Friday, October 5, 2012

"NITAONDOA MAKUNDI NDANI YA CCM UYUI"-MUSSA NTIMIZI



Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Uyui mkoani Tabora,Bw.Mussa Ntimizi amesema kazi kubwa iliyoko mbele yake baada ya uchaguzi ni kuhakikisha anavunja makundi miongoni mwa wanachama ambayo amedai kuwa bado ni tatizo na yatachangia kwa kiasi kikubwa  kukizorotesha  Chama hicho.

Mussa Ntimizi ambaye alikuwa akiongea na mtandao huu ofisini kwake mjini Tabora,amesema amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwepo kwa mgawanyiko miongoni mwa wanachama akiwemo Mbunge wa jimbo la Tabora Kaskazini Mh.Shaffin Suma ambaye katika kipindi chote cha kampeni hadi uchaguzi alikuwa akimsaidia Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Bw. Abdallah Kazwika ambapo katika uchaguzi huo alishindwa na Bw.Mussa Ntimizi.

''Ninahitaji kuvunja makambi na kama tukiweza hili mengine yote yatakuwa rahisi ndani ya Chama chetu"alisema Mussa huku akiweza wazi kuhusu makundi hayo yanavyoendelea kujionesha wazi wakati wa hatua za mwanzoni tu za uongozi wake jambo ambalo amedai kutoliachia liendelee ndani ya CCM.

Katika kudhihirisha kuwepo kwa athari za makambi hayo yeye kama Mwenyekiti amejaribu mara kadhaa kumpigia simu Mbunge wa Tabora Kaskazini Mh.Suma kumuita katika kikao cha chama ambaye hakutaka kupokea simu hiyo....''Nilimpigia Mh.Suma kumwita kwenye kikao,mara ya kwanza alipokea na nilipojitambulisha kwake kwakuwa namba ya simu yangu alikuwa hana alipokea na kuikata,niliendelea kumpigia hakupokea kabisa na hatimaye akazima simu,jambo ambalo lilinifanya nitambue kuwa bado tatizo lipo kwakuwa nilipiga tena simu kwa siku iliyofuata hali ilikuwa ni ile ile kwa kiongozi huyo aliyepewa dhamana kubwa na wananchi ya kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"

Akiendelea kuzungumzia vipaumbele alivyojiwekea mara baada ya kuchaguliwa Ntimizi alisema mbali na kuvunja makambi hayo sasa ni wakati muafaka wa kusimamia kwa dhati Ilani ya CCM.

Na kuhusu suala la Kuwania Ubunge ifikapo mwaka 2015 Bw.Ntimizi alisema bado ni mapema mno kulizungumzia hilo.     

No comments:

Post a Comment