Bi.Hadija Mwangatwa mkazi wa
kijiji cha Ndevelwa manispaa ya Tabora akijaribu kutayarisha mihogo ili
akauze aweze kununua debe la mahindi.
Na mwandishi wetu Tabora.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida
tayari imeripotiwa kuwa vijiji vitatu kata ya Ndevelwa manispaa ya
Tabora viko hatarini kukumbwa na njaa hali ambayo imetishia wakazi zaidi
ya 6790 waishio kwenye vijiji hivyo.
Wakazi wa vijiji vya kata ya
Ndevelwa tayari imebainika kuwa wamekuwa wakila mlo mmoja kwa siku na
wengine hata kupitisha siku nzima pasipo kupata chakula.
Akizungumza na mwandishi wetu
diwani wa kata ya Ndevelwa Bw.Seleman Maganga amekiri kuwepo kwa hali
hiyo huku akiitaka serikali kuchukua juhudi za makusudi kukabiliana na
janga hilo linalovinyemelea vijiji hivyo.
Diwani huyo Bw.Maganga amesema
tatizo hilo ni matokeo ya hali ya ukame iliyovikumba vijiji hivyo tangu
mwishoni mwa mwaka jana,na tayari amekwisha lifikisha kwenye vikao vya
baraza la madiwani na kujadiliwa.
Maganga amefafanua kuwa kwa upande
mwingine hali hiyo imechangiwa na idadi kubwa ya vijana waishio vijiji
vya Inala,Ituru na Ndevelwa kutoshiriki shughuli za kilimo hata cha
bustani na kuwaachia wazee peke yao ambao huzalisha kidogo kulingana na
uwezo wao.
Aidha alisema idadi kubwa ya
vijana wamekuwa wakikimbilia mjini na wale wanaobaki hapo vijijini
hujihusisha na vitendo vya kiharifu ilimradi kujihakikishia kipato
kisicho cha halali.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa
vjijiji hivyo waliolima zao la Muhogo wanalazima kuuza madebe mawili kwa
shilingi elfu kumi na sita ili wakanunue debe moja la mahindi ambalo
wanadai kuwa ndio linatosheleza kwa mlo wa siku saba katika familia
moja.
Mnamo mwaka 2010 oktoba serikali
ilitoa chakula cha msaada baada ya vijiji hivyo vya kata ya Ndevelwa
kukubwa na mvua kubwa iliyoharibu mazao ya chakula na biashara kama
tumbaku na mahindi.
No comments:
Post a Comment