Monday, October 15, 2012

MWANDISHI WA HABARI VICKY MACHA AFARIKI DUNIA



Na Hakimu Mwafongo, Iringa  
MWANDISHI wa habari wa gazeti la Nipashe mkoani Iringa, Vicky Macha amekufa leo (jana) asubuhi katika hospitali ya mkoa wa Iringa alikokuwa amelazwa kwa siku tatu. 
 
Macha ambaye alikuwa Mtunza Hazina wa Chama cha Waandishi wa Habari Iringa (IPC) amekufa kutokana na ugonjwa malaria uliokuwa ukimsumbua. 
 
Kwa mujibu wa mumewe Celective Shirima, marehemu alifikishwa hospitali ya mkoa wa Iringa Jumanne Oktoba 9 mwaka huu na kuwa wakati anafika hospitali hali ilikuwa mbaya zaidi kuanzia usiku wa kumkia leo (Jana). 
 
Alisema mkewe alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria na kisukari hali iliyopelekea waganga wa hospitali hiyo kuanza kutibu kisukari ndipo warudi kutibu malaria. 
 
 Alisema wakati waganga wakihangaika na matibabu mkewe alifariki na kwamba mwili wa marehemu unasafirishwa na utazikwa nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro. 
 
Katibu Mtendaji wa IPC, Frank Leonard alisema kifo cha Macha ni pengo kubwa kwa wanahabari na Taifa kwa ujumla na kuwa msiba wa Macha umetokea ikiwa zimepita takribani siku 40 tangu Mwenyekiti wa IPC, Daudi Mwangosi kufa mapema Septemba mwaka huu. 
 
Kabla ya kufanya kazi na Nipashe aliwahi kufanya kazi Kampuni ya Busines Time mkoa wa Kilimanjaro na kuhamishiwa Mufindi kabla ya kuhamishiwa tena Iringa ambako aliachana nao na kujiunga na The Guardian.

No comments:

Post a Comment