Sunday, January 20, 2013

SERIKALI KUTUMIA VIJIJI VYA MILENIA MBOLA KAMA MFANO WA KUONDOA UMASIKINI NCHINI

 

Na Lucas Raphael ,Uyui.

Vijiji vya Millenia

SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kusambaza teknolojia na mbinu
zilizotumika katika kijiji cha millennia Mbola mkoani Tabora, zitumike
katika vijiji vyote hapa nchini, ili kuweza  kuutokomeza umasikini kwa
haraka na kutimiza malengo 8 ya milenia.

Waziri Fedha Dkt William Mgimwa, aliyasema hayo katika kijiji cha
Ilolangulu, wakati akifungua zahanati ya kijiji hicho iliyogharimu
shilingi milioni 49,iliyoko wilaya ya Uyui mkoani Tabora,wakati
akizungumza na wakazi wa vijiji  16 vya millennia Mbola , ambapo
aliwapongeza kwa kazi nzuri na jinsi walivyoupokea mradi huo, ambao
leo ni kielelezo, umekuwa wa mfano.

Alisema kwamba ni vema wananchi wakahakikisha miradi yote
iliyotekelezwa chini ya mradi wa vijiji vya millennia mbola, inatunzwa
vizuri ili iwe daraja la kufundishia vijiji vingine nchini katika
utekelezaji wa malengo 8 ya Milenia .

Waziri Mgimwa, aliyefika kijiji hapo kwa ajili ya kujifunza na
kujionea jinsi mradi huo shirikishi wa kijiji cha Milenia
unavyooendeshwa na Umoja wa mataifa ulivyoweza kupambana na umasikini
kwa wakazi wa vijiji 16 vya wilaya ya Uyui.

Awali Mratibu wa mradi wa kijiji cha Milenia cha Mbola mkoani Tabora,
Dkt Gerson Nyadzi, alisema kuwa wakazi wa kijiji hicho wameweza kupiga
hatua kubwa ya maendeleo baada ya kuwezeshwa na serikali na mradi wa
kijiji hicho kwa kupewa pembejeo ili kuweza kuondokana na umasikini
uliokithiri iliyowawezesha wakulima kulima na kuvuna zaid ya magunia
20 hadi 40 kwa heka moja ya mahindi .

Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Ilolangulu Ali Magoha, alisema kuwa
mradi wa kijiji cha millennia unaojumlisha vijiji 16 umefanikiwa kwa
kutimiza malengo yote 8 yaliyokusudiwa kwa kiwango cha zaidi ya
asilimia 85.

Alitaja manufaa ambayo wameweza kupatikana toka mradi wa vijiji vya
milenia Mbalo ulipoanza ni pamoja na  ujenzi wa nyumba za kisasa za
matofari ya kuchoma na bati ,uzalishaji wa mazao ya chakula
umeongezeka .

Pia alisema kwamba mradi huo umesaidia kupunguza tatizo la vifo vya
watoto chini ya miaka 5 na vifo vya akina  mama wajawazito.

Alisema hapa awali vifo hivyo vilikuwa wastani wa watoto 3 nadi
5katika kipindi cha miezi mitatu na kinamama 5 kwa kila mwezi lakini
kwa sasa wastani huo ni kwa kipindi cha miezi 6 na wakati mwingine
hakuna kabisa.

Magoha alisema kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya wananchi kupata
elimu juu ya kutumia vyandarua na kuua mazalia ya mbuhivyo kupunguza
kasi ya maradhi yan malaria katika eneo hilo..

Mwenyekiti huyo wa serikali ya vijiji vya mrai wa vijiji vya Millenia
Mbola akizungumzia swala la elimu alisema kwamba kwa sasa kiwango cha
wanafunzi wanaoacha masomo imepungua tangu mradi huo umeanza na kuwa
sasa wanafunzi wengi wanamaliza masomo ua darasa la saba .

Alitaja mbinu hizo ni pamoja na kutoa chakula kwa wanafunzi na
kuhamasisha michezo mashuleni hivyo wakuwavutia watoto wengi kujiunga
na shule .

Kuhusu suala la maji alisema kwamba wanaendelea vizuri ambapo wastani
wa asilimia 60 ya wakazi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama
tofauti na ilivyokuwa awali .

Naye Mbunge wa jimbo la Tabora kaskazini Shaffin Sumar, aliishukuru
serikali kwa kuendelea kuchochea maendeleo katika vijiji vyote 16 vya
millennia kwa kuanza mchakato wa kupeleka umeme katika vijiji hivyo
vyote ili kusaidia kukua kwa maendeleo ya haraka.

No comments:

Post a Comment