Monday, November 26, 2012

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAA BALOZI SEIF IDD AWALIA NJUGA MASUALA YA UMILIKI WA ARDHI ,SERIKALI YAFUTA HATI YA UMILIKI


Mmoja wa Wana kijiji wa Selemu wakitoa duku duku lao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi dhidi ya Vitendo wanavyofanyiwa na baadhi ya wamiliki wa mashamba yaliyomo katika maeneo yao.
  Bwana Abeis Said Shankar anayemiliki shamba katika eneo la Selemu akijitetea mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baada ya kulalamikiwa ukorofi anaowafanyia wana kijiji wa hapo katika shughuli za Kilimo na Ufugaji
  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Ndugu Juma Ali Juma na Ofisa wake wa Kilimo wakimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif eneo la Ramani ya Shamba la Wizara hiyo la ekari 6 linaloleta mzozo wa umiliki.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuonyesha Mkurugenzi wa Kituo cha Kujiendeleza Kielimu Kilichopo Selemu Ndugu Kassim Hassan Nyaraka zake alizozigushi za umiliki wa eneo la shamba la Kilimo katika Kijiji hicho.
--
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kumfutia mara moja hati ya umiliki wa Eneo la Shamba la Serikali Bwana Abeid Said Shankar alilopewa katika Kijiji cha Sehemu kufuatia mgongano unaoendelea kujitokeza kati yake na Wana kijiji wa eneo hilo ambao unaashiria hatma mbaya ya kuvunjika kwa amani baina ya pande hizo mbili.
Serikali pia imeuzuia Uongozi wa Kituo cha Kujiendeleza Kielimu cha Eneo hilo kufanya shuguli yoyote ya ujenzi kwa vile umiliki wake hauko kihalali katika vyombo vinavyosimamia masuala ya Ardhi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi katika eneo hilo ambapo alishuhudia mgongano na malalamiko ya Wananchi hao dhidi ya wawaoendesha na Kumiliki Mashamba na Maeneo hayo.

Mama Mmoja alietaka kujenga nyumba katika eneo la Kituo hicho cha Kujiendeleza Kielimu baada ya kuombewa ruhusa na Uongozi wa Shehia hiyo alijikuta akizuiwa kujenga na Mkurugenzi wa Kituo hicho Bwana Kassim Hassan Juma ambaye alikuwa na nyaraka sizizo halali zinazokisiwa kuwa ni za kughushi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo na Mali asili Ndugu Juma Ali Juma ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Bwana Kassim Hassan hakuwa na Nyaraka halali za eneo hilo ambalo ni milki ya Wizara ya Kilimo.
Ndugu Juma alisema kutokana na maombi na umuhimu wa Ardhi kwa mahitaji ya Jamii Serikali imeshaiagiza Wizara hiyo kulipima eneo hilo ili baadae ligaiwe kwa Wananchi kwa kuendeleza mahitaji yao Kilimo na Ujenzi ambapo alieleza kuwa kazi hiyo imeshakamika.
Malalamiko hayo yamekwenda sambamba na ule mzozo unaovukuta wa Wakulima waliokuwa wakiendeleza shughuli za Kilimo katika shamba la Bwana Abeid Said wakidai kwamba mmiliki huyo alikuwa akionyesha dalili mbali mbali za kuhatarisha maisha ya Mifugo pamoja na Vipando vyao.
Akitoa ufafanuzi wa kadhia hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiagiza Wizara ya Kilimo kumtafutia Shamba Jengine Bwana Abei Said Shankar ili kuwepuka shari ambayo imeshaanza kuchomoza.
“ Nakuagizezi Wizara ya Kilimo mhakikishe kwa Hatua ya mwanzo mnampatia Eneo la Kujenga Nyumba Mwananchi huyu Masikini wa Mungu, mnampimia eneo la ujenzi Bwana Kassim kwa ajili ya Kituo chao waweze kumiliki Kihalali pamoja na Kumpatia shamba jengine Bwana Abeid. Hatua hii nahakika itaondoa kabisa mvutano huu unaoweza kutafutiwa njia bila ya migongano”. Alifafanua Balozi Seif.
“ Kama Mtu anashindwa kuishi na Jamii inayomzunguuka katika maeneo ya umiliki wa Serikali mtu huyo inafaa aondoshwe na mamlaka zinazosimamia umiliki huo wa Serikal,I ili kuwepuka shari”.Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Aidha Balozi Seif aliendelea kuiasa Jamii kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali ili kuwepuka mizozo isiyokuwa na lazima na kutahadharisha kwamba ardhi itaendelea kuwa mali ya Serikali na itakapoamua kuitumia ardhi hiyo kwa maslahi ya umma haitasita kufanya hivyo mara moja.
Eneo hilo la Ekari sita liliopo katika Kijiji cha Selemu kilichojaaliwa utajiri wa ardhi ya Rutba liko chini ya Umiliki wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar tokea mwaka 1964.


Na 
Othman Khamis Ame, 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment