Thursday, November 1, 2012

DIWANI AMKWIDA MTU KWA UTAPELI MAHAKAMANI TABORA


Kumwami Mwongezya akiwa chini ya ulinzi wa Polisi
 
Diwani wa CCM kata ya Igigwa wilaya ya Sikonge Saada Said Sizya  amejikuta akimkwida mtu mmoja kwa kutapeli kiasi cha Shilingi mil.moja na laki mbili akidai kutumwa na hakimu ili aweze kufuta kesi inayowakabili watu 26 waliokamatwa ndani ya hifadhi ya Nyahua iliyoko wilayani Sikonge.

Katika tukio hilo lililokuwa kama mchezo wa sinema eneo la Mahakama ya hakimu mkazi Tabora,diwani huyo Saada Sizya ambaye alifika kwa lengo la kutaka kuwasaidia watuhumiwa hao 26 wanaoishi eneo la Mwamsonga lililopo kwenye kata yake alipata habari kutoka kwa mmoja kati ya ndugu waliofika mapema mahakamani kwa hatua zaidi za kushughulikia kesi hiyo kuwa tayari kuna mtu wamekwisha mpatia kiasi cha shilingi mil.moja na laki mbili alizodai ametumwa na hakimu  anayeshughulikia kesi hiyo ili watuhumiwa hao waweze kuachiwa huru.

Saada Said Sizya diwani kata ya Igigwa-Sikonge
Hali hiyo ilimtia mashaka diwani huyo na kutaka aoneshwe mtu huyo ambaye alifahamika kwa jina la Kumwami
Mwongezya(60),ambapo sasa diwani Saada alitupa mkoba wake pembeni na kumkwida huku akiomba msaada kwa askari Polisi waliokuwapo mahakamani hapo.

Hata hivyo mtu huyo Kumwami ambaye ni mkazi wa kata ya Ilolangulu alijaribu kujitetea kwa diwani huyo huku akimvutia pembeni ya eneo la mahakama alitoa kiasi cha shilingi elfu hamsini za noti ya elfu kumi kumi huku akiomba wazungumze kimyakimya jambo ambalo lilidhihirisha kuwa mtu huyo ni kweli amechukua kiasi hicho cha fedha.

Baada ya askari Polisi kumkata na kumfunga pingu Kumwami alikiri kuchukua kiasi cha shilingi mil.moja na laki moja taslimu na laki moja iliyobaki aliipokea kupitia M-pesa kwa madai ya kusaidia kutoa hongo ili kufuta kesi ya watuhumiwa hao 26 wanaokabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kuingia na kuweka makazi ndani ya hifadhi ya msitu wa Nyahua kinyume cha sheria namba 14 ya mwaka 2002 kifungu 84(1)(a) na (5).

Licha ya kukubali kutenda kosa hilo la utapeli Kumwami hadi anatolewa mhakamani hapo kupelekwa kituo cha Polisi ili akafunguliwe jarada lakini hakuwa tayari kumtaja hakimu aliyemtuma kufanya hivyo.

Aidha kwa upande mwingine watuhumiwa hao wapatao 26 wakiwemo wanawake watano na wanaume 21 walilirudishwa mahabusu baada ya kusomewa mashitaka matatu na mwanasheria wa serikali Miraji Kajiru mbele ya hakimu mkazi Jocktani Rushwela ambaye aliisogeza mbele kwa muda wa siku moja kesi hiyo kwa madai ya kusubiri ushahidi upande wa mashtaka.

No comments:

Post a Comment