti juu juu wakiashiria kupongeza uamuzi wa busara wa mwenyekiti huyo.

Aidha kwa upande mwingine hata kabla ya uteuzi huo wa wajumbe hao wa halmashauri kuu ya wilaya ya Tabora  Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Bw.Aden Rage amekuwa katika wakati mgumu ndani na nje ya CCM wilaya ya Tabora mjini kwa kile kinachodaiwa kuwa kutokuwa karibu na baadhi ya viongozi na wanachama tangu kuchaguliwa kwake kushika wadhifa huo katika uchaguzi wa mwaka 2010,jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa hata na baadhi ya wananchi wa kawaida  ambao kimsingi ndio wapigakura waliomuweka madarakani kupitia Chama hicho.

Hata hivyo  mtihani mkubwa umebaki kwa Rage ambao macho ya wengi yanaangazia kuona kama ataweza kuonesha ushirikiano kwa wajumbe hao wawili wa halmashauri kuu ya wilaya  na hasa kwa mjumbe mmoja ambaye tayari amekwisha fikisha malalamiko dhidi yake CCM ngazi ya Taifa kwamba ameanza kampeni mapema hatua ambayo imejionesha kuwa Rage anahofia nafasi yake ya Ubunge katika uchaguzi ujao bila kujali nafasi hiyo ya Ubunge mara nyingi kwa jimbo la Tabora mjini hutumikiwa kwa awamu moja tu.


No comments:

Post a Comment