Na Mohammed
Mhina, wa Jeshi la Polisi- Zanzibar
Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa Zanzibar Bw. Vuai Mussa Suleiman,
ameelezea utaratibu na ratiba ya usajili na utambuzi wa watu watakaopatiwa
vitambulisho vya Taifa kwa upande wa Zanzibar.
Bw. Vuai ambaye alikuwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakiwemo wa
Mtandao wa kutoa elimu juu ya Vitambulisho hivyo, amesema kuwa kazi hiyo
itafanywa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa kila mwenye sifa ya kupatiwa
kitambulisho cha taifa anasajiliwa.
Amesema kuwa usajili huo utaanza rasmi Oktoka 15, 2012 Visiwani humo na
ameitaja wilaya itakayoanza kuwa ni wilaya ya Kusini Unguja kuanzia siku hiyo
hadi tarehe 26,10,2012.
Amesema wilaya ya kati zoezi litafanyika kuanzia tarehe 29.10.2012 hadi
tarehe 9.11.2012 ikifuatiwa na wilaya ya Magharibi kuanzia tarehe 12.11.2012
hadi tarehe 23.11.2012.
Amesema wilaya ya mjini kazi ya usajili itaanza tarehe 26.11.2012 hadi
tarehe 7.12.2012. Wilaya ya Kaskazini B. kazi hiyo itaanza tarehe 10.12.2012
hadi tarehe 21.12.2012 na Wilaya ya Kaskazini A. itafanyika Tarehe 24.12.2012
hadi tarehe 4.1.2013.
Bw. Vuai amesema kwa upande wa Pemba zoezi hilo litaendelea kwa kuanzia
wilaya ya Mkoani tarehe 7.1.2013 hadi 18.1.2013. Wilaya ya Micheweni
litafanyika kuanzia tarehe 21.1.2013 hadi tarehe 1.2.2013.
Amesema kuwa wilaya ya Wete zoezi hilo litaanza tarehe 4.2.2013 hadi
tarehe 15.2.2013 na wilaya ya mwisho kwa upande wa Pemba itakuwa ni wilaya ya
Chakechake ambayo itaanza zoezi hilo tarehe 18.2.2013 hadi tarehe 1.3.2013.
Bw. Vuai amewataka wananchi kujitokeza kuhakikisha kuwa wanasajiliwa kwa
manufaa yao na ya taifa kwa ujumla.
Amewakumbusha wananchi kuwa na vielelezo mbalimbali vikiwemo vyeti vya
kuzaliwa, vyeti vya elimu ya msingi na Sekondari, vitambulisho vya bima ya afya
ama mfuko wowote wa hifadhi za jamii ama leseni ya udereva, hati ya kusafiria,
cheti cha mlipakodi kutoka TRA, ZRB.
Bw. Vuai amesema kuwa zoezi hilo halifungamani na itikadi zozote za
kivyama, kidini na kwamba maafisa wake watawasajili wale wote watakao kuwa na
vielelezo vyote ama kimojawapo kati ya hivyo.
Hata hivyo amesema kuwa usemi wa kuwepo vielelezo hauna maana kuwa mtu
atakayekosa kielelezo hataandikishwa bali ataweza kuthibitishwa na Masheha ama
viongozi wengine wa serikali za mitaa ama serikali za Vijiji na Vitongoji.
No comments:
Post a Comment