Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa kutoka Umoja wa Mataifa
unaoshughulikia Matumzi endelevu ya Nishati kwa wote, wakati ujumbe huo
ulipofika Ofisini kwa Makamu wa rais, Ikulu jijini Dar es Salaam,
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Ujumbe kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja
wa Ulaya Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya nao mazungumzo ambayo mengi
yalijikita katika suala la Nishati Endelevu katika Tanzania.
Ujumbe huo uliwajumuisha; Bw. Christopher Jones
(Mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Umoja wa Ulaya), Bw. Faouzi Bensarsa
(Mshauri wa Nishati Umoja wa Ulaya), Bw. Luis Gomez Echeverri (Mshauri Mkuu wa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Masuala ya Matumizi Endelevu ya Nishati kwa
wote) na Bw Alberic Kacou (Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania).
Katika mazungumzo hayo; Bw. Jones alimueleza Mheshimiwa Makamu wa
Rais namna Umoja wa Ulaya ulivyo na nia thabiti ya kushirikiana na Tanzania
katika kupanga mipango madhubuti itakayowezesha sekta ya nishati nchini kukua
na hivyo taifa kuondokana na utegemezi wa nishati hasa ya umeme uliopo sasa.
Pia alifafanua kuwa, Umoja huo umeshafanya mazungumzo na Wizara ya Nishati na
Madini ya Tanzania na hivyo ni matarajio yake kuwa kupitia ushirikiano baina ya
Tanzania na Umoja wa Ulaya, sekta ya Nishati itapata ahueni katika siku zijazo
na hivyo kuongeza uwezo pamoja na idadi ya watumiaji wa nishati hasa ya umeme
kwa Tanzania.
Kwa upande wake Bw. Bensarsa yeye alimueleza Mheshimiwa Makamu wa
Rais kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuweka agenda ya nishati
kuwa moja ya agenda zake kubwa na akafafanua kuwa kupitia mpango wa ‘Nishati
Endelevu kwa Wote’, Tanzania itaweza kunufaika na fursa zinazotokana na mpango
huo na hasa sasa ambapo bado kuna tatizo la nishati japokuwa katika miaka
michache ijayo Tanzania inategemewa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati
ambayo itatumika hapa na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa alieleza pia kuwa, Tanzania
inakabiliwa na changamoto mbalimbali na moja kubwa ni juu ya kuhakikisha kuwa
uzalishaji wa nishati unafanyika kwa kiwango cha juu hali inayoweza kutoa fursa
za kukuza uchumi zaidi, pamoja na kuhakikisha inashirikisha wadau mbalimbali wa
sekta ya nishati katika kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Akizungumza na wageni wake, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal
alifafanua kuwa Tanzania imejipanga vema licha ya kwamba inahitaji ushirikiano
kutoka kwa mataifa wahisani, makampuni na watu binafsi ili kuwekeza katika
uzalishaji wa nishati. Pia akafafanua kuwa, nchi yetu inavyo vyanzo vingi
lakini tatizo kubwa lipo katika upatikanaji mtaji wa kuvitumia vyanzo hivyo
hasa kile cha Geo-Thermal. Tena Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwahakikishia
wageni wake kuwa, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa sekta ya nishati
inatanuka na kuondokana na utendaji usioridhisha na kwamba anatarajia kuwepo
mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kimfumo katika shirika la umeme nchini
TANESCO , ili lifanye kazi kwa ufanisi na kuongeza tija kwa watumiaji nishati
ya umeme hapa nchini.
Imetolewa na: Ofisi ya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
No comments:
Post a Comment