Monday, November 26, 2012

JB MPIANA KUWASILI NCHINI


Na Mwandishi Wetu.

 MWANAMUZIKI nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana akiwa na Bendi yake ya Wenge BCBG anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya maonesho matatu tofauti ikiwa ni pamoja na litalofanyika Ijumaa kwenye Viwanja vya Leaders Club Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya QS J Mhonda, Joseph Mhonda alisema kuwa mwanamuziki huyo atawasili nchini kwa kutumia ndege ya Shirikika la Ndege la Kenya.

Mhonda alisema kuwa katika Onesho hilo ambalo litakuwa sambamba na uzinduzi wa Albamu ya Bendi ya Mashujaa ijulikanayo kama Risasi Kidole.

Alisema kabla ya kufanyika kwa onesho la jijini Dar es Salaam, JB Mpiana na Bendi nzima ya Wenge BCBG wataelekea MKoani Arusha ambako watafanya onesho maalum siku ya Alhamis na Ijumaa kufanya mambo yake katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam na baadaye Mwanza Desemba 2.

Mhonda alisema wakiwa MKoani Arusha watafanya onesho hilo katika Ukumbi wa Tripple A na Mkoani Mwanza watakuwa kwenye Ukumbi wa Villa Park.

Alisema kuwa kila kitu kimekamilika kuhusu ujio wa mwanamuziki huyo, ambaye atakuja na Wanamuziki wake wote 25 ambao yupo nao katika bendi hiyo.

Alisema wameona ni bora aanze mikoani na baadae amalizie hapa na kuondoka zake katika ziara za nchi nyingine. Mhando alisema mwanamuziki huyo atawasiri nchini na wanamuziki wake kutoa burudani ya aina yake.

Wakati JB akiwasili leo na Bendi ya Mashujaa chini ya Charles Gabriel ‘Chaz Baba’, wameingia kambini jana kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi huo.

Akizungumzia kwa upande wao Chaz baba alisema kuwa bendi hiyo ipo hapa hapa jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya mazoezi maalum ya uzinduzi.

Chaz Baba alisema wamejipanga kufanya uzinduzi wa aina yake katika albam yao hiyo ya pili huku kwa upande wake ikiwa ya kwanza.

"Leo (Jana) ndiyo tumeingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi wetu kubwa ni kwamba tumejipanga kufanya kweli katika uzinduzi huo ambao kwa upande wangu ni wa kwanza katika bendi ya Mashujaa"alisema Chalz Baba.

Alisema albamu yao, wanayozindua iitwayo Risasi Kidole ina nyimbo sita, ambazo ni Risasi Kidole yenyewe utunzi wake Chaz Baba, Ungenieleza utunzi wake Raja Ladha, Umeninyima utunzi wa Freddy Masimango, Hukumu ya Mnafiki utunzi wake Jado FFU, Kwa Mkweo utunzi wake Baba Isaya na Penzi la Mvutano, ambao umetungwa na Masoud Namba ya Mwisho.

Chaz Baba alisema kama ilivyopangwa, mbali na JB Mpiana, wanamuziki wengine watakaopamba uzinduzi huo ni MB Dogg, H Baba, Ney wa Mitego na wengineo ambao watajulikana baadaye.

“Sisi kwa upande wetu tumejipanga vizuri kuwapa watu burudani ambayo tunajua kwa muda mrefu wameikosa, Mashujaa tunakuja kushujaa, ushujaa wa kuwaburudisha watu na kukata kabisa kiu yao,”alisema Chaz Baba.

Alisema wanataka kufanya shoo ambayo hata JB mwenyewe akiona atakubali kwamba Tanzania kuna bendi yenye ubora sawa na bendi za kwao, Kongo, ambayo ni Mashujaa.“Hadi sasa wapenzi wa muziki hapa Dar es Salaam ambao wamebahatika kuona shoo zetu wanakiri sisi ndio mabingwa wapya wa muziki wa dansi Tanzania, sasa tunataka tumdhihirishie hilo na JB Mpiana,”alisema Chaz Baba.

No comments:

Post a Comment