Na Lucas Raphael.Tabora
Makala.
Januari 16 mwaka huu ni siku
ya kukumbukwa katika mkoa wa Tabora, kutokana na mkoa huo kuandika historia
mpya katika nyanja ya elimu nchini. Mkoa huo umeweza kupata Chuo kikuu cha
Kwanza toka Tanganyika ilipopata uhuru wake mwaka 1961.
Kwa muda mrefu Mkoa wa
Tabora haukuwa na vyuo vinavyotoa elimu ya juu hapa nchini hali ambayo
iliufanya mkoa huo ushindwe kupata ustawi mkubwa wa kimaendeleo ikilinganishwa
na mikoa mingine, ambayo ina vyuo vikuu.
Mkoa huo ulikuwa na vyuo
vinavyotoa elimu ya kati tu kama vyuo vya Ualimu ambavyo ni chuo cha Ualimu
Ndala, wilayani Nzega na Chuo cha Ualimu cha Tabora ambavyo vilianza kutoa
huduma hiyo kwenye miaka ya sitini na sabini.
Ukiondoa vyuo hivyo vyuo
vingine vilivyopo ni Chuo cha Utumishi wa Umma, Chuo cha Ardhi na chuo cha
kilimo Tumbi na vyuo vya ufundi vya VETA na vituo vidogo vidogo vya utoaji wa
elimu mbali mbali ndivyo vilivyokuwa vikifanyakazi ya kuwaelimisha wakazi wa
Tabora katika fani Tofauti.
Kabla ya vyuo hivyo Mkoa wa
Tabora, ulikuwa ukisifika sana kutokana na kuwa na shule mahiri za sekondari
ambazo ziliweza kuchangia maendeleo ya taifa hili kikamilifu na kwa ushindani
uliostahili.
Shule hizo ni Pamoja na
Tabora Boys, Milambo sekondari, Tabora Girls, Kazima ambazo kwa pamoja zimetoa
wataalam wengi zaidi hapa nchini pamoja na viongozi wa serikali.
Hata hivyo kukosekana kwa
elimu ya chuo kikuu katika mkoa wa Tabora, kumeufanya mkoa huo uliokuwa
ukisifika kielimu hapa nchini upoteze umaarufu wake wa miaka mingi na kujikuta
ukiwa miongoni mwa mikoa isiyokuwa tena na sifa ya kufanya vizuri katika nyanja
hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Chuo hicho kikuu
kilizinduliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, ambaye
ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo za uzinduzi zilizofanyika
katika uwanja wa Chipukizi mjini hapa.
Katika hotuba yake waziri
Sitta, alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo katika mkoa wa Tabora,
ambao alisema umekuwa nyuma kwa muda mrefu na hivyo kuufanya usiwe miongoni mwa
mikoa yenye maendeleo makubwa kielimu hapa nchini.
Alisema kuwepo kwa chuo
hicho ni maendeleo ya kweli kwa mkoa na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuwa makini
na kushiriki katika utoaji wa mazingira mazuri na kuwapa ushirikiano watumishi,
wahadhiri na wanafunzi ili kuongeza sifa za mkoa huo katika elimu ya juu
nchini.
Aliilaumu bodi ya mikopo
Tanzania kutokana na kushindwa kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini huku akibainisha wazi kuwa utendaji
katika bodi hiyo umejaa urasimu.
Alisema pamoja na Urasimu,
bodi hiyo imekuwa ikifanyakazi zake kwa chuki, upendeleo, dhulma na kufanya
mambo mengine ambayo hayakubaliki katika utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.
Alisema kunahaja ya kufanya
mabadiliko makubwa katika bodi hiyo ili utendaji wake uwe na tija kwa watanzania
wanaotafuta elimu ya juu nchini ili waweze kuja kulitumikia taifa katika nyanja
mbali mbali.
Alisema suala hilo
atalifikisha serikalini kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi wa kina ambao
utasaidia kuboresha utendaji katika bodi ya mikopo nchini ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kuwa watoto wa watanzania wananufaika zaidi na mikopo hiyo ya
kielimu.
Akizungumza katika Ibada
maalum ya ufunguzi wa chuo hicho Askofu mkuu wa kanisa Katoliki Jimbo kuu la
Tabora, Mhasham Paul Ruzoka, alisema kuwa elimu ni kitu muhimu kwa maisha ya
binadamu na kudokeza kuwa Kanisa katoliki linapenda kutoa huduma hiyo kwa
watanzania wote pasipokuwa na ubaguzi wa aina yeyote.
Alisema elimu ni kama Mwanga
unaomuwezesha mtu yeyote kuona na kufanya shughuli mbali mbali za kimaendeleo
na kijamii hapa nchini, huku akisema kuwa kinyume na elimu ni ujinga ambao
unafananishwa na giza nene ambalo linamzuia binadamu kufanya kazi mbali mbali
za maendeleo.
Askofu alisema ni wajibu wa
kila mtu kuhakikisha kuwa anapata elimu ili aweze siyo tu kuishi vizuri bali
pia kuishi maisha ambayo yatamsaidia kumjua na kumthamini Mungu ambaye ndiye
aliyejalia vipawa vya kila namna kwa binadamu.
Alisema kwa kuwa Kanisa
katoliki linatambua umuhimu wa jambo hilo litaendelea kutumia fursa zilizopo
ili kuweza kuendelea kuwasaidia wananchi waweze kupata fursa hiyo muhimu kwa
maendeleo ya umma na kuondoa ubabaishaji katika utoaji wa huduma za kijamii
miongoni mwa watanzania.
Askofu mkuu aliwahimiza
waumini wa kanisa hilo na wale ambao si waumini kukitumia vizuri chuo hicho
kikuu kwa ajili ya manufaa ya kijamii na kudokeza kuwa lengo la kanisa ni
kuhakikisha kwamba ustawi wa watu unakuwabora zaidi kadri miaka inavyoongezeka.
Akizungumza mara baada ya
ibada hiyo maalum ya kufungua chuo kikuu cha Archbishop Mihayo university
College of Tabora ( AMUCTA) ambacho kitakuwa chuo kikuu kishiriki cha mtakatifu
Augustine cha Jijini Mwanza (SAUT) Makamo mkuu wa chuo hicho nchini Dk. Charles
Kitima, alisema ni muhimu watoto wa Tanzania wakinufaika na elimu ya juu.
Alisema katika siku za
karibuni kumeibuka mtindo wa viongozi wa kiserikali kuweka vikwazo kadha wa
kadha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma katika vyuo binafsi wasipatiwe
mikopo na kwamba wanafunzi watakaopewa mikopo ni wale wanaosoma katika vyuo na
taasisi za serikali pekee.
Alisema kauli hiyo ilipingwa
vikali na wakuu wa vyuo binafsi kwa sababu si haki kufanya hivyo na kwamba vyuo
vya elimu ya juu vya binafsi vimeanzishwa kwa ajili ya kuisaidia serikali iweze
kupata wataalam wengi zaidi.
Kulingana na Dk. Kitima,
serikali haiwezi kuwasomesha wanafunzi wote waliomaliza elimu ya kidato cha
sita na kufaulu mtihani kwahiyo ni vyema ikashirikiana na vyuo vikuu vya
binafsi vinavyowapatia vijana elimu hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Alisema ni vyema basi
serikali ikajitahidi kuondoa kero hizo ndogo ndogo zinazowakabili wanafunzi
hasa katika sekta ya mikopo kwani alisema bodi ya mikopo nchini imekuwa
ikionekana kama kikwazo kwa watoto wa wakulima kupata elimu ya juu nchini
Tanzania.
Alisema mikopo ni haki yao
na kwamba wananchi wanapaswa kujua na kutambua kuwa suala la utoaji wa elimu ya
juu nchini ni la lazima na ni haki yao ya kimsingi watoto wao kuipata elimu
hiyo muhimu kwa ustawi wa taifa hili.
Alisema jamii ya wasomi
itaendelea kupinga sera mbovu ambazo hazina tija kwa taifa letu na kubainisha
kuwa jamii hiyo itaendelea kufanya utafiti utakaosaidia kuimarika kwa elimu
nchini ikiwa ni njia pekee ya kupambana na tatizo la kuwa na wataalam wasiokuwa
na sifa zinazotakiwa.
Mkuu wa chuo kikuu cha
Askofu Mkuu Mihayo cha Tabora ( AMUCTA) Dk. Thadeus Mkamwa, alisema kuwa chuo
hicho kikuu kimeanza rasmi novemba 3 mwaka jana, kwa kuanza na mafunzo ya
shahada ya kwanza ya Ualimu kikiwa na wanachuo 886.
Alisema kutokana na mikakati
ya chuo hicho kinatarajia kuanzisha pia shahada za masomo ya sayansi ya jamii,
biashara na sheria ambayo yanatarajia kuleta mapinduzi mazito katika suala zima
litakalosaidia maendeleo ya Taifa hili.
Alisema pamoja na kuanza
fani hizo, alisema katika mipango ya muda mfupi chuo hicho kitaanza kutoa
mafunzo ya elimu ya juu katika fani hizo kwa watu wa makundi maalum ambao ni
walemavu kama wasiosikia, wasiosema na wenye matatizo tofauti.
Alisema kwa mujibu muongozo
wa chuo hicho, kinapaswa kuwa na wanachuo wasiopungua 5000 kitakapokamilika
kimejikita zaidi katika ufundishaji wa masomo ya juu kwa kiwango kizuri na bila
ya kusahau suala zima la maadili ya umma.
Alisema kampasi ya chuo
hicho inatarajia kujengwa katika eneo la Kazima, umbali kama wa kilomita nane
kutoka mjini Tabora, ambapo kazi ya kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa
wakimiliki eneo hilo ikiwa inaendelea.
Aliwataka wakazi wa Tabora
kuwatambua na kuwathamini wanafunzi wa chuo hicho, hasa pale wanapotafuta
makazi kwa ajili ya kusoma wasiwapandishie bei kwa kudhani kwamba wanapesa za
kutosha hivyo kuwakwamisha kufikia malengo yao ya kielimu.
Alisema hao ni watoto wa
masikini kama wao hivyo wanachopaswa kukifanya ni kuwasaidia na si kuwakomoa
kwani kama tujuavyo kuwepo kwa wanachuo kutasaidia pia kukuza maendeleo katika
mji huo kwa sababu mzunguuko wa pesa utaongezeka katika mji huo.
Mkuu wa Chuo, aliwataka
wanachuo kusoma kwa bidii kubwa na kuhakikisha kuwa wanapata taaluma bora zaidi
itakayowasaidia kupata uelewa mkubwa utakaosaidia kuwapa ushindani na kumudu
kufanyakazi mahali popote katika ulimwengu bila ya kuathiri mila na desturi za
wenyeji wao.
Sherehe hizo za ufunguzi wa
chuo hicho zimehudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mji wa Tabora, viongozi wa
chama Tawala na serikali, wabunge, maaskofu wa majimbo mbali mbali nchini na
mapadri wanaoziwakilisha jumuiya mbali mbali katika jimbo Kuu la Tabora.
Mwisho.
|
Thursday, November 29, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment