Na
George Ramadhan,Mwanza.
MAJONZI,
simanzi na kauli za kulipa kisasi ni miongoni mwa masuala yaliyogubika shughuli
ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Liberatus Barlow
aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita eneo la
Kitangiri Jijini hapa.
Mwili
wa Barlow uliagwa jana na wakazi wa Jiji la Mwanza na mikoa ya jirani katika
shughuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana kabla ya jioni kusafirishwa
kwa ndege kuelekea Jijini Dar es salaam ambapo unatarajiwa kusafirishwa kesho
kwenda kijijini kwake huko Vunjo mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Akizungumza
mbele ya umati mkubwa wa wakazi wa Jiji la Mwanza waliojawa na majonzi, Mkuu wa
mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo alisema kifo cha Barlow sio mwisho wa serikali
kupambana na uhalifu na wahalifu.
Alisema
hivi sasa vyombo vyote vya dola vipo kazini vikifanya uchunguzi wa tukio hilo la mauaji na
kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni haraka iwezekanavyo.
“Leo
Kamanda na Jemedari wetu katika mapambano dhidi ya uhalifu ameondoka, lakini
nataka niwahakikishie kwamba tupo vitani, hatupaswi kuweka silaha chini, kama mkoa tuweke silaha zetu vizuri hadi ushindi
utakapopatikana”alisema
Aliongeza
kusema kwamba jamii ya Mwanza na Tanzania kwa ujumla iwe na imani
kuwa waliohusika na mauaji ya RPC Barlow hawako salama, kwani lazima
watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Naomba
niwahakikishie kwamba vyombo vyote vya dola viko kazini, waliotenda mauaji haya
hawako salama, watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na jambo
hili litafikia tamati mapema iwezekanavyo”alisisitiza Ndikilo.
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba aliwaambia waombolezaji
kwamba taarifa ambazo Jeshi la Polisi limezipata kutoka kwa wananchi zimeongeza
kasi ya upelelezi wa mauaji hayo.
Aliwataka
askari kuwa watulivu katika kipindi hiki cha majonzi lakini akawataka kulipa
kisasi dhidi ya mauaji ya RPC Barlow kwa kuhakikisha wanawakamata wote
waliohusika.
“Umma
utambue kwamba hatutalala hadi tuwatie mbaroni wauaji, na hii inapaswa kuwa
ndiyo kawaida yetu kuhakikisha uhalifu wa aina yoyote unashughulikiwa kwa uzito
ule ule kama tunavyofanya hivi sasa katika
mauaji ya RPC Barlow”alisema Manumba.
Akitoa
salaam za rambirambi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma alisema
kwamba iwapo kuna wananchi wenye taarifa za watu waliohusika na mauaji hayo
wampelekee yeye na atazifanyia kazi.
“Ningependa
kuwaambi wananchi wenye taarifa za muaji ya RPC Barlow kama wanaona shida
kuzipeleka kwingine waniletee mimi tutazifanyia kazi”alisema Mwakyoma ambaye
alimfananisha Barlow sawa na kitabu cha marejeo (encyclopedia) kutokana na
jinsi alivyokuwa akimsaidia kutatua masuala mbalimbali.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Phillip Kalangi alisema kwamba idadi
ya wahalifu ni ndogo sana
ikilinganishwa na idadi ya raia wema hivyo ana imani wakiunganisha nguvu
ushindi utapatikana.
Naye
Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Salum Msangi alisema kwamba Jeshi la Polisi
halitakata tamaa kupambana na wahalifu licha ya Kamanda Barlow kuuawa.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Geita Lenard Paul na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Anthony
Ruta, katika salaam zao za rambirambi walisema kwamba Jeshi la Polisi
limepoteza Kamanda shupavu, mkweli, mweledi na mwalimu kwa makamanda wengine.
Mwenyekiti
wa CCM mkoa wa Mwanza Clement Mabina alisema kwamba Kamanda Barlow alizingatia sana sheria katika utendaji wake wa kazi na alikuwa tayari
kuitika wito hata kama ni usiku wa manane.
Katibu
Mwenezi wa Chadema wilaya ya Ilemela Carlos Majura alisema kifo cha Barlow ni
pigo kwa wapenda amani wote, hivyo wananchi watumie nguvu ya umma kuhakikisha
wanaimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Wakati
hali ikiwa hivyo katika kuuaga mwili wa Kamanda Barlow, baadhi ya walimu wa
shule ya msingi Nyamagana wameelezea kusikitishwa kwao na jinsi tukio hilo la mauaji ya RPC
lilivyotokea mbele ya mwalimu mwenzao Doris Moses.
Mwalimu
Doris ndiye aliyekuwa na RPC Barlow ndani ya gari wakati watu wanaosadikiwa
kuwa majambazi walipowavamia na kumuua kwa kumpiga risasi Kamanda huyo wa
polisi.
Katika
mahojiano na Nipashe, Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Mary Ngalula alisema
kwamba kimsingi wanamuonea huruma mwalimu mwenzao kutokana na kushuhudia tukio hilo la kuogofya.
Alisema
kwamba wanamsikitikia kwa sababu jamii imeanza kumfikiria vibaya kwa kudhani
anahusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.
“Tunamuonea
huruma mwalimu mwenzetu kutokana na maneno tunayoyasikia, lakini sisi tuko
pamoja naye kwa sababu tunamfahamu ni mtu safi,
na hivi tunajiandaa kwenda kumuona na kumtia moyo ili amudu kuilea familia yake
kwani ni mjane”alisema.
Mwalimu
Baraka Magafu yeye alisema kwamba tofauti na hisia za baadhi ya watu kuhusu
uhusiano wa Mwalimu Doris na Kamanda Barlow,
wao (walimu) wanafahamu kuwa ni watu wa kabila moja wanaotoka kijiji kimoja
huko Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Alibainisha
kuwa Mwalimu Doris amekuwa ni mtu anayejihusisha sana na shughuli mbalimbali za watu wa kabila
lake (wachaga), hivyo hakuna sababu ya kumfikiria vibaya kwa sababu tu mtu
aliyekuwa amemsindikiza nyumbani wakitokea kwenye kikao cha maandalizi ya
harusi aliuawa kwa kupigwa risasi.
“Ukifuatilia
mwenendo wa tukio lote, utaona kwamba kilichotokea ni bahati mbaya na kingeweza
kumtokea yeyote, kwani Barlow alikuwa akimsindikiza Mwalimu Doris
nyumbani kwake, na hata baada ya tukio, alipowapigia simu wenzao waliokuwa nao
kwenye kikao walikuwa ndo na wao wanafika majumbani mwao”alisema.
Aliongeza
kwamba katika mazingira kama hayo ni makosa
kuwa na mtazamo hasi dhidi ya Mwalimu Doris kama ambavyo baadhi ya watu
wameanza kuvumisha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Wakati
huo huo habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza kitengo cha
upelelezi zimeeleza kwamba simu ya upepo (radio call) ndiyo iliyomponza Kamanda
Barlow na kumsababishia kifo.
Mmoja
wa maofisa upelelezi ambaye hata hivyo hakupenda jina lake litajwe
alisema kwamba baada ya Kamanda Barlow kuwa amemfikisha Mwalimu Doris nyumbani
kwake, walitokea watu wawili waliokuwa na tochi ambao walimtaka azime taa za
gari lakini yeye (Barlow) akagoma.
Alibainisha
kuwa upelelezi zaidi unaonyesha kwamba walipomsogelea walimlazimisha azime taa
za gari lakini aliendelea kushikilia msimamo wake huku akiwaambia kuwa yeye ni
RPC.
Aliendelea
kusema kwamba ghafla walitokea watu wengine takribani watatu ambao inaonekana
bado hawakuamini kama kweli huyo ni RPC,lakini
alipotoa radio call ili kufanya mawasiliano ndipo walipomfyatulia risasi na
kumuua.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment