Thursday, January 17, 2013

ATOROKA GEREZANI NA KUVUA NGUO ILI ASIKAMATWE

Askari Polisi wa kikosi cha FFU Tabora mjini wakijaribu kumdhibiti kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Jonas Oscar(25)ambaye inadaiwa kuwa alitoroka Gereza la mahabusu Tabora maarufu kwa Zuberi wakati akiwa anatumikia kifungo cha mwaka mmoja. 


Na mwandishi wetu maalumu
Mwananchi mmoja kwa kushirikiana na askari wa kikosi cha kuzuia ghasia FFU mjini Tabora wamefanikiwa kumkamata  mfungwa mmoja wa gereza la mahabusu Tabora wakati akifanya jaribio la kutoroka akiwa amevua nguo na kubakia uchi wa mnyama. 

Mfungwa huyo ambaye anafahamika kwa jina la Jonas Oscar(25)imedaiwa kuwa mnamo majira ya mchana siku ya tarehe 14 januari 2013 alifanya jaribio hilo wakati akiwa kwenye kazi za bustanini na wafungwa wenzake.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililokuwa kama mchezo wa kuigiza mfungwa huyo alilazimika kuvua nguo zote(sare za kifungwa) ili isiwe rahisi kumkamata na kuanza kutokomea mitaani.

Hata hivyo wakati akiwa ameanza safari hiyo ya kukwepa kifungo cha mwaka mmoja ambacho ameanza kukitumikia mapema mwaka huu,mfungwa huyo Jonas aliibukia katika kambi ya Jeshi la Polisi iliyoko jirani na gereza hilo la mahabusu hatua ambayo ilisababisha kuonwa mapema kwakuwa alionekana kuwa ni mtu wa ajabu kwa kukimbia akiwa uchi wa mnyama.

"Nilipomuona niliamua kumkimbiza na kutaka kujua anatatizo gani,nilimkamata na kuwaomba msaada FFU waliokuwepo hapo jirani na Kituo chao"alisema mwananchi huyo ambaye alijifahamisha kwa jina la Mapinduzi

Aidha katika hatua nyingine mfungwa huyo amefikishwa mahakama ya wilaya ya Tabora,mbele ya hakimu Mheshimiwa Magori na kukabiliwa  kwa kosa la kutoroka chini ya ulinzi halali kinyume cha sheria namba 16 kifungu cha 116 ya mwaka 2002,ambapo alihukumiwa kutumikia adhabu kwenda jela kwa kifungo cha miezi 16,adhabu ambayo ameanza kuitumikia mara moja.

Awali Jonas Oscar imedaiwa kuwa alikuwa akitumikia kifungo cha mwaka mmoja akiwa ni mfungwa No.02,2013 katika Gereza la mahabusu Tabora mjini baada ya kupatikana na hatia ya kutishia kumuua baba yake mdogo huko katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.   

No comments:

Post a Comment