MTOTO wa Baba
wa Taifa, Makongoro Nyerere, ameangushwa katika kinyang’anyiro cha kutetea
nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, ambayo
sasa imechukuliwa na Christopher Sanya. Makongoro ambaye amekuwa mwenyekiti wa mkoa huo kwa miaka mitano, alishindwa katika uchaguzi huo uliofanyika juzi chini ya usimamizi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa kutoka Mkoa wa Kagera, Nasir Karamagi. Akitangaza matokeo ya awali, Karamagi alisema kuwa kati ya kura 1,012 zilizopigwa, Sanya alipata 469 na Makongoro alijikusanyia 402 huku Enock Chambili akiambulia 144. Lakini kwa mujibu wa Katiba ya CCM mshindi hakuwa amevuka nusu ya kura, na hivyo ilibidi Sanya na Makongoro, kuingia katika duru ya pili ambapo mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake alipitwa kwa kura 59. Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, Makongoro alimuasa Sanya kufanya kazi kwa mujibu wa katiba ya chama na kuvunja makundi yaliyoshamiri ndani ya CCM huku akiahidi kutoa ushirikiano wake. “Naomba uwe muadilifu, mkoa huu wa Mara ni mgumu sana kuufanyia kazi, kwani kazi ya uenyekiti si lelemama, hii ndiyo nafasi kubwa ambayo itatusaidia katika uchaguzi wa 2014/2015,” alisema. Makongoro aliwataka pia wajumbe kuachana na mambo ya kambi, akisema uchaguzi umekwisha kilichopo ni kushikamana na kuwapa ushirikiano viongozi wapya wakiongoze chama vizuri. Katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM mkoa - kila wilaya nafasi mbili, waliopenya ni Josephat Seronga na Ester Nyarobi (Serengeti), Zuhura Makongoro na Jackson Waryoba (Bunda), Josehat Kisusi na Felister Nyambaya (Rorya). Wengine ni Grace Bunyinyiga na Thabita Idd (Butiama), Abdalah Jumapili na Kananda Kananda (Musoma Mjini) na Mariam Mkono na Samson Gesase (Tarime). Kamani ang’ara Simiyu Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani, amepata ushindi wa kishindo katika kinyanganyiro cha uenyekiti Mkoa mpya wa Simiyu baada ya kujizolea kura 415. Waliobwagwa ni aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, George Nangale na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Meatu, Enock Yacob. Msimamizi wa uchaguzi huo, Jackson Msome, alisema kuwa kati ya kura 714 zilizopigwa, mbali na Dk. Kamani, Nangale alipata 234 huku Enock akiambulia 91. Wakasuvi arejea Tabora Mwenyekiti CCM Mkoa wa Tabora aliyemaliza muda wake, Hassan Wakasuvi, amefanikiwa kutetea kiti hicho kwa ushindi wa kishindo. Wakasuvi aliwamwaga wenzake watatu ambao ni Zuberi Mwamba, Juma Nkumba na Haji Bagio ambao walijitoa muda mfupi kabla ya uchaguzi kuanza. Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Mwigulu Mchemba, alisema kati ya kura 996 zilizopigwa, Wakasuvi alipata 921, akifuatiwa na Zuberi Mwamba kura 75 na 16 ziliharibika. Katika nasaha zake, Wakasuvi aliwataka wajumbe wavunje makundi na wamsaidie kukijenga chama, huku akiahidi kushirikiana na kila mmoja bila kujali makovu ya uchaguzi. Alionya kuwa wapo watu ambao wanadhani kwamba bila wao CCM Tabora haipo, akisema atawachukulia hatua maana ndani ya chama wamekuwa wakiketi vikao vya kukibomoa. Msukuma apeta Geita Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Joseph Msukuma, aliyeng’olewa madarakani na Baraza la Madiwani kwa tuhuma za ufisadi, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM Mkoa mpya wa Geita. Katika uchaguzi huo, Msukuma alipata kura 565 kati ya 698 zilizopigwa na wajumbe wa wilaya tano za Nyang'hwale, Geita, Chato, Mbogwe na Bukombe zinazounda mkoa huo. Msukuma aliwabwaga Jeremiah Ikangala, aliyepata kura 130 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo aliyemaliza muda wake, John Luhemeja aliyeambulia kura tano. Mlao arudi Pwani Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, aliyemaliza muda wake, Mwinshehe Mlao, amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kuibuka na ushindi wa kura 528 dhidi ya Kapteni Mpembenue Seif Ally aliyepata kura 196 na Mziwanda Yahaya aliyeambulia 13. Washindi wa ujumbe wa NEC kutoka wilayani ni Halfan Mavala, Asia Madima (Kibaha Vijijini), Fatma Ngozi, Mwajuma Denge (Bagamoyo), Hafsa Kilingo, Imani Madega (Kibaha Mjini) na Bakari Mbonde, Hawa Mtopa (Rufiji). Kingunge anena Kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema kuwa vitendo vya rushwa ndani ya chama hicho, vimeshamiri kutokana na ubinafsi wa baadhi ya wanachama kuweka mbele maslahi binafsi. Mzee Kingunge, alitoa kauli hiyo juzi mkoani Pwani, wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa mkoa wa chama hicho, akisema kuwa ubinafsi huo umefanya vyama kuwa mali ya mtu na ushindani unakuwa si wa kindugu bali uhasama. Alisema wakati wa Afro- Shiraz na TANU, nchi iliwekwa mbele tofauti na sasa ambapo ubinafsi ndio unawekwa mbele na nchi inabaki peke yake. “Kwa kuwa suala ni ubinafsi ndiyo maana sasa watu wanafikia hatua ya kununua vyeo kutoka kwa wapiga kura, jambo linalomdhalilisha mtoaji na mpokeaji wa rushwa,”alisema. JK ashauriwa Mmoja wa wagombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya CCM kupitia Wilaya ya Bunda, Cyprian Musiba, amemshauri Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete, kuwafutia matokeo baadhi ya wagombea waliopita kwa rushwa. Musiba ambaye ni mwanahabari kitaaluma na Mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano ya I&RH, alitaja nafasi ambazo Rais Kikwete anapaswa kutengua matokeo yake kuwa ni ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara na Morogoro. Pia Musiba alitaja washindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC katika wilaya za Monduli, Bunda na Musoma Mjini pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Musiba alifafanua kuwa wenye fedha wameifanya CCM kuwa sehemu ya kufichia madhambi yao, hivyo hawaoni hatari kutumia gharama yoyote kupata uongozi. “Penye rushwa hakuna haki, hakuna kuwatumikia wananchi, mimi ni miongoni mwa wagombea nilioshuhudia hali hii, watu kutoa fedha kwa ajili ya kununua uongozi ni jambo la kawaida kwa CCM. Mkoani mara zimetumika zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya kumwangusha Makongoro,” alisema Musiba. Kada huyo ambaye wiki iliyopita aliwasilisha malalamiko yake ndani ya chama kupinga uchaguzi aliyoshiriki wilayani Bunda, alishauri kuwa rufaa hizo hazipaswi kusikilizwa na kamati za siasa na maadili za wilaya kwa vile wajumbe wake ndio watuhumiwa. Alisisitiza kuwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara, fedha zilikuwa zikigawiwa wazi wazi kwa wajumbe na baadhi ya vigogo na wafanyabiashara wakubwa kuhakikisha watu wao wanashinda. “Viongozi wanaotumia fedha ndani ya CCM hawawezi kuwa watetezi wa wanyonge. Na kwa rushwa hii hata uchaguzi wa Bunda kanuni zilikiukwa kwa kuruhusu mfanyakazi wa serikali kugombea,” alisema. Musiba alisema kuwa anaungana na kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ya kutaka wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya CCM wawajibishwe kwa kutoswa. Alisema ni fursa nzuri kwa NEC mpya aliyosema ina sura nyingi ngeni kutomuonea mtu aibu kwa lengo la kukinusuru chama kutokana na kutekwa na mafisadi hali aliyosema inazidi |
Monday, October 15, 2012
MAKONGORO NYERERE APINGWA MWEREKA MARA CCM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment