Sunday, September 2, 2012

WATAKA WANAOWAPA MIMBA WANAFUNZI WANYONGWE

NA Lucas Raphael,Tabora
WANANCHI wa jimbo la Bukene, wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamependekeza kwamba, kwenye katiba mpya ijayo, kuwe na kipengele kitakachotoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mtu yoyote  atakaye bainika na kosa la kumpa mimba mwanafunzi wa kike ilikupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi huo hasa maeneo ya mijini na vijijini.

Kauli hiyo waliitoa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakichangia mawazo yao kwenye mdahalo wa wananchi juu ya mchakato wa kupata katiba mpya, ulifanyika katika ukumbi wa Igembe Nsabo  mjini Bukene.

Bahati Ramadhani ambaye alikuwa ni mmoja wa washiriki wa  mdahalo huo,  alisema kuwa kwenye katiba mpya, kuwe na kifungu kitakachompa adhabu ya kunyongwa Mwanaume yoyote atakaye tiwa hatiani na mahakama kuwa amempa mamba mtoto wa kike anaesoma shule aidha ya msingi au sekondari.

Alisema kwamba licha ya sasa kuwepo na adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu anayempa mimba mwanafunzi wa kike, lakini watu hao bado wanaendeleza tabia hiyo na kufanya maisha ya watoto hao wa kike kuwa magumu baada ya kupewa mimba sanjali na kutelekezwa na kubaki wanahangaika na watoto wao.

“Hiyo adhabu ya jela miaka 30 kwa mtazamo wangu mimi, haitoshi, hapa suruhisho ni kunyongwa tu, maana wakishanyongwa kama watu wawili kwa kosa hilo nadhani wataogopa” alisema   Bahati.

“Harafu sioni kama itakuwa dhambi kwa watu hao kunyongwa maana nao ni wauaji pia, hivi karibuni mtoto wangu wa kidato cha pili, kapewa mimba na baada ya kupewa huo ujauzito yule bwana alikimbia na hadi sasa hajulikani mahali alipo, sasa kwa nini huyu mtu asinyongwe? Alihoji  Bahati.

“Niwaombe wananchi wenzangu watakapo kuja kina Wariaoba na tume yao tuwe makini kutoa maoni yetu bila woga” alisisitiza ,Bahati.
Nae Sospeter Kasiga alisema kwamba, katiba mpya ni lazima impunguzie madaraka Rais wanchi ili asiwe na mamlaka ya kuteuwa mawaziri, wakuu wa Wilaya na mikoa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki ya msingi wananchi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Bunge ni  moja ya mihimili mitatu ya nchi, sasa unapomteua tena mbunge kuwa Waziri maana yake nini,huyo tayari ni mhimili anayetokana na bunge harafu unamteua kuwa mhimili tena katika baraza la mawaziri, hayo ni matumizi mabaya ya madaraka ya Rais yanayotokana na ubovu wa katiba iliyopo sasa” alisema   Kasiga.

Alibainisha kuwa katika katiba mpya ijayo iainishe kwamba wakuu wa mikoa na wilaya wachaguliwe kwa kupigiwa kura na wananchi badala ya ilivyo sasa kuteuliwa na Rais na kwamba mawaziri wasitokane na ubunge bali watume maombi ya kazi.

Mdahalo huo uliandaliwa na umoja wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wilayani Nzega (UWAZIKI) na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society kutoka jijini Dar es salaam, ambapo mwezeshaji wa mdahalo , Christopher Nyamwanji, alisema kuwa lengo la kuu ni kutoa uamsho kwa jamii ili siku ya kutoa maoni kuhusu katiba mpya ijitokeze na kutoa maoni yao bila woga.

Mwisho..

No comments:

Post a Comment