Friday, November 16, 2012

UGANDA YATHIBITISHA KUWEPO KWA UGONJWA WA EBOLA NCHINI HUMO

Virusi wa Ebola
Virusi wa Ebola

Wizara ya afya nchini Uganda imesema kuwa watu wawili wameaga dunia kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola.

Waziri wa afya Christine Ondoa amesema, watu wawili kutoka jamii moja waliaga dunia mwishoni mwa juma lililopita, katika wilaya moja viungani mwa mji mkuu Kampala.


Inakadiriwa kuwa watu 17 waliaga dunia magharibi mwa Uganda, kutokana na ugonjwa huo mwezi Julai mwaka huu.


Kwa mujibu wa shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres (MSF), hakuna maafa yoyote yaliyoripotiwa kuhusiana na ugonjwa huo hatari tangu mwezi Agosti.


Waziri huyo wa Afya ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa uchunguzi uliofanywa umethibitisha kuwa watu hao waliaga dunia kutokana na ugonjwa huo wa Ebola katika eneo la Luwero, takriban kilomita sitini kutoka mki mkuu Kampala.


Lakini amesema mwanaume mmoja kutoka eneo hilo, pia aliaga dunia mwezi uliopita, kutokana na kile kilionekana kuwa dalili za ugonjwa huo, lakini hakuna uchunguzi uliofanyika kuhusiana na kifo hicho.


Watu watano ambao ni jamaa wa karibu wa walioaga dunia, wanaendelea kuchunguzwa na madaktari. Wawili kati yao wamelazwa katika chumba maalum katika hospital kuu ya kitaifa ya Mulago mjini Kampala.


Hakuna tiba maalum inayojulikana ambayo inaweza kutumika kutibu ugonjwa huo, lakini wagonjwa hupewa dawa za kawaida za kinga pamoja na zile za kupunguza maumivu na kutibu Malaria ili kuongeza kinga mwilini.


Asilimia Tisini ya watu wanaogunduliwa kuwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo wa Ebola huaga dunia, na katika kipindi cha miaka Kumi na mbili iliyopita kumekuwa na visa kadhaa vya mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda.

Takriban asilimia 50 ya yatu 425 ambao walikuwa wameambukizwa virusi hivyo waliaga dunia mwaka wa 2000.


Taarifa hii kwa hisani ya BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment