Serikali ya Tanzania imekitaka kituo cha televisheni cha Kimataifa cha CNN kusahihisha taarifa potofu ilizotoa kuhusu mgogoro wa mpaka unaoendelea kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.
Taarifa hizo zinaonyesha kwamba
mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa upo kwenye ufukwe wa Pwani
ya Tanzania jambo ambalo Serikali imesema siyo sahihi.
Akiongea na waaandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Assah
Mwambene amesema Serikali ya Tanzania imesikitishwa sana na taarifa hiyo
na kuitaka CNN kuisahihisha mara moja.
“Tumesikitishwa sana na taarifa
hiyo na tunashangaa kuona chombo kikubwa kama CNN wanaweza kutoa taarifa
za uongo kwa kiasi hicho” amesema Bw. Mwambene.
Amesema ukweli ni kwamba
unapozungumia eneo la Tanzania kilometa za mraba 947,300 (947,300 sq
km) ikiwa ni pamoja na nusu ya eneo la ziwa kaskazini mwa mpaka wa
Tanzania na Msumbiji na kwamba mpaka upo katikati ya ziwa kama ilivyo
kwa mpaka wa Malawi na Msumbiji.
Kwa muda wa siku tatu kuanzia
tarehe 24 Novemba, 2012, CNN International yenye makao yake Makuu nchini
Marekani imekuwa ikiendesha kipindi kuhusu mgogoro wa Tanzania na
Malawi na kuonyesha kwamba mpaka uko pembezoni mwa ufukwe wa Tanzania.
Bw. Mwambene amesema kuwa suala
hilo hivi sasa linatarajiwa kupelekwa katika Baraza la Marais wastaafu
wa Nchi za Umoja wa SADC kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi.
Wakati huo huo, Sherehe za miaka
51 ya Uhuru wa Tanzania bara zinatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa
Uhuru jijini Dar es salaam Desemba 9 mwaka huu.
Kauli mbiu za sherehe za uhuru mwaka huu ni uwajibikaji , uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI
No comments:
Post a Comment