Mwili wa aliyekuwa kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mwanza Marehemu Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)
Liberatus Barlow (52) ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi
kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, utaagwa
Jumanne saa tano asubuhi katika kanisa la Katoliki lililoko Ukonga,
jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa
na Kamati ya maandalizi ya mazishi na kuthibitishwa na Msemaji wa Jeshi
la Polisi Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Advera Senso, Mwili Marehemu
utawasili siku ya Jumatatu jioni ukitokea mwanza.
Siku ya Jumanne mwili wa marehemu
utafikishwa nyumbani kwake Ukonga kabla ya kupelekwa katika kanisa la
Katoliki Ukonga kwa shughuli za ibada na kutoa heshima za mwisho.
Aliendelea kusema kuwa viongozi
mbalimbali wa Serikali, Maofisa wa waandamizi wa Polisi, Askari na
wananchi watatoa heshima zao za mwisho katika kanisa la hilo.
Aliongeza kuwa baada ya ibada na
shughuli ya kuaga kukamilika, mwili wa marehemu utasafilishwa kuelekea
nyumbani kwao kilema, Moshi vijijini Mkoani Kilimanjaro kwa mazishi
yatakayofanyika siku ya Jumatano mchana kwa taratibu zote za kidini na
baadae kuhitimishwa kwa kufuata taratibu za kijeshi.
Marehemu kamanda Barlow alizaliwa
katika kijiji cha Kyou Wilaya ya Moshi vijijini, Mkoani Kilimanjaro
mwaka 1960, baada ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 1974 katika shule ya
msingi Lombetha, alijiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Maua
Seminary na baadae kujiunga kidato cha tano na sita katika shule ya
Sekondary Milambo na kuhitimu mwaka 1981.
Baaada ya kumaliza elimu ya
sekondari, marehemu kamanda Barlow alilitumikia taifa katika Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) Operesheni Imarisha katika kikosi cha Mafinga JKT,
Mkoani Iringa.
Mwaka 1982, Marehemu alijiunga na
Chuo cha mafunzo cha Polisi Moshi (CCP) kwa ajili ya kusomea mafunzo ya
awali ya sheria ya Uhamiaji na baadae kupangiwa kufanya kazi mpakani
mkoani Mtwara akiwa kama Mkuu wa kituo cha Uhamiaji.
Marehemu kamanda Barlow
aliajiriwa na Jeshi la Polisi baada ya kumaliza shahada ya kwanza ya
utawala kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa kuomba kazi katika
Idara ya Polisi mwaka 1987 katika ngazi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi.
Kutokana na uadilifu wake katika
kazi, Marehemu aliweza kuaminiwa na viongozi wake na kupandishwa vyeo
mbalimbali mpaka kufikia ngazi ya Cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi,
cheo ambacho kilimuwezesha kupewa madaraka ya kuwa Kamanda wa Polisi
Mikoa mbalimbali ikiwemo Tabora na Mwanza.
Kabla ya kufikia ngazi
aliyokuwanayo, marehemu aliwahi kuaminiwa na kushika nyazifa mbalimbali
akiwa kama Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID), Mkuu wa Polisi Wilaya
(OCD) na Mkuu Upelelezi Mkoa (RCO) na hatimaye kupata wadhifa wa kuwa
Kamanda wa Polisi Mkoa.
Marehemu Kamanda Barlow hadi umauti unamkuta
alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na atakumbukwa kwa
juhudi zake za kupambana na kudhibiti uharifu.
No comments:
Post a Comment