Friday, September 21, 2012

WILAYA YA SIKONGE YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA WATUMISHI.

 Na mwaanshi wetu Sikinge
HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora licha ya kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wake inakabiliwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku kwa sababu ya upungufu wa watendaji katika idara mbalimbali za halmashauri hiyo.
 
Akizungumza na mwandishi wetu, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. Paul Nkulila alibainisha kuwa athari zinazotokana na upungufu huu wa watumishi ni utoaji wa huduma usioridhisha, pamoja na watumishi kukosa ari ya kufanya kazi kwa kuwa mtumishi mmoja kwa wastani anafanya kazi ya watu wawili hadi watatu jambo ambalo huchangia ucheleweshaji wa shughuli nyingi za kimaendeleo ndani ya halmashauri hii.
 
Bw. Nkulila alisema kuwa idara zilizoathirika kwa upungufu wa watendaji  kwa kiasi kikubwa ni  idara ya  Afya, idara ya Elimu ya Msingi na Sekondari, Utawala, Kilimo, Mifugo na Ushirika. Idara zingine zenye mapungufu kidogo ni Manunuzi, Ukaguzi wa ndani, Ujenzi, Sheria na Maji.
 
Aidha Bw. Nkulila alitaja sababu kuu za upungufu huu wa watumishi kuwa ni mazingira yasioridhisha kufanyia kazi ambayo huwafanya watumishi wengi kufika na kuhama baada ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi wanaofanyia kazi vijijini mfano walimu na watoa huduma za afya.
 
Akitoa takwimu za upungufu wa watumishi katika halmashauri hii Afisa Utumishi wa halmashauri hii Bi. Flora Malima alisema kuwa  idara ya Afya ina upungufu wa watumishi 271 katika vituo mbalimbali vya Afya  kati ya mahitaji ya watumishi 511, idara ya Elimu ya Msingi ina upungufu wa waalimu 270 kati ya 876 wanaohitajika wakati  Elimu ya Sekondari inaupungufu  wa waalimu 129 kati ya 270 wanaohitajika.
 
Aidha Bi. Malima  aliongeza kuwa idara ya Utawala katika kada zake zote kuanzia maofisa wa vijiji, kata hadi wilaya ina upungufu wa watumishi 63 kati ya 150 wanaohitajika, idara ya Maji ina upungufu wa watumishi 6 kati ya 20 wanaohitajika, idara za Ushirika, Kilimo na Mifugo kwa pamoja  zina upungufu wa watumishi 53 kati ya 116 wanaohitajika wakati idara ya Manunuzi ina upungufu wa watumishi 4 kati ya 6 wanaohitajika na idara zilizobaki zina upungufu wa watumishi kati ya 1 na 2.
 
Bi.Malima akifafanua mikakati ya kumaliza tatizo hilo , alisema kuwa mwaka jana waliomba kibali cha kuajiri ila hawakupata, hivyo wamepanga kuomba tena mwaka huu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya kujaza nafasi za kada mbalimbali.
 
Aidha Bi. Malima alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuongeza nyumba za watumishi ambapo kwa kuanzia tayari wamepata fedha kiasi cha sh. million 200 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 10 za watumishi wa afya kwa mwaka huu wa fedha, lakini pia wanafikiria uwezekano wa kuwa na utaratibu wa kuwalipia pango watumishi wanaopangiwa kituo cha kazi hapa wilayani Sikonge.

No comments:

Post a Comment