Thursday, November 1, 2012

WANANCHI SASA KUTUMA MAONI YAO KUHUSU KATIBA MPYA KWA SMS


Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza namba nne (04) za simu za mkononi ambazo wananchi kwa sasa wanaweza kuzitumia kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (‘sms’) kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume hiyo kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo (Jumatano, Oktoba 31, 2012) namba ambazo wananchi wanaweza kutuma maoni yao kwa njia ya ‘sms’ ni 0715 (Tigo) /0767 (Vodacom) / 0787 (Airtel) / 0774 (Zantel) – 08 15 08.
“Kwa kuzingatia kuwa Watanzania wengi waliopo mijini na vijijini wanamiliki simu za mkononi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaamini kuwa njia hii ni fursa nyingine muhimu kwa Watanzania kuweza kuwasilisha maoni yao kwa Tume,” imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid.
Ili kutuma maoni, Bw. Assaa amesema, mwananchi anapaswa kufungua ukurasa wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) katika simu yake na kuandika maoni yake pamoja na jina lake kamili, jinsia, mahali anapoishi, umri, elimu na kazi na kutuma kwenda kwenye namba yoyote kati ya zilizotolewa.
Kwa mujibu wa Bw. Assaa, baada ya kutumwa, maoni hayo yatakwenda kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambapo yatafanyiwa kazi pamoja na maoni yanayokusanywa kwa njia nyingine.
Uanzishwaji wa njia hii ya ujumbe mfupi wa maandishi unalenga kuwapa fursa nyingine wananchi kutoa maoni yao. Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia inapokea maoni ya wananchi kupitia mikutano ya ana kwa ana; barua pepe (maoni@katiba.go.tz); njia za posta (S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P. 2775, Zanzibar); ukurasa wa ‘facebook’ (Tume ya Mabadiliko ya Katiba) na tovuti (http://www.katiba.go.tz/).
Katika taarifa yake hiyo, Tume imewaomba wananchi kutumia namba hizo kutuma maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya bila kushawishiwa na watu, makundi, vyama au taasisi yoyote na kufafanua kuwa  Tume inatarajia kuanza kupokea maoni ya makundi, vyama na taasisi mara baada ya kumaliza kukusanya maoni binafsi ya wananchi katika awamu ya nne na ya mwisho itakayomalizika mwezi Desemba, 2012

No comments:

Post a Comment