Sunday, January 13, 2013

TAREFA YAANZA KAZI BILA KUKABIDHIWA VYA OFISI


 Mwenyekiti wa Chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora Yusuph Kitumbo akizungumza katika kikao cha kwanza cha kamati tendaji ya Chama hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Frankman Hotel mjini Tabora.
 Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kamati tendaji wakitoa hoja na maoni mbalimbali katika kikao hicho kilichofanyika Frankman Hotel.

Mwandishi maalum,Tabora

Wajumbe wa kikao cha kamati tendaji ya Chama cha mpira wa miguu mkoani Tabora Tarefa leo wamejikuta katika wakati mgumu na kulazimika kuendesha mkutano wao pasipo kuwa na vifaa na nyaraka mbalimbali za chama hicho kufuatia viongozi waliomaliza muda wao kutokabidhi vifaa hivyo tangu waachie madaraka mwishoni mwa mwaka jana.

Mwenyekiti wa Tarefa Yusuph Kitumbo pamoja na kuzungumzia mambo kadhaa  kama hatua ya kwanza kwa uongozi mpya tangu uchaguliwe,wakiwa katika kikao hicho cha kamati tendaji  alilazimika kupiga simu kwa aliyekuwa katibu wa Chama hicho Albert Sitta kumtaka arejee barua aliyoandikiwa kukabidhi vifaa vya ofisi, hatua ambayo itawezesha uongozi mpya kupata fursa ya kuanza kutumikia Chama hicho kikamilifu.

Katika mahojiano ya simu Yusuph Kitumbo walikubaliana na Katibu huyo wa zamani Albert Sitta kuwa anataraji kukabidhi vifaa hivyo mnamo siku ya jumatatu tarehe 14 Januari 2013 saa nne na nusu asubuhi ingawa haijajulikana ni wapi makabidhiano hayo yatafanyika.

Hata hivyo kikao hicho cha kamati tendaji kiliendelea pasipokuwa na nyaraka mbalimbali za kumbukumbu za Chama hicho na hivyo kufanya utaratibu wa kikao kuwa mgumu.

Pamoja na maadhimio kadhaa yaliyofikiwa na Tarefa lakini Chama hicho kimeendelea kuwa na wakati mgumu kwa madai kwamba uongozi uliopita umepoteza mvuto kwa baadhi ya wadau wa soka pamoja na kutoaminiwa na Viongozi wa Serikali ya mkoa wa Tabora.

Kitumbo aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa bado kuna kazi mgumu ya kujaribu kurejesha heshima ya uamini kwa Chama hicho ili kiweze kupata misaada kutoka kwa wadau wa soka wa ndani na nje ya mkoa waliokuwa wamekisusia kwa muda mrefu.

"Jamani uongozi uliopita tayari umekiathiri sana Chama chetu,na hii imetokana zaidi na migogoro ya mara kwa mara ya viongozi jambo ambalo hata kwa sisi viongozi wapya  limetufikisha kupoteza mvuto kabisa kwa Serikali ya mkoa wetu"alisema Kitumbo huku akiwatahadharisha wajumbe kuwa makini ikiwa ni pamoja na kuepukana na  tabia ya kuzungumzia mambo ya chama hicho nje ya vikao visivyo rasmi. 

Aidha uongozi mpya wa Tarefa uliingia madarakani mnamo Desemba 22 mwaka jana baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Chama hicho.     

 

No comments:

Post a Comment