Tuesday, July 16, 2013

UZALISHAJI MDOGO WA MAZAO YA CHAKULA NI CHANZO CHA UMASKINI






 Na Lucas Raphael,Tabora



Tatizo la kuongezeka kwa umaskini kwa wananchi wa wilaya ya URAMBO mkoani TABORA linatokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula  na ulipaji wa madeni ya mikopo ya pembejeo kwa ajili ya kilimo cha zao la tumbaku.

Wakizungumza katika mkutano wa juu ya uelewa wa Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini (MKUKUTA), wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani URAMBO wamesema mikopo ya pembejeo na kutowajibika ipasavyo kwa wananchi katika kilimo cha mazao ya chakula ni chanzo kikubwa cha kuendelea kuwepo kwa umaskini wilayani humo.

Wamesema licha ya wilaya ya URAMBO kuongoza nchini kwa kilimo cha tumbaku, lakini wananchi wake wanaendelea kuwa maskini kwa sababu fedha wanazopata zinalipa madeni ya pembejeo na fedha zinazobaki kununulia chakula.

Wameshauri kwamba ili kuondoa umaskini, wananchi wanapaswa kuwajibika katika kulima mazao ya chakula kukidhi mahitaji ya kaya zao na pia kutumia mapato ya tumbaku kwa mahitaji mengine muhimu ya kijamii kwa vile afya, elimu kwa watotona ujenzi wa nyumba bora  badala ya  kununulia chakula.

Katika mkutano huo wa siku  mbili ulioandaliwa na Shirika la JIDA la mjini TABORA kwa ufadhili ya Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) la jijini  Dar es salaam , washiriki pia walielimishwa juu ya umuhimu wa  matumizi ya mfumo wa kuhifadhi takwimu katika kupambana na umaskini.

JIDA ni shirika lisilo la kiserikali mkoani TABORA linalohamasisha maendeleo ya watu kwa kupambana na vikwazo vya maendeleo na kutoka huduma endelevu za jamii kwa makundi yaliyo katika hatari ya kupata madhara zaidi.



No comments:

Post a Comment