Shirika lisilo la kiserikali la mpango endelevu wa uboreshaji wa mazingira (SEMA), limetumia zaidi ya shilingi milioni 20 kugharamia ujenzi wa kituo cha ushauri na ujenzi wa vyoo bora (Sanitation Centre) kilichopo kata ya Mwakashanhala wilayani Nzega mkoa wa Tabora.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo hicho Mkuu wa wilaya ya Nzega Bituni Msangi amesema ni ukweli ulio wazi kwamba maisha ya mwanadamu na maendeleo yake, yanajengwa kwa kuboresha usafi wa mazingira.

Akifafanua zaidi, Msangi amesema usafi wa mazingira ni muhimu kwa usalama wa mwananchi yeyote.

Amesema mazingira machafu, yanapelekea maambukizi ya magonjwa ya matumbo, kipindupindu, kuhara, magonjwa ya minyoo, malaria na magonjwa ya macho. 

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Herman Materu, amesema kuyatibu maradhi hayo ni gharama kubwa ambayo inachangia au inapelekea jamii husika kuwa maskini.

Amesema siyo hivyo tu, magonjwa hayo wakati mwingine husababisha vifo ambavyo mazingira yangekuwa masafi, visingetokea.

Mkuu huyo wa wilaya, alitumia fursa hiyo kulishukuru na kulipongeza shirika la Water Aid kwa kufadhili mradi wa ujenzi wa kituo hicho na pia, amelipongeza shirika la SEMA kwa ujenzi bora wa kituo  hicho na kutoa mafunzo kwa mafundi ujenzi wa vyoo bora.

Awali Meneja wa SEMA Ivo Manyaku, alisema kituo hicho cha Mwakashanhala kinatarajiwa kitahudumia wakazi 18,287 wa kata hiyo na kata jirani.

Amesema gharama ya vyoo hivyo bora ni ya chini kwa vile vifaa vingi  vinavyotumika vinapatikana huko huko vijijini.

Kwa mfano,  amesema mfuko mmoja wa saruji ambao umechanganywa na udongo wa kisuguu, unatoa matofali bora, zaidi ya 120.