Thursday, November 29, 2012

 Na Lucas Raphael.Tabora

Makala.

Januari 16 mwaka huu ni siku ya kukumbukwa katika mkoa wa Tabora, kutokana na mkoa huo kuandika historia mpya katika nyanja ya elimu nchini. Mkoa huo umeweza kupata Chuo kikuu cha Kwanza toka Tanganyika ilipopata uhuru wake mwaka 1961.

Kwa muda mrefu Mkoa wa Tabora haukuwa na vyuo vinavyotoa elimu ya juu hapa nchini hali ambayo iliufanya mkoa huo ushindwe kupata ustawi mkubwa wa kimaendeleo ikilinganishwa na mikoa mingine, ambayo ina vyuo vikuu.

Mkoa huo ulikuwa na vyuo vinavyotoa elimu ya kati tu kama vyuo vya Ualimu ambavyo ni chuo cha Ualimu Ndala, wilayani Nzega na Chuo cha Ualimu cha Tabora ambavyo vilianza kutoa huduma hiyo kwenye miaka ya sitini na sabini.

Ukiondoa vyuo hivyo vyuo vingine vilivyopo ni Chuo cha Utumishi wa Umma, Chuo cha Ardhi na chuo cha kilimo Tumbi na vyuo vya ufundi vya VETA na vituo vidogo vidogo vya utoaji wa elimu mbali mbali ndivyo vilivyokuwa vikifanyakazi ya kuwaelimisha wakazi wa Tabora katika fani Tofauti.

Kabla ya vyuo hivyo Mkoa wa Tabora, ulikuwa ukisifika sana kutokana na kuwa na shule mahiri za sekondari ambazo ziliweza kuchangia maendeleo ya taifa hili kikamilifu na kwa ushindani uliostahili.

Shule hizo ni Pamoja na Tabora Boys, Milambo sekondari, Tabora Girls, Kazima ambazo kwa pamoja zimetoa wataalam wengi zaidi hapa nchini pamoja na viongozi wa serikali.

Hata hivyo kukosekana kwa elimu ya chuo kikuu katika mkoa wa Tabora, kumeufanya mkoa huo uliokuwa ukisifika kielimu hapa nchini upoteze umaarufu wake wa miaka mingi na kujikuta ukiwa miongoni mwa mikoa isiyokuwa tena na sifa ya kufanya vizuri katika nyanja hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.

Chuo hicho kikuu kilizinduliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo za uzinduzi zilizofanyika katika uwanja wa Chipukizi mjini hapa.

Katika hotuba yake waziri Sitta, alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo katika mkoa wa Tabora, ambao alisema umekuwa nyuma kwa muda mrefu na hivyo kuufanya usiwe miongoni mwa mikoa yenye maendeleo makubwa kielimu hapa nchini.

Alisema kuwepo kwa chuo hicho ni maendeleo ya kweli kwa mkoa na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuwa makini na kushiriki katika utoaji wa mazingira mazuri na kuwapa ushirikiano watumishi, wahadhiri na wanafunzi ili kuongeza sifa za mkoa huo katika elimu ya juu nchini.

Aliilaumu bodi ya mikopo Tanzania kutokana na kushindwa kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini huku akibainisha wazi kuwa utendaji katika bodi hiyo umejaa urasimu.

Alisema pamoja na Urasimu, bodi hiyo imekuwa ikifanyakazi zake kwa chuki, upendeleo, dhulma na kufanya mambo mengine ambayo hayakubaliki katika utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.

Alisema kunahaja ya kufanya mabadiliko makubwa katika bodi hiyo ili utendaji wake uwe na tija kwa watanzania wanaotafuta elimu ya juu nchini ili waweze kuja kulitumikia taifa katika nyanja mbali mbali.

Alisema suala hilo atalifikisha serikalini kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi wa kina ambao utasaidia kuboresha utendaji katika bodi ya mikopo nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watoto wa watanzania wananufaika zaidi na mikopo hiyo ya kielimu.

Akizungumza katika Ibada maalum ya ufunguzi wa chuo hicho Askofu mkuu wa kanisa Katoliki Jimbo kuu la Tabora, Mhasham Paul Ruzoka, alisema kuwa elimu ni kitu muhimu kwa maisha ya binadamu na kudokeza kuwa Kanisa katoliki linapenda kutoa huduma hiyo kwa watanzania wote pasipokuwa na ubaguzi wa aina yeyote.

Alisema elimu ni kama Mwanga unaomuwezesha mtu yeyote kuona na kufanya shughuli mbali mbali za kimaendeleo na kijamii hapa nchini, huku akisema kuwa kinyume na elimu ni ujinga ambao unafananishwa na giza nene ambalo linamzuia binadamu kufanya kazi mbali mbali za maendeleo.

Askofu alisema ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha kuwa anapata elimu ili aweze siyo tu kuishi vizuri bali pia kuishi maisha ambayo yatamsaidia kumjua na kumthamini Mungu ambaye ndiye aliyejalia vipawa vya kila namna kwa binadamu.

Alisema kwa kuwa Kanisa katoliki linatambua umuhimu wa jambo hilo litaendelea kutumia fursa zilizopo ili kuweza kuendelea kuwasaidia wananchi waweze kupata fursa hiyo muhimu kwa maendeleo ya umma na kuondoa ubabaishaji katika utoaji wa huduma za kijamii miongoni mwa watanzania.

Askofu mkuu aliwahimiza waumini wa kanisa hilo na wale ambao si waumini kukitumia vizuri chuo hicho kikuu kwa ajili ya manufaa ya kijamii na kudokeza kuwa lengo la kanisa ni kuhakikisha kwamba ustawi wa watu unakuwabora zaidi kadri miaka inavyoongezeka.

Akizungumza mara baada ya ibada hiyo maalum ya kufungua chuo kikuu cha Archbishop Mihayo university College of Tabora ( AMUCTA) ambacho kitakuwa chuo kikuu kishiriki cha mtakatifu Augustine cha Jijini Mwanza (SAUT) Makamo mkuu wa chuo hicho nchini Dk. Charles Kitima, alisema ni muhimu watoto wa Tanzania wakinufaika na elimu ya juu.

Alisema katika siku za karibuni kumeibuka mtindo wa viongozi wa kiserikali kuweka vikwazo kadha wa kadha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma katika vyuo binafsi wasipatiwe mikopo na kwamba wanafunzi watakaopewa mikopo ni wale wanaosoma katika vyuo na taasisi za serikali pekee.

Alisema kauli hiyo ilipingwa vikali na wakuu wa vyuo binafsi kwa sababu si haki kufanya hivyo na kwamba vyuo vya elimu ya juu vya binafsi vimeanzishwa kwa ajili ya kuisaidia serikali iweze kupata wataalam wengi zaidi.

Kulingana na Dk. Kitima, serikali haiwezi kuwasomesha wanafunzi wote waliomaliza elimu ya kidato cha sita na kufaulu mtihani kwahiyo ni vyema ikashirikiana na vyuo vikuu vya binafsi vinavyowapatia vijana elimu hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Alisema ni vyema basi serikali ikajitahidi kuondoa kero hizo ndogo ndogo zinazowakabili wanafunzi hasa katika sekta ya mikopo kwani alisema bodi ya mikopo nchini imekuwa ikionekana kama kikwazo kwa watoto wa wakulima kupata elimu ya juu nchini Tanzania.

Alisema mikopo ni haki yao na kwamba wananchi wanapaswa kujua na kutambua kuwa suala la utoaji wa elimu ya juu nchini ni la lazima na ni haki yao ya kimsingi watoto wao kuipata elimu hiyo muhimu kwa ustawi wa taifa hili.

Alisema jamii ya wasomi itaendelea kupinga sera mbovu ambazo hazina tija kwa taifa letu na kubainisha kuwa jamii hiyo itaendelea kufanya utafiti utakaosaidia kuimarika kwa elimu nchini ikiwa ni njia pekee ya kupambana na tatizo la kuwa na wataalam wasiokuwa na sifa zinazotakiwa.

Mkuu wa chuo kikuu cha Askofu Mkuu Mihayo cha Tabora ( AMUCTA) Dk. Thadeus Mkamwa, alisema kuwa chuo hicho kikuu kimeanza rasmi novemba 3 mwaka jana, kwa kuanza na mafunzo ya shahada ya kwanza ya Ualimu kikiwa na wanachuo 886.

Alisema kutokana na mikakati ya chuo hicho kinatarajia kuanzisha pia shahada za masomo ya sayansi ya jamii, biashara na sheria ambayo yanatarajia kuleta mapinduzi mazito katika suala zima litakalosaidia maendeleo ya Taifa hili.

Alisema pamoja na kuanza fani hizo, alisema katika mipango ya muda mfupi chuo hicho kitaanza kutoa mafunzo ya elimu ya juu katika fani hizo kwa watu wa makundi maalum ambao ni walemavu kama wasiosikia, wasiosema na wenye matatizo tofauti.

Alisema kwa mujibu muongozo wa chuo hicho, kinapaswa kuwa na wanachuo wasiopungua 5000 kitakapokamilika kimejikita zaidi katika ufundishaji wa masomo ya juu kwa kiwango kizuri na bila ya kusahau suala zima la maadili ya umma.

Alisema kampasi ya chuo hicho inatarajia kujengwa katika eneo la Kazima, umbali kama wa kilomita nane kutoka mjini Tabora, ambapo kazi ya kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa wakimiliki eneo hilo ikiwa inaendelea.

Aliwataka wakazi wa Tabora kuwatambua na kuwathamini wanafunzi wa chuo hicho, hasa pale wanapotafuta makazi kwa ajili ya kusoma wasiwapandishie bei kwa kudhani kwamba wanapesa za kutosha hivyo kuwakwamisha kufikia malengo yao ya kielimu.

Alisema hao ni watoto wa masikini kama wao hivyo wanachopaswa kukifanya ni kuwasaidia na si kuwakomoa kwani kama tujuavyo kuwepo kwa wanachuo kutasaidia pia kukuza maendeleo katika mji huo kwa sababu mzunguuko wa pesa utaongezeka katika mji huo.

Mkuu wa Chuo, aliwataka wanachuo kusoma kwa bidii kubwa na kuhakikisha kuwa wanapata taaluma bora zaidi itakayowasaidia kupata uelewa mkubwa utakaosaidia kuwapa ushindani na kumudu kufanyakazi mahali popote katika ulimwengu bila ya kuathiri mila na desturi za wenyeji wao.

Sherehe hizo za ufunguzi wa chuo hicho zimehudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mji wa Tabora, viongozi wa chama Tawala na serikali, wabunge, maaskofu wa majimbo mbali mbali nchini na mapadri wanaoziwakilisha jumuiya mbali mbali katika jimbo Kuu la Tabora.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment