Monday, October 15, 2012

HASSAN WAKASUVI ACHAGULIWA TENA KUWA MWENYEKITI CCM TABORA


 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Bw.Hassan Wakasuvi akitoa neno la shukrani mbele ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi mkuu wa mkoani Tabora Bw.Samweli Sitta uliofanyika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
 Baadhi ya wajumbe wakishangilia baada ya matokeo kutangazwa
 Bw.Samwel Sitta akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Tabora .
 Ismail Rage na Prof.Juma Kapuya wakimsikiliza mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora wakati akitoa hotuba yake mara baada ya kutangazwa mshindi.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora Bw.Hassan Wakasuvi akihutubia mkutano wa uchaguzi mkuu mkoani Tabora.
Bw.Hassan Wakasuvi Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora.

Na Hastin Liumba,Tabora

CHAMA cha mapinduzi,(CCM),mkoa wa Tabora jana kimekamilisha uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa mkoa huo,huku mwenyekiti wa zamani Hassan Wakasuvi,akifanikiwa kutetea nafasi yake kwa kishindo.


Katika uchaguzi huo wagombewa walikuwa wanne ambao ni Hassan Wakasuvi ambaye alikuwa akitetea kiti chake na Zuberi Mwamba, wengine ni Juma Nkumba na Haji Bagio ambao walijitoa muda mfupi kabla ya zoezi la kupiga kura halijaanza.


Wakati wajumbe wakiendelea kujiandaa na uchaguzi huo,mbunge wa jimbo la Sikonge,Said Nkumba,alipanda jukwaani na kutoa taarifa kuwa,mgombea Juma Nkumba ambaye ni baba yake mzazi amemuagiza awaombe radhi wajumbe kuwa ametafakari na kuona ajitoe kwenye kinyang`anyiro hicho.

Aidha Juma Nkumba ambaye alishawahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora,alisema kuwa licha ya kujitoa ameamua kubaki kuwa mwanachama mtiifu na ataendelea kuwa mshauri ndani ya CCM hivyo anapisha vijana wakipiganie chama mbele ya wapinzani.

Aidha mgombea mwingine Haji Bagio, naye alitangaza kuwa ameamua kujitoa bila ya shinikizo la mtu hivyo asifikiriwe vibaya kwa kile alichodai kuwa ni  uamuzi wake wa  burasa.

Akitangaza matokeo hayo majira ya saa mbili za usiku,msimamizi wa uchaguzi huo Mwigulu Mchemba,alisema katika uchaguzi huo kura zilizopigwa ni 996  ambapo Hassan Wakasuvi alipata kura 921 na mshindani wake Zuberi Mwamba alipata kura 75 na kura zilizoharibika ni 16.

Katika nasaha zake mwenyekiti aliyeshinda nafasi hiyo Hassan Wakasuvi aliwataka wajumbe wavunje makundi na wamsaidie kukijenga chama na atashirikiana na kila mmoja bila kujali makovu ya uchaguzi.

Alisema chama kamwe hakiwezi kujengwa kwa makundi na majungu na atachukua hatua kwa mwanachama yoyote mwenye kutaka chama kisitawalike.

“Nitashirikiana na wote na nitaunda baraza la ushauri la wazee na mzee Juma Nkumba atakuwa mwenyekiti wake ili uongozi wake ukipotoka washauriwe kwa maslahi ya chama.” Alisema Wakasuvi.

Aidha Wakasuvi aliwataka wabunge wa mkoa wa Tabora wamsaidie kuongoza na kujenga chama imara na kamwe wenye majungu safari hii wasipewe nafasi maana wamezidi.

“Nawaomba wanachama na viongozi wenzangu,wabunga…..hata Munde na Bashe, ambao hawakuhudhuria mkutano huo wamsaidie kuimarisha chama kwani majungu hayana nafasi kwa karne hii.” Aliosema.

Alisema wapo watu ambao wanaona eti bila ya wao CCM Tabora haipo na aliwaonya kuwachukulia hatua maana wao ndani ya chama wamekuwa wakiketi vikao vya kukibomoa chama cha mapinduzi.

“Naomba niwapshe kuwa wasifikiri wao ndani ya chama bila ya wao CCM haiendi….wanajidanganya kwani wanaweza wakawepo lakini wakawa kama sanamu tu isiyo na msaada.

Wakasuvi aliwashukuru wajumbe kwa kumpigia kura za kishindo na kuongeza hadhani kama kuna mwenyekiti mwingine nchini ambaye anaweza kupata ushindi kama aliopata.

No comments:

Post a Comment