TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watu sita wamekamatwa kwa tuhuma za kumuua Ofisa wa Polisi marehemu Said
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali
Mussa aliwaambia waandishi wa habari kwamba watuhumiwa hao (majina
yanahifadhiwa) walikamatwa sehemu tofauti, mmoja amekamatwa Kisiwa
kidogo cha Tumbatu, wa pili maeneo ya Mjini Unguja, mtuhumiwa wa tatu
alikamatwa ofisi za Idara ya Uhamiaji alikokwenda kushughulikia hati ya
kusafiria ili aweze kutoroka hapa nchini.
Kamishna Mussa alisema watuhumiwa
wengine watatu wamekamatwa mkoani Tanga ambako walikimbilia kujificha
baada ya kufanya mauaji ya Ofisa Polisi Koplo Said Abdulrahman.
“Watu hao walitorokea huko na
tunaendelea kuwahoji… tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa
uliotuwezesha kufanikisha ukamataji huo,tunavishukuru vikundi vya ulinzi
shirikishi vilivyo katika Shehia mbalimbali kwa kuimarisha ulinzi wa
maeneo yao katika kipindi chote cha fujo na vurugu hizo,” alisema
Kamishna Mussa.
Kamishna Mussa aliwaambia waandishi wa
habari kuwa Polisi hivi sasa inaendelea kuwahoji Sheikh Farid Hadi na
viongozi wenzake wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam ili
kufahamu wapi alipokuwa na kuthibitisha kama kweli alitekwa ama la.
Katika hatua nyengine Polisi imeonya
kuchukua hatua kali dhidi ya wafuasi wa UAMSHO wanaodaiwa kutaka
kuvamia kambi za Polisi, kambi za Majeshi na Ofisi za Serikali ya
Mapinduzi.
“Natoa onyo kali kwa wananchi wote kuwa
hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria, Jeshi la Polisi na Vikosi vyote
vya ulinzi na usalama tumejipanga madhubuti kukabiliana na mtu yoyote
ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu” alisema Kamishna Mussa.
Akizungumzia hali ya amani, Kamishna
Polisi alisema kwamba Mji wa Zanzibar ni shwari kwa sasa na wananchi
wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na
usalama vimeimarisha ulinzi, tunaomba wananchi wasiwe na hofu na
waendelee kutii sheria za nchi bila kushurutishwa, waendelee kudumisha
amani katika maeneo yao na pia waendelee kutupatia taarifa za mara kwa
mara za hali ilivyo huko wanakoishi.”
Imetolewa na:
Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzibar
21/10/2012
No comments:
Post a Comment