Shirika
lisilo la kiserikali la mpango endelevu wa uboreshaji wa mazingira
(SEMA), limetumia zaidi ya shilingi milioni 20 kugharamia ujenzi wa
kituo cha ushauri na ujenzi wa vyoo bora (Sanitation Centre) kilichopo
kata ya Mwakashanhala wilayani Nzega mkoa wa Tabora.
Akizungumza
kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo hicho Mkuu wa wilaya ya Nzega Bituni
Msangi amesema ni ukweli ulio wazi kwamba maisha ya mwanadamu na
maendeleo yake, yanajengwa kwa kuboresha usafi wa mazingira.
Akifafanua
zaidi, Msangi amesema usafi wa mazingira ni muhimu kwa usalama wa
mwananchi yeyote.
Amesema
mazingira machafu, yanapelekea maambukizi ya magonjwa ya matumbo,
kipindupindu, kuhara, magonjwa ya minyoo, malaria na magonjwa ya macho.
Katika
hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Herman Materu,
amesema kuyatibu maradhi hayo ni gharama kubwa ambayo inachangia au
inapelekea jamii husika kuwa maskini.
Amesema
siyo hivyo tu, magonjwa hayo wakati mwingine husababisha vifo ambavyo
mazingira yangekuwa masafi, visingetokea.
Mkuu
huyo wa wilaya, alitumia fursa hiyo kulishukuru na kulipongeza shirika
la Water Aid kwa kufadhili mradi wa ujenzi wa kituo hicho na pia,
amelipongeza shirika la SEMA kwa ujenzi bora wa kituo hicho na kutoa
mafunzo kwa mafundi ujenzi wa vyoo bora.
Awali
Meneja wa SEMA Ivo Manyaku, alisema kituo hicho cha Mwakashanhala
kinatarajiwa kitahudumia wakazi 18,287 wa kata hiyo na kata jirani.
Amesema
gharama ya vyoo hivyo bora ni ya chini kwa vile vifaa vingi
vinavyotumika vinapatikana huko huko vijijini.
Kwa
mfano, amesema mfuko mmoja wa saruji ambao umechanganywa na udongo wa
kisuguu, unatoa matofali bora, zaidi ya 120.
No comments:
Post a Comment