Kamishna wa Polisi Zanzibar,Mussa
Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kwamba watuhumiwa hao (majina
yanahifadhiwa) walikamatwa sehemu tofauti, mmoja amekamatwa Kisiwa
kidogo cha Tumbatu, wa pili maeneo ya Mjini Unguja,mtuhumiwa wa tatu
alikamatwa ofisi za Idara ya Uhamiaji alikokwenda kushughulikia hati ya
kusafiria ili aweze kutoroka hapa nchini.
Kamishna Mussa alisema watuhumiwa
wengine watatu wamekamatwa Mkoani Tanga ambako walikimbilia kujificha
baada ya kufanya mauaji ya Afisa Polisi Koplo Said Abdulrahman.
“Watu hao walitorokea huko na
tunaendelea kuwahoji…tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa
uliotuwezesha kufanikisha ukamataji huo,tunavishukuru vikundi vya ulinzi
shirikishi vilivyo katika Shehia mbalimbali kwa kuimarisha ulinzi wa
maeneo yao katika kipindi chote cha fujo na vurugu hizo” Alisema
Kamishna Mussa.
Kamishna Mussa aliwaambia
waandishi wa habari kuwa Polisi hivi sasa inaendelea kuwahoji Sheikh
Farid Hadi na viongozi wenzake wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya
Kiislam ili kufahamu wapi alipokuwa na kuthibitisha kama kweli alitekwa
ama la.
Katika hatua nyengine Polisi
imeonya kuchukua hatua kali dhidi ya wafuasi wa UAMSHO wanaodaiwa
kutaka kuvamia kambi za Polisi,kambi za Majeshi na Ofisi za Serikali ya
Mapinduzi.
“Natoa onyo kali kwa wananchi
wote kuwa hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria,Jeshi la Polisi na
Vikosi vyote vya ulinzi na usalama tumejipanga madhubuti kukabiliana na
mtu yoyote ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu” Alisema Kamishna
Mussa.
Akizungumzia hali ya amani,
Kamishna Polisi alisema kwamba Mji wa Zanzibar ni shwari kwa sasa na
wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
No comments:
Post a Comment