Meneja
wa Sekta Kupunguza Umaskini na Kusimamia Maendeleo ukanda wa Afrika wa
Benki ya Dunia Dkt Albert Zeufack, akongea wakati wa mkutano na
wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya Gesi asilia
nchini, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa pamoja na Timu ya
wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na inayowakilisha Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa,
Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akongea wakati wa mkutano na
wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya Gesi asilia
nchini. Nyuma yake mwenye laptop ni Meneja wa Sekta Kupunguza Umaskini
na Kusimamia Maendeleo ukanda wa Afrika wa Benki ya Dunia Dkt Albert
Zeufack, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa pamoja na Timu ya
wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na inayowakilisha Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa,
Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya
waandishi wa habari baada ya mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es
salaam leo kuhusu sekta ya Gesi asilia nchini.Mkutano huo ulihudhruiwa
pia na mabalozi wa nchi kadhaa pamoja na timu ya wataalam walioletwa na
washirika wa maendeleo na inayowakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika,
Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya
na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani ilipotembelea Ikulu jijini Dar
es salaam leo. Wa pili kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Bw. Mathias
Chikawe, akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu Ikulu Mama Suzan Mlawi na
maafisa waandamizi wa Ofisi ya Rais, kamati hiyo
Katika
miaka ya karibuni kumekuwepo kwa ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini
Tanzania katika maeneo ya mwambao na maeneo ya kina kirefu cha bahari
ambapo mpaka sasa jumla ya futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa. Kazi
ya utafutaji inaendelea na upo uwezekano wa ugunduzi zaidi.
Kiasi hicho kilichothibitika hadi sasa hakitoshi kutuingiza kwenye ligi
ya wazalishaji gesi wakubwa duniani. Hata jirani zetu Msumbiji wanayo
gesi asilia iliyothibitika nyingi zaidi kuliko sisi.
Lakini kiasi cha gesi asilia kilichothibitika katika nchi yetu
kinatosha kutuwezesha kuwa wazalishaji muhimu wa gesi asilia, na
tukijipanga vizuri na kuisimamia kwa umakini sekta hii ndogo, inaweza
kutusaidia kuharakisha maendeleo.
Kinyume chake, tusipojipanga na kuisimamia vizuri tunaweza, kama nchi,
tusipate faida kubwa. Mbaya zaidi ipo mifano ya kutosha ya nchi ambazo
uvumbuzi wa gesi na mafuta umevuruga uchumi wao.
Hivyo, kabla hatujaenda mbali ni muhimu kama taifa tuwe na uhakika wa
tunachokitaka na tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ikiwemo
kwenye kutunga sera, kuandaa mkakati na kutunga sheria itakayosimamia
uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi.
Katika kufanya hivyo, hatuna sababu ya kuvumbua upya gurudumu. Duniani
upo uzoefu wa kutosha wa nchi ambazo hazikusimia vizuri sekta hii na
kuharibiwa. Ipo pia mifano na uzoefu wa kutosha wa waliosimamia vizuri
na kufanikiwa.
Sisi tunaoanza leo tuna fursa ya kuepuka makosa waliyofanya wengine na
tuna fursa ya kuchukua uzoefu wa waliofanya vizuri. Lakini lazima
tuchukue hatua sasa. Tukichelewa itakuwa vigumu kurekebisha makosa
baadaye.
Serikali
imepania tusifanye makosa na inaandaa utaratibu bora wa kusimamia
uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi asili. Tunataka kuhakikisha
kunakuwepo uwajibikaji, uwazi na uongozi bora ili Taifa letu lipate
mapato stahiki yatokanayo na uvunaji wa rasilimali hii, na mapato hayo
yatumike vizuri kama msingi wa kujenga uchumi endelevu wa kisasa,
utakaonufaisha wananchi wengi zaidi.
Mchakato
wa kupata maoni ya wadau wote ndani ya nchi unaendelea, lakini pia
tunahitaji uzoefu na ushauri kutoka kwingine duniani. Na ndio maana kwa
karibu wiki moja sasa tumekuwa na ugeni wa Timu ya wataalam walioletwa
na washirika wa maendeleo kutokana na maombi yetu. Timu hiyo
inawakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la
Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza
na Ujerumani.
Tumekuwa na majadiliano kadhaa na Timu hii ambayo imekutana na wadau
mbalimbali ikiwemo Serikali, taasisi za umma, makampuni ya utafutaji wa
mafuta na gesi, sekta binafsi, asasi zisizo za kiserikali, wanazuoni,
baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani na wenyeviti wa Kamati za
Bunge. Mikutano hii ililenga kuipa Timu hii mawazo na maoni wa wadau
muhimu ndani ya Tanzania ili wayazingatie katika ushauri wao kwetu.
Mazungumzo yote yalikwenda vizuri na yana manufaa makubwa.
Napenda kusisitiza mambo yafuatayo:-
(i) Timu
hii tumeiomba sisi. Kama mnavyoona ina uwakilishi mpana wa Washirika wa
Maendeleo. Hivyo, badala ya kujadiliana na mmoja mmoja tumepata fursa
ya kuzungumza nao wote kwa pamoja.
(ii) Uamuzi
wa mwisho kuhusu sera, mkakati na sheria zitakazotawala sekta hii, ni
wetu kwa asilimia mia moja. Lakini katika kuamua tunataka tupate uzoefu
wa wengine, ushauri wa kitaalam na taarifa zote muhimu za kutuwezesha
kufanya maamuzi sahihi. Kwa mfano, tunachohitaji kutoka kwa Timu hii
ni:-
(a) Uzoefu
wa nchi ambazo zimefanya vibaya katika kusimamia sekta zao za mafuta na
gesi asilia. Lengo ni kuhakikisha hatufanyi makosa waliyofanya wengine.
(b) Uzoefu
wa nchi ambazo zimefanya vizuri katika kusimamia sekta hii. Lengo ni
kuzingatia yale yote yaliyothibitika kwa wengine kuwa ni ya manufaa.
Mambo ya msingi kwa upande wa Serikali ni kuhakikisha:-
(a) Tunakuwa
na mikataba bora inayolinda maslahi ya taifa lakini bila kukosa mvuto
kwa wawekezaji. Hivyo tunahitaji kujenga uwezo mkubwa kwenye eneo hili.
(b) Tunahimiza wajasiriamali wetu wajiandae kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya gesi ili kupata manufaa zaidi kutokana na gesi.
(c) Tunaandaa watalaam na mafundi wanaoweza kuajiriwa na makampuni ya gesi.
(d) Tuna
mfumo thabiti wa kusimamia matumizi ya mapato yakatakayotokana na gesi
ili yasiyumbishe uchumi mkuu wa nchi bali yawe msingi wa uwekezaji
katika kubadili mfumo wa uchumi wetu na maendeleo endelevu.
(e) Tuna mfumo thabiti na uwezo wa usimamizi na udhibiti.
Pamoja
na hayo ni muhimu wananchi waelewe kuwa hatutakuwa matajiri mara moja.
Hatutarajii mapato katika miaka michache ijayo. Isitoshe lazima
tufikirie vizazi vijavyo. Sisi tulio hai leo ni wadhamini wa kile
ambacho vizazi vijavyo vitarithi kutoka kwetu. Hivyo itabidi tufikiri
vya kutosha na kuamua kiasi gani cha mapato tutakayopata kitumike leo na
kiasi gani kitumike kujenga msingi wa maisha bora ya vizazi vijavyo
hasa ikizingatiwa kuwa kuna siku gesi hiyo itakwisha.
Nawashukuru washirika wa maendeleo waliotoa wajumbe kushiriki kwenye
timu hii. Pia nawashukuru wajumbe wenyewe kwa ushirikiano mzuri
waliouonyesha wakati wa zoezi hili.
Aidha nawashukuru watanzania walioshiriki na kutoa maoni yao hata kufanikisha zoezi hili.
Kwa pamoja tuhakikishe Tanzania inakuwa mfano bora wa matumizi sahihi
ya rasilimali hii kwa faida na maendeleo yetu na vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment