Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi –Zanzibar
ZANZIBAR ALHAMISI NOVEMBA 01, 2012. Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, ameagiza
kukamatwa kwa wale wote walioshiriki katika vurugu zilizopelekea uporaji
na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ya barabara za mjini wa
Zanzibar, wasakwe na kukamatwa ili wafikishwe mahakamani.
IGP
Mwema ametoa agizo hilo mjini Zanzibar wakati akizungumza kwenye baraza
la Askari lililohudhuriwa pia na Makamanda wa Polisi wa mikoa mitatu ya
Unjuja kuhusiana na vurugu zilizotokea mwezi uliopita na kupelekea kifo cha Askari Koplo Saidi Abdarahamani Juma.
Akizungumzia
kuuawa kwa Askari Koplo Saidi, IGP Mwema amesema mtu yeyote
aliyeshiriki katika vitendo hivyo ambavyo vimepelekea taathira kubwa ya
uvunjifu wa amani katika mji wa Zanzibar na viunga vyake, ni lazima
apelelezwe na popote alipo akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.
Amesema
kumuua Askari mmoja ni sawa na kuathiri huduma za kiusalama kwa watu
zaidi ya 1,300 na kwa nafasi ya askari mwenye cheo cha Koplo kama
Marehemu Saidi, mwenye uwezo wa kuongoza Askari wenzake wanane hadi
kumi, atakuwa amewanyima haki watu wengine zaidi ya watu 13,000 kutokana
na vitendo vya uhalifu.
IGP
Mwema amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Askari Polisi na Askari na
maafisa wa Vyombo vingine vya ulinzi na usalama na kusema kuwa
ushirikiano huo ndio ulioleta mafanikio ya kuwakamata washiriki wa
makosa na hatimaye kuleta ushwari katika kisiwa cha Zanzibar.
Amesema
nia ya Serikali ya kusajili vikundi mbalimbali vikiwemo vya kidini, ni
kutaka kuleta maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa Jamii na maendeleo ya
kiusalama na kudumisha amani na utulivu wa taifa letu na kwamba hakuna
Serikali yoyote Duniani inayoweza kuruhusu vikundi kama hivyo vigeuke
kuwa vyenye kuleta vurugu na machafuko ya taifa husika.
Amesema
amefurahishwa na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.
Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, za kuwatia
moyo askari na kukemea vikali vitendo vya vurugu za kidini zilizopelekea
machafuko visiwani zanzibar na Dar es Salaam.
Awali Kamishna
wa Polisi Zanzibar CP. Mussa Ali Mussa, amesema kuwa Jeshi la Polisi
visiwani hapa linafanya operesheni ya kisayansi ya kuwasaka na kuwanasa
wale wote waliohusika katika vurugu za hivi karibuni na zile zilizopita
kwa kutumia picha za kawaida na za video ili kumbaini kila mtu
aliyeshiriki katika matukio hayo.
Kamishna
Mussa amesema hadi sasa watuhumiwa 98 wamekamatwa na 35 kati yao
wamefikishwa Mahakamani na wengine wanaendelea kuhojiwa na
watakaothibitika kushiriki katika matukio hayo watafikishwa mahakamani
kuunganishwa na wenzao.
Amesema
tayari Makachero wa Jeshi Polisi wamepata picha 72 pamoja na CD na DVD
zenye kuonyesha sura za washiriki wa vurugu katika maeneo mbalimbali ya
mji wa Zanzibar na shughuli ya uchambuzi na utambuzi wa kuwabaini na
maeneo wanaoishi inaendelea na kila atakayebainika atakamatwa na
kufikishwa mahakamani.
Amesema
picha hizo zimesambazwa katika vituo mbalimbali vya Polisi na ofisi za
Vikosi vya usalama Zanzibar pamoja na vyombo vya Habari ili kuwafuatilia
na kuwakamata wahusika hao kwa hatua zaidi.
..............Mawasiliano
Simu 0784 886488, 0715 886488, 0767 886488 Insp. Mohammed Mhina. Afisa
Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar.......................
No comments:
Post a Comment